UNAWEZA kudhani kama masihara, lakini ukweli ni kwamba kadi nyekundu aliyoonyeshwa Ramadhan Chalamanda wa JKT Tanzania dhidi ya Mbeya City, inafanana na ile aliyowahi kuonyeshwa dhidi ya timu hiyo misimu miwili iliyopita.
Chalamanda ambaye ameingia JKT Tanzania msimu huu akitokea Kagera Sugar, alionyeshwa kadi hiyo dakika ya 17 katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Uwanja wa KMC Complex, Dar na kumalizika kwa sare ya 2-2.
Tukio la kadi hiyo nyekundu juzi, lilitokana pasi aliyorudishiwa Chalamanda kwa kichwa kuwa fupi ambapo kipa huyo alikuwa ametoka eneo lake, mshambuliaji wa Mbeya City, Vitalis Mayanga akauwahi, wakati anajaribu kufunga, ndipo Chalamanda akauzuia mpira huo kwa mikono akiwa nje ya boksi, mwamuzi Raphael Ikambi akamuonyesha kadi nyekundu.
Hiyo ilitokea ikiwa ni baada ya dakika 14, Hamad Majimengi kuifungia Mbeya City bao la kwanza akimalizia pasi ya Omar Chibada. Tukio kama hilo, lilitokea misimu miwili tena dhidi ya Mbeya City.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chalamanda amesema, Mbeya City imekuwa timu ambayo inampa wakati mgumu kwani kwenye maisha yake ya soka amepata adhabu ya kadi nyekundu mara mbili alizocheza na kikosi hicho.
Amesema kuwa, anajisikia vibaya kwa adhabu hiyo kwani itamfanya awe nje kwenye mechi ijayo, kwa sababu hatamani kukosa mchezo wowote.
“Mchezo wa kwanza misimu miwili iliyopita dhidi ya Mbeya City nilionyesha kadi nyekundu, wakati niliporudishiwa mpira ukawa mfupi nilipojaribu kuufuata mshambuliaji wa Mbeya wakati huo Tariq Seif Kiakala, akanizidi akili na kuuwahi, nilipomvuta nikapewa red card (kadi nyekundu).
“Jana (Juzi) nikarudishiwa mpira, lakini nilipokuwa nataka kuuwahi mshambuliaji Vitalis Mayanga akanizidi akili nikaucheza mpira nje ya eneo langu, nikapewa red (nyekundu).”
Aliongeza kuwa, “nimeumizwa na hali hiyo lakini ndio mambo ya soka, nilikuwa nataka kuzuia timu yangu isiruhusu bao lingine, ligi ni ngumu mechi zetu zimekuwa kali sana kwa hiyo tunajipanga tusiendelee kuangusha pointi.”
