Zanzibar. Katika kampeni zake Dar es Salaam na Visiwani Zanzibar mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ametoa ahadi mbalimbali zinazolenga kuongeza kasi ya biashara na kukuza uchumi ikiwemo mageuzi mapya ya usafirishaji.
Samia ameahidi iwapo atachaguliwa kuendelea kuongoza nchi kwa kipindi kijacho atakamilisha miradi mikubwa itakayoongeza kasi ya biashara na kukuza uchumi wa Jiji la Dar es Salaam, ukiwamo wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) na kujenga Tanzania yenye uchumi Jumuishi.
Aidha, akiwa Visiwani Zanzibar, Samia amesema wataulinda Muungano kwa nguvu zote kwani una faida kwa pande zote mbili (Bara na Visiwani) huku akieleza chama hicho kikipewa ridhaa wataendeleza uchumi mkubwa na maendeleo jumuishi.
Ahadi nyingine aliyotoa ni maendeleo jumuishi yatakayomgusa kila Mtanzania na kuwa Samia na Dk Hussein Mwinyi kwa upande wa Zanzibar, wakipata ridhaa ya wananchi wataenda kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha huduma za kijamii ikiwemo elimu, maji, afya pamoja na umeme vinamfikia kila mtu.
Pia, amesema changamoto ya umeme Zanzibar watasimama imara kumaliza kadhia hiyo ili huduma hiyo ipatikane saa 24.
Kwa nyakati tofauti mgombea huyo ametoa ahadi binafsi na nyingine zilizopo kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2025/30 ikiwa ni kampeni za lala salama kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ambapo anatarajiwa kufunga kampeni wiki ijayo jijini Mwanza.
Samia ametoa ahadi hizo jijini Dar es Salaam katika wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke pamoja na viwanja vya Mnazi Mmoja, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar akitilia mkazo ujenzi wa viwanda, uboreshaji miundombinu ya usafiri na kuboresha huduma za jamii.
Samia amezungumzia kwa uzito mageuzi ya miundombinu Dar es Salaam, akisema ataboresha miundombinu ya barabara ikiwemo kujenga daraja la juu (fly over) katika Barabara ya Morocco, Mwenge hadi Magomeni na Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Umoja wa Mataifa ili kupunguza msongamano na kukuza shughuli za biashara katika jiji hilo.
Amesema kuhusu mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), tayari sekta binafsi imeshaanza kutoa huduma hiyo ya kusafirisha watu na kuwa kilomita 94.9 za barabara katika mradi huo tayari zimekamilika, ujenzi umefikia asilimia 61 na Sh2.1 trilioni zimetumika katika mradi huo.
Amesema akichaguliwa ujenzi wa awamu zote za mradi watasimamia na kuzikamilisha na mradi huo utatekelezwa na sekta binafsi na kuwahakikishia wana Dar es Salaam kuanzia Januari 2026 wataona mageuzi makubwa katika huduma hiyo.
“Sekta binafsi wataendesha mabasi hayo kupakia abiria, Kampuni ya ENG imeingiza mabasi 177, Kampuni ya YG Link ina mabasi 166, Kampuni ya Metro City ina mabasi 334 na Kampuni ya Mofat ina mabasi 255 yako njiani.
“Kuanzia Januari 2026 mtaona mageuzi makubwa katika kutoa huduma mabasi ya mwendokasi. Mradi huu hatua iliyofikia tuna sifa ya kimataifa, uwekezaji ndani ya Jiji la Dar es Salaam ni mkubwa na utaleta mapinduzi kwenye usafiri,” amesema.
Ameahidi uboreshaji na ujenzi mpya wa barabara za ndani jijini humo huku kuhusu adha ya mafuriko katika baadhi ya maeneo jijini humo ikiwemo maeneo yanayopakana na Mto Gide, Mto Mbezi na Mto China na kuwa changamoto hiyo itatatuliwa kupitia mradi wa pili wa uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam awamu ya pili (DMDP) pamoja na mifereji.
Kuhusu maji, Samia ameahidi Serikali itaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maji itakayohudumia mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro na Serikali itatekeleza mradi mkubwa wa kutoa maji Mto Rufiji ambao umelenga kumaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa maji hasa kipindi cha kiangazi jijini humo.
Amesema atahakikisha bwawa la Kidunda lenye thamani ya Sh336 bilioni unakamilika haraka ambao utasaidia kuondoa adha ya upatikanaji wa maji, huku akieleza Serikali yake imejipanga kuongeza nguvu katika utatuzi wa migogoro ya ardhi jijini humo na urasimishaji makazi.
Vilevile, ametaja mbali na uwezeshaji wananchi kiuchumi, pia Serikali yake imejikita kuweka nguvu kubwa katika kuboresha makazi ya watu.
Amesema jitihada za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) la kuendeleza miradi ya ujenzi wa makazi ya kudumu katika miji mbalimbali nchini, Samia amesema ajenda kuu ya eneo hilo ni kuhakikisha wananchi wanapata makazi ya kudumu.
Samia amesema Tanzania ina uhitaji wa nyumba milioni tano kila mwaka na kuwa Serikali yake itajenga nyumba 5,000 katika miji mbalimbali nchini ambazo ujenzi wake umeshaanza jijini Dar es Salaam.
Ameahidi pia kuboresha miundombinu ya usafirishaji mingine ikiwemo bandari, reli, anga, ujenzi wa masoko na stendi pamoja na huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo, elimu, afya, umeme na huduma zingine.
Akifunga kampeni visiwani Zanzibar kwa upande wa Muungano, Samia amesema wataenda kuulinda Muungano kwa nguvu zote kwani Muungano una faida kwa pande zote.
Amebainisha kuwa Serikali za CCM (Muungano na Zanzibar) zinathamini utekelezaji wa ahadi zinazotolewa na chama hicho na kuwa katika ilani inayoisha ya 2020/2025 kazi kubwa imefanyika.
Kuhusu uwezeshaji wananchi kiuchumi ameahidi wataendelea kutoa mitaji na fursa za kufanya biashara na kuwa wataweka nguvu kubwa ili vijana wajiajiri na kuendesha maisha yao.
“Katika kukuza uchumi mkubwa, pande zote mbili za Muungano tunafanya kazi kwa pamoja kukuza uchumi wetu mkubwa wa nchi na katika hili tumefanya kazi kubwa kuhakikisha vichocheo vya uchumi tunaimarisha ikiwemo usafiri na usafirishaji ambao ukikaa vizuri tutaimarisha biashara na uchumi,” amesema.
Mbali na ahadi za ilani ya 2025/2030, Samia amekuwa akisisitiza namna Serikali yake imejipanga kujenga Tanzania jumuishi huku akisisitiza amani, umoja na mshikamano wakati na baada ya uchaguzi mkuu.
