Ukerewe. Dk Emmanuel Nchimbi amehitimisha safari ya siku 57 za kusaka ushindi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchi nzima kwa kuwaahidi wananchi wa visiwani Ukerewe ujenzi wa kiwanda cha kuchakata samaki na mazao yake.
Pia, ujenzi wa soko la kisasa, barabara, shule za msingi na sekondari, nyumba za watumishi, kuboresha huduma za afya, maji na kuwawezesha wavuvi kwa zana za uvuvi ni miongoni kwa ahadi zitakazotekelezwa miaka mitano ijayo iwapo kitaibuka na ushindi.
Dk Nchimbi ambaye ni mgombea mwenza wa urais, alianza kampeni zake Agosti 29, 2025 katika majimbo mbalimbali Mwanza na amehitimisha leo Jumamosi, Oktoba 25, 2025 visiwani Ukerewe, mkoani humo.
Uzinduzi wa kampeni za CCM kitaifa zilifanyika Agosti 28, 2025 Uwanja wa Tanganyika Packers, jijini Dar es Salaam ukiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan na kuhudhuriwa na watu mbalimbali.
Baada ya uzinduzi huo, Samia ambaye ni mgombea urais na Dk Nchimbi, waligawana mikoa kwenda kunadi ilani ya uchaguzi 2025/2030 ambapo Dk Nchimbi yeye alianzia Mwanza na Samia akiwa Morogoro.
Dk Nchimbi amehitimisha kampeni mkoani humo sawia na Samia ambaye naye Jumanne ya Oktoba 28, 2025 atafunga kampeni zake Mwanza.
Agosti 28 hadi leo Oktoba 25, 2025 ni sawa na siku 57 ambazo Dk Nchimbi amezitumia kufanya mikutano nchi nzima ikiwemo Zanzibar kuomba kura za Samia za urais, wabunge na madiwani katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.
Katika mkutano wa leo Jumamosi, uliofanyikia Nansio, Ukerewe, uliofanyika wakati mvua ikinyesha, Dk Nchimbi ameeleza mafanikio ya miaka mitano iliyopita kwenye sekta mbalimbali na yale yatakayofanyika mitano ijayo endapo Samia atachaguliwa.
“Kwenye eneo la uvuvi, tumesema katika miaka mitano inayokuja, kwanza tunahakikisha tunaenda kujenga soko la kisasa la samaki Ukerewe. Lakini pia, tutakwenda kujenga kiwanda cha kuchakata samaki na mazao yake Ukerewe.
Kiwanda hiki cha samaki kitahusika pia na kukausha dagaa wetu,” amesema Dk Nchimbi.
Amesema ndani ya miaka mitano inayokuja, CCM imeweka mkakati wa kutoa mafunzo kwa wavuvi ili wavue na kufanya biashara kisasa.
“Miaka mitano ijayo, Serikali ya CCM Itaimarisha utoaji wa zana za kilimo, na zana za uvuvi kwa maana ya mitumbwi na boti,” amesema.
Mgombea mwenza huyo amesema wataboresha masoko katika soko la Nansio kwa kutengeneza vibanda zaidi ya 98 katika soko la Katunguru, vibanda 37 soko la Sungura, vibanda 63 soko la Getrude Mongela pamoja na kuboresha stendi yetu iwe ya kisasa zaidi.
Kwenye nishati, Dk Nchimbi ameahidi ndani ya miaka mitano hakuna kitongoji cha Ukerewe kitakachokuwa hakijafikiwa na umeme. Pia, ujenzi wa vituo viwili vya afya na kukamilisha zahanati 16 zinazoendelea kujengwa.
Dk Nchimbi ameahidi ujenzi wa barabara mbalimbali za Ukerewe zikiwemo za lami, kuboresha upatikanaji wa maji kwa wananchi pamoja na ujenzi wa shule za msingi, sekondari na madarasa kwa shule za zamani.
Awali, mgombea ubunge wa Ukerewe, Dk Swetbert Mkama amesema Sh25 bilioni zilitolewa ili kujenga Hospitali ya Rufaa ngazi ya Mkoa katika Wilaya ya Ukerewe. Pia, wanapata umeme toka gridi ya taifa.
Aidha, amesema Serikali ya CCM chini ya Rais Samia ilitoa Sh11 bilioni kutengeneza vivuko viwili kati ya vinne: “Sasa hivi viko tayari na muda wowote vitaanza kufanya kazi hapo na kupunguza changamoto ya usafiri katika Wilaya yetu.
“Lakini, katika kipindi hiki cha miaka mitano ijayo kwa mara ya kwanza Ukerewe tunapata kilomita nyingi za barabara ya lami. Lami ilianza kujengwa Ukerewe miaka 35 iliyopita, lakini hadi tunafika leo tuna kilometa saba za barabara kuu na kilometa tatu za barabara za mjini,” amesema.
Mbali na kueleza mafanikio mbalimbali, Dk Mkama amewasilisha maombi kwa Dk Nchimbi akisema: “Tuliahidiwa kujengewa vivuko vinne viwili vimekamilika. Viwili bado na hivyo ambavyo bado ndio vinavyohudumia visiwa vingi zaidi. Kwa hiyo tunaviomba.
“Ombi la pili, Kuna barabara ya kutoka Goma kuja Nansio kilometa kumi. Mkandarasi alikuja kubomoa nyumba za watu, akakata na maji kwenye nyumba za watu, alipomaliza akaingia mitini hatujamwona mpaka leo. Miaka mitatu sasa tunataka arudi aje akamilishe.”
