Bakwata Mara waandaa dua maalumu kuliombea Taifa amani

Musoma. Waumini wa dini ya kiislamu mkoani Mara wamefanya dua maalumu kuliombea Taifa amani keuelekea uchaguzi mkuu, huku waumini hao wakitakiwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, 2025.

Dua hiyo imefanyika mjini Musoma leo Oktoba 25, 2025 katika Msikiti Mkubwa wa Ijumaa ambapo Sheikh wa Mkoa wa Mara, Kassim Msabaha amewataka waumini na Watanzania kwa ujumla kuhakikisha siku ya uchaguzi wanawachagua viongozi wanao wataka.

Amesema dua hiyo maalumu imelenga kuombea amani na usalama ili nchi iendelee kuwa na amani kabla na baada ya uchaguzi, hali ambayo pamoja na mambo mengine itasaidia wananchi wote kuendelea na shughuli zao za maendeleo pamoja na uwezo wa kufanya ibada na kuabudu.

Amesema amani na utulivu wa nchi ni msingi wa kila kitu, hivyo wadau wote wanapaswa kuungana kwa pamoja kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na utulivu hata baada ya uchaguzi.

“Uchaguzi sio sababu ya kupoteza amani yetu, Watanzania tunapaswa kuilinda amani hii kwa wivu mkubwa na kama kuna yeyote ambaye hataki amani, basi yeye aondoke aende kwenye nchi ambayo haina amani kwani zipo nchi nyingi tu hazina amani labda huko patamfaa sisi tunataka amani yetu na tumeizoea,” amesema.

Amesema wapo baadhi ya watu wanaodai kuwa dua hiyo inalenga kufanya kampeni kwa baadhi ya wagombea, jambo ambalo amesema halina ukweli wowote na ndio maana amewataka waumini kuchagua viongozi wanaowataka kwa ustawi wa nchi na si vinginevyo.

“Nasisitiza neema ya amani ni tunu muhimu sana kuna mataifa huko wanatutamani kwani awali hawakuona umuhimu wa kuwa na amani, sasa wameichezea na imetoweka sisi tumezoea amani na bado tunaitaka amani,” amesema.

Amewataka waumini wa dini hiyo kila mmoja kwa wakati wake kumuomba Mungu aweze kujalia uchaguzi ufanyike na kuisha kwa amani na usalama.

Sheikh Msabaha pia amewataka watanzania kujipeusha na ushawishi unaofanywa na baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii, badala yake wahakikishe uchaguzi unawaacha Watanzania wakiwa salama na wenye mahusiano mazuri baina yao.

Katibu wa Baraza la Waislamu (Bakwata) Mikidadi Shada amesema dua maalumu ya kuliombea Taifa zimefanyika katika wilaya zote za mkoa wa Mara.

“Hizi dua tumeandaa kwa mkoa mzima kwani tumeona ipo haja ya sisi kama taasisi ya dini kushiriki katika suala zima la uendelevu wa amani iliyopo nchini amani ambayo tuna wajibu wa kuilinda kama watanzania,” amesema.

Amesema wameratibu dua kwa ajili ya kuombea nchi amani katika misikiti yote mkoani Mara kwa maelezo kuwa kila Mtanzania ana haki na wajibu wa kuhakikisha amani inadumu.

Baadhi ya waumini wamesema suala la amani ni la kila Mtanzania bila kujali itikadi ya kisiasa wala dini na kwamba Watanzania wote kwa pamoja, wanapaswa kuepukana na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi.

“Tukiwa tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu yapo mambo mengi sana lakini amani ni kitu muhimu sana, amani ndio nguzo ya taifa letu,tumezoea amani tunataka amani iendelee,” amesema Salma Mrisho.

Juma Masirori amesema suala la kuiombea nchi ni la muhimu katika kipindi hiki huku akiwataka watanzania kujitokeza na kuwachagua viongozi watakao kuwa mstari wa mbele kupambania maslahi ya umma wa Watanzania.