BITEKO AHITIMISHA KAMPENI ZA UBUNGE CHATO KUSINI NA AHADI RUKUKI

 …………….

CHATO 

NAIBU Waziri mkuu Dkt. na Waziri wa Nishati, Doto Biteko, amehitimisha kampeni za Uchaguzi wa Jimbo la Chato kusini, huku akitoa ahadi nyingi kwa wananchi wa Jimbo hilo iwapo Oktoba 29,2025 watawachagua wagombea wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hatua hiyo imefikiwa zikiwa zimesalia siku nne kufanyika kwa Uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani mwaka 2025.

Akiwa katika wa mkutano wa kuhitimisha kampeni za Jimbo hilo ziliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Bwanga, Dkt. Biteko amemtaja mgombea wa Jimbo hilo kuwa ni mchapa kazi na mwenye kukerwa na shida za wananchi.

Amesema Paschal Lutandula, ni mtu mnyenyekevu, muadilifu na mwenye kutaka kutatua changamoto za wananchi wake, na kwamba miongoni mwa majimbo yaliyopata mtu sahihi ni Jimbo la Chato kusini.

Aidha Dkt. Biteko amesema changamoto za wananchi wa Jimbo hilo kuhusiana na maeneo ya kulima tayali zimeshapokelewa na Rais Samia Suluhu Hassan alipofika mjini Chato kuomba kura kwa wananchi.

Hata hivyo amewataka wananchi wa Jimbo hilo, kuwapigia kura nyingi wagombea wote wa CCM ili kumshawishi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuharakisha maendeleo ya Jimbo hilo jipya.

Awali katika mkutano huo, mgombea wa Jimbo la Chato kusini, Paschal Lutandula, ametumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi wa Jimbo hilo kutokana na mwitikio mkubwa wa kumsikiliza wakati wote wa kampeni zake.

Amesema baada ya kuzindua kampeni zake Septemba 25 mwaka huu, jumla ya vijiji 59 na vitongoji 264 ameitembelea na kuzungumza na wananchi mbalimbali wakiwemo Wakulima, wafugaji, Wafanyabiashara, Wavuvi, Waganga wa Jadi, Wachungaji pamoja na Mashekhe.

Hata hivyo Lutandula, hakuacha kuwazungumzia wananchi wa Matabe, mchangani na Ipembelang’ombe ambao wamekuwa wakililia maeneo ya kulima kutokana na maeneo yao ya awali kutwaliwa na Wakala wa huduma za misitu nchini(TFS).

Vilevile amewakumbusha wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, mwaka huu ili kutimiza haki yao ya msingi ya kuwapigia kura wagombea wa CCM ili waweze kuleta maendeleo ya kweli.

                          Mwisho.