EAC watuma kikosi kazi kufuatilia mwenendo wa uchaguzi nchini

Arusha. Uongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imetuma wajumbe wa uangalizi wa Uchaguzi (EOM) 67 nchini kwa ajili ya kufuatilia mwenendo mzima wa uchaguzi na kusaidia kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unakuwa huru, wa haki na unaoendana na kanuni za kidemokrasia.

Waangalizi hao kutoka nchi za EAC wanakuja kutekeleza majukumu hayo wakati Tanzania ikiwa imebakiza siku tatu pekee, kufanyika kwa uchaguzi wa kitaifa kwa nafasi ya Rais wa nchi, wabunge na madiwani kote nchini.

Wajumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa EAC unajumuisha wataalamu 67 kutoka nchi zote wanachama, wakiwemo Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), maofisa wa Tume za Taifa za Uchaguzi, Tume za Haki za Binadamu, wawakilishi wa Asasi za Kiraia na watumishi wa Sekretarieti ya EAC.

Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva akizungumza katika hafla hiyo

Waangalizi hao wamepelekwa katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania kufuatilia mchakato wa uchaguzi kwa mujibu wa sheria za nchi, Kanuni za EAC za Uangalizi na Tathmini ya Uchaguzi, pamoja na viwango vingine vinavyokubalika kimataifa.

Akizungumza wakati wa kutambulisha wajumbe hao, jana Octoba 24, 2025 ndani ya makao makuu ya EAC jijini Arusha, Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva amesema wajumbe hao watatoa taarifa ya awali muda mfupi baada ya uchaguzi, ikifuatiwa na ripoti ya mwisho yenye mapendekezo ya kuboresha chaguzi zijazo katika nchi za ukanda huo.

“Waangalizi wetu watawasiliana na wadau muhimu, kufuatilia kampeni, na kushuhudia upigaji kura, kuhesabu na utangazaji wa matokeo ili kuhakikisha uwazi na uaminifu, unakuwepo,” amesema.

Katibu Mkuu wa wajumbe hao, Maina Karobia, Mbunge wa Afrika Mashariki (EALA), amesema kuwa jukumu la wajumbe ni kutokuegemea upande wowote.

“Tupo hapa kwa mshikamano na wananchi wa Tanzania,” amesema na kuongeza, “Hatupo kuingilia, bali kufuatilia na kuripoti kwa uadilifu.”

Ametumia nafasi hiyo kuwataka wadau wote wa uchaguzi kudumisha amani na uadilifu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.

Wajumbe wa EAC wanaunganisha nguvu na taasisi zingine za kikanda na kimataifa, zikiwemo Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), na Jumuiya ya Madola (Commonwealth), ambazo pia zimetuma waangalizi wake kwa uchaguzi huo.

Wajumbe hao wanaongozwa na Mwenyekiti Dk Speciosa Kazibwe, aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa Uganda na mtetezi mashuhuri wa afya ya umma na usawa wa kijinsia.

Dk Kazibwe ndiye mwanamke wa kwanza barani Afrika kushika wadhifa wa Makamu wa Rais katika nchi huru na aliwahi pia kuwa Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukimwi barani Afrika.

“Kama Jumuiya inayojengwa juu ya misingi ya utawala bora, heshima kwa sheria na haki za binadamu, EAC inaona uchaguzi huru na wa haki kuwa nguzo muhimu ya demokrasia na ujumuishaji wa kikanda,” amesema Dk Kazibwe.

Kwa mujibu wa Ibara ya 6(d) ya Mkataba wa EAC, uangalizi huu unaimarisha wajibu wa Nchi Wanachama katika kuendeleza utawala bora, uwajibikaji, usawa wa kijinsia, na heshima kwa haki za binadamu misingi iliyowekwa ndani ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu.