Bagamoyo. Mgombea mwenza wa urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Devotha Minja amefanya mkutano wa hadhara katika soko la Magomeni, Bagamoyo, mkoani Pwani akiahidi kufufua mradi wa Bandari ya Bagamoyo uliokwama kwa miaka mingi.
Akihutubia wananchi waliokusanyika kusikiliza sera za chama hicho, mgombea mwenza huyo amesema kuwa bandari hiyo ni injini ya maendeleo ambayo imeachwa kufa kutokana na ubinafsi na uzembe wa wanasiasa.
“Kumekuwa na wazo la kuwa na bandari kubwa hapa Bagamoyo lakini imeshindwa kutanuliwa kwa miaka mingi.
“Wataalamu walisema bandari hii ingeweza kujenga viwanda 80 na kutoa ajira zaidi ya 2,000. Miaka yote CCM wanaleta porojo. Tupeni Chaumma, tutahakikisha tunapata wawekezaji wazuri wasioiumiza nchi, tujenge bandari kubwa Bagamoyo,” amesema.
Ameongeza kuwa ujenzi wa bandari hiyo utasaidia kupunguza mzigo katika Bandari ya Dar es Salaam na kufungua fursa mpya za uchumi kwa mikoa ya Pwani na nchi jirani.
“Bandari hii ikijengwa itaharakisha uchumi wa Mkoa wa Pwani na maeneo yote ya jirani. Wakati sisi tunapata uhuru, Korea Kusini ilikuwa na uchumi sawa na wetu. Leo ni taifa tajiri kwa sababu walijenga bandari kubwa miaka ya 80. Chaumma mkituchagua, tutaharakisha ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo tujenge uchumi wa Bagamoyo na wa taifa letu,” ameongeza.
Mgombea mwenza huyo pia amelalamikia hali ya ajira nchini, akisema vijana wameelemewa na umasikini licha ya kuwa na elimu za vyuo vikuu.
“Leo madaktari hawatoshi, walimu hawatoshi, lakini vijana wamesoma hadi vyuo vikuu wako majumbani wanaishi na wazazi. Serikali haiwapi ajira. Miaka 64 ya Chama cha Mapinduzi inatosha, twendeni tukaipumzishe CCM,” amesema.
Amegusia pia ubovu wa huduma za afya nchini, akisema wagonjwa wengi hawapati matibabu kwa gharama nafuu na familia zinahangaika hata katika shughuli za mazishi.
“Huduma za afya zimekuwa mbovu sana, kila kitu gharama kubwa, hadi kukomboa mwili wa marehemu hospitalini ni mzigo. Huu ni wakati wa mabadiliko,” amesema.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo la Bagamoyo, Zaituni Rungwe amewataka wana Bagamoyo kujitambua na kupiga kura ya ukombozi.
Zaituni amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ifikapo Oktoba 29, akiahidi kupambana na changamoto za mikopo na ajira kwa vijana.
“Ndugu zangu wa Bagamoyo, ifike wakati mjitambue. Oktoba 29, nendeni mkanichague ili niwasaidie kuondoa kero za mikopo na maandiko yasiyoeleweka mnayoletwa bila mchanganuo. Tukiamua kwa umoja, tutabadilisha Bagamoyo,” amesema.
Ameonya dhidi ya siasa za hongo na ahadi hewa, akiwataka wananchi kuchagua viongozi wa Chaumma watakaokuwa karibu na wananchi.
“Achaneni na wagombea wanaowadanganya. Ofisi yangu itakuwa wazi kila siku kuanzia asubuhi hadi saa nne, nikiwasikiliza wananchi wangu. Hiyo ndiyo maana ya uongozi wa uwazi,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chaumma Wilaya ya Bagamoyo, Selemani Boyi, amewataka wananchi kuachana na tamaa ya zawadi ndogo zinazotolewa na wanasiasa wasiokuwa waaminifu.
“Ndugu zangu wa Kata ya Nianjema badilikeni. Acheni kudanganyika na vitenge na vinywaji. Viongozi wa kweli hawatoi zawadi, wanatoa dira. Mpeni kura Zaituni Rungwe, anatufaa sisi sote,” amesema.
Boyi amesitiza kuwa Chaumma ni chama cha matumaini mapya, kinachojali maendeleo ya watu kuliko maslahi ya wachache.
Mkutano huo pia umehudhuriwa na wagombea udiwani waliotumia nafasi hiyo kuomba kura kwa wananchi wa kata zao.
Mgombea udiwani wa Kata ya Nianjema, Mamwiso Selemani, ameahidi kupigania masilahi ya wafanyabiashara wa soko la Magomeni, akisema soko hilo limepangwa kuondolewa kinyume cha matakwa ya wananchi.
“Fanyeni mabadiliko mwaka huu, acheni kutishwa eti kutakuwa na vita. Hakuna vita ya kura, ni vita ya maendeleo. Kapigeni kura mchague viongozi wa Chaumma,” amesema.
Ameahidi pia kuboresha miundombinu ya barabara katika kata hiyo ambayo imekuwa kero kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Kilomo, Haruna Banda, amewahimiza vijana kujitokeza kupiga kura ili kupinga mifumo kandamizi.
“Mwalimu Nyerere alitufundisha kuwa waasi dhidi ya mifumo kandamizi. Vijana wenzangu, tusikubali kunyanyaswa. Oktoba 29, jitokezeni mkatuchague viongozi wa Chaumma,” amesema.
