Chadema yaeleza Heche anashikiliwa Dodoma, ahojiwa na Uhamiaji

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimedai Makamu Mwenyekiti Taifa wa chama hicho, John Heche anashikiliwa katika mahabusu ya Jeshi la Polisi Mtumba, jijini Dodoma.

Chadema katika taarifa kwa umma iliyotolewa jana ljumaa, Oktoba 24, 2025 kimesema Heche anashikiliwa na polisi katika mahabusu hiyo, lakini hakuna mamlaka ya jeshi hilo iliyozungumzia taarifa hiyo.

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia aliyesaini taarifa hiyo, vilevile amesema jana Oktoba 24, Heche alihojiwa na Idara ya Uhamiaji mbele ya wakili wa chama hicho na kaka yake.

Vilevile, ameeleza kwamba alihijiwa kuhusu kuvunja sheria za uhamiaji kwa kuvuka mpaka wa Tanzania na kuingia nchini Kenya bila kufuata taratibu.

“Pamoja na kosa hilo alilotajiwa ambalo lina dhamana, Jeshi la Polisi limekataa kumpa dhamana…” inadai taarifa hiyo.

Hata hivyo, juhudi za kumpata msemaji wa Uhamiaji kuzungumzia suala hilo haikuzaa matunda.

Heche alikamatwa na Polisi Jumatano Oktoba 22, kwenye geti la Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.

Chadema inadai baada ya Heche kukamatwa alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, kisha jeshi hilo likasema linamsafirisha kumpeleka Tarime mkoani Mara.

Kwa mujibu wa Chadema, kuendelea kushikiliwa Heche ni kinyume cha sheria, na mwendelezo wa mpango wa kuwakamata viongozi wakuu wa chama hicho mpaka baada ya uchaguzi.

Kabla Heche hajakamatwa, Idara ya Uhamiaji Makao Makuu ilitoa taarifa ikidai alivuka mpaka kinyume cha sheria, madai ambayo Heche alikanusha, akisema alikamatwa mpakani wa Sirari akiwa anataka kuvuka kwenye Kenya kwenda kwenye maziko ya Raila Odinga, akiwa amefuata taratibu.

Taarifa ya uhamiaji ilieleza: “Oktoba 18, 2025 katika Kituo cha Uhamiaji cha mpaka wa Sirari mkoani Mara, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Heche) ameondoka nchini kwa kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani bila kufuata taratibu na kanuni za uhamiaji.”

“Idara ya Uhamiaji inatoa wito kwa raia wa Tanzania na wageni wote wanaotoka na kuingia nchini kufuata taratibu na kanuni zinazoongoza uingiaji, ukaazi na utokaji wa watu nchini ili kuepuka kutenda kosa na kuchukuliwa hatua za kisheria,” ilieleza taarifa hiyo.

Akizungumza na Mwananchi Oktoba 19, Heche alisema hakusafiri kwenda Kenya. Alidai pasipoti yake ilichukuliwa na kuwa wakati akizungumza na gazeti hili saa 5:39 asubuhi alikuwa kijijini kwao Tarime.

Alidai zuio la kusafiri ni la kisiasa na siyo mambo ya kutofuatwa kwa utaratibu kama taarifa ya msemaji wa uhamiaji ilivyoeleza.

“Hapa Sirari kuingia Kenya hakuna ukuta, ni kwetu, nazifahamu njia zote kama ningetaka kuingia bila kufuata utaratibu ningepita njia za panya, kunizuia nisisafiri ni masuala ya kisiasa tu.”

Oktoba 23, 2025, familia ya Heche iliyopo Kijiji cha Ketagasembe, Wilaya ya Tarime, ilitoa muda wa siku moja ielezwe ndugu yao yuko wapi.

Chacha Heche, mdogo wake na kiongozi huyo wa Chadema alisema:

“Ndugu yetu hawezi kufa kama kuku. Ikifika kesho sisi tutaandika wosia kwa watoto wetu, tuko tayari kufa kwa ajili yake. Hawezi kufa peke yake, tunataka kujua yuko wapi hadi sasa kwani tuna wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wake na afya yake.”

Chacha alisema ndugu yao ana mfumo tofauti wa maisha kutokana na masuala ya usalama na afya yake, hivyo kushikiliwa kwa muda mrefu bila kujua alipo ni hatari kwa maisha yake.