Bukoba. Mahakama Kuu imeliamuru Jeshi la Polisi nchini, kuwaachia huru watuhumiwa saba inaowashikilia nje ya saa 24 za kisheria, akiwamo Mwenyekiti wa Chadema Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, Chief Adronicus Kalumuna.
Katika uamuzi wao, majaji kwa nyakati tofauti wamesema kutoheshimiwa kwa sheria hakuvumiliki, wakinukuu ibara ya 15(1) na (2) ya Katiba ya Tanzania inayokataza mtu kukamatwa na kuzuiwa pasipo kufuata sheria za nchi.
Amri hizo zimetolewa na majaji wawili wakati wanatoa uamuzi wa maombi ya shauri la kutaka wanaoshikiliwa wafikishwe kortini (habeas corpus) yaliyowasilishwa kortini na washtakiwa kupitia mawakili wao, Pereus Mutasingwa na Derick Zephrine kwa hati ya dharura.
Maombi hayo namba 25281 na 25115 ya mwaka 2025 yalikuwa dhidi ya Mkuu wa Kituo cha Polisi (OCS) Bukoba, Mkuu wa Upelelezi wa Jinai (RCO) Mkoa wa Kagera, Kamanda wa Polisi (RPC) Mkoa wa Kagera na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP).
Pia walimuunganisha Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) kama mjibu maombi wa tano katika maombi hayo yaliyowasilishwa kwa hati ya dharura.
Maombi namba 25115 ya 2025, yalifunguliwa na Kalumuna, Daniel Rwebugisa, Paulo Musisi, Revocatus Nkesha na Egbert Kikarugaha wakati kwa maombi namba 25281 yalifunguliwa na Baziri Waziri na Rashidi Hamza.
Uamuzi wa maombi hayo ulitolewa Oktoba 23, 2025 na majaji Lilian Itemba aliyesikiliza maombi namba 25115 na Jaji Gabriel Malata aliyesikiliza maombi namba 25281, wote wakiwa majaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Bukoba.
Katika uamuzi uliowekwa kwenye tovuti ya mahakama Oktoba 24, 2025, majaji hao wameamuru watuhumiwa wanaoshikiliwa mahabusu waachiwe huru au wafikishwe mahakamani si zaidi ya Oktoba 24, ambayo ni jana.
Kwa mujibu wa kiapo cha Yusuph Abdalah, ambaye ni kaka wa Kalumuna, Oktoba 12, 2025, saa 4:00 usiku, maofisa wa Polisi waliokuwa na silaha walivamia nyumba ya Kalumuna wakamshambulia na kuondoka naye.
Alidai kila aliyejaribu kuingilia kati naye alipigwa, kisha maofisa hao walimbeba Kalumuna na kumwingiza kwenye gari na kumpeleka Kituo cha Polisi Bukoba alikowekwa mahabusu.
Siku iliyofuata mchana, mleta maombi wa pili hadi wa tano ambao ni Rwebugisa, Musisi, Nkesha na Kikarugaha walifuatilia sababu za kukamatwa kwa Kalumuna lakini nao wakaishia kuwekwa mahabusu.
Alieleza wajibu maombi wamezuia waleta maombi kupata haki yao ya kujulishwa kosa na kupewa haki ya kuwajulisha mawakili wao, jambo ambalo ni ukiukwaji wa misingi ya haki jinai.
Katika maombi namba 25281 ya 2025, waleta maombi (Waziri na Hamza), wanaeleza walikamatwa na Polisi kwa nyakati tofauti Oktoba 14, 2025 katika maeneo yao ya biashara yaliyopo Kijiji cha Nkwenda, wilayani Kyerwa.
Walichukuliwa kwa gari aina ya Toyota Land Cruiser, hivyo ndugu wakiwa na gari aina ya Toyota Premio waliwafuatilia na kuwakuta mahabusu ya Kituo cha Polisi Bukoba, bila kuwaeleza sababu.
Wakiwa kituoni wakisubiri kuonana na mjibu maombi wa pili ambaye ni RCO Kagera, walidai walitishwa na kutakiwa kukaa mbali, vinginevyo nao wangekamatwa.
Mawakili katika kesi hiyo walinukuu kifungu cha 33 na 34 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA). Kifungu cha 34 kinataka mshukiwa wa uhalifu afikishwe katika mahakama ya karibu ndani ya saa 24.
Pia, walinukuu ibara ya 15(2) ya Katiba inayosema: “Itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kukamatwa, kufungwa, kufungiwa, kuwekwa kizuizini, kuhamishwa kwa nguvu au kunyang’anywa uhuru wake isipokuwa tu kwa kufuata sheria.”
Wajibu maombi walivyojibu
Katika majibu ya wajibu maombi kupitia kiapo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Boniphace Mayala, ambayo yana maudhui yanayofanana katika maombi hayo, alieleza waleta maombi wanatuhumiwa kwa uchochezi katika maeneo mbalimbali nchini kupitia vyombo vya habari.
Alieleza upelelezi ulikuwa unaendelea na kwamba, waombaji hao ndio ambao wanasaidia upelelezi ili kupata ushahidi katika mikoa mbalimbali nchini na kuachiwa kwao kutaingilia mchakato wa upelelezi.
Katika uamuzi kuhusu maombi ya Waziri na Hamza, Jaji Malata amesema hakuna ubishi kuwa waleta maombi walikamatwa na wajibu maombi Oktoba 14, 2025 na bado wako mahabusu kwa siku ya nane hadi anatoa uamuzi wake.
Amesema ni jambo lisilobishaniwa pia kuwa waleta maombi walikuwa hawajafikishwa kortini na kwamba, wajibu maombi wanasema kukamatwa kwao kunahusiana na kuhamasisha kutendeka kwa kosa la uchochezi maeneo mbalimbali.
Akinukuu ibara ya 15(1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji Malata amesema kifungu hicho ni ushahidi kuwa masuala yote yanayohusiana na kukamata na kumweka mtu chini ya ulinzi lazima yafanywe kwa mujibu wa sheria.
“Kwa maneno mengine, ni sahihi kumkamata na kumweka mtu chini ya ulinzi lakini utaratibu huo lazima ufanywe kwa mujibu wa sheria kwa sababu nzuri. Kama kuna hatua za kufuata ni lazima zifuatwe,” amesema.
Amesema katika maombi hayo, wajibu maombi waliwakamata waombaji Oktoba 14, 2025 kuhusu makosa ya uchochezi kupitia vyombo vya habari na kwamba, walitumia mamlaka yao waliyopewa na CPA kama ilivyorejewa mwaka 2023.
“Lakini baada ya kuwakamata waombaji, wajibu maombi wana wajibu wa kufanya kitu kwa mujibu wa sheria? Au sheria hiyo inawapa mamlaka ya kuwakamata na kuendelea tu kuwashikilia watuhumiwa,” ameeleza.
Amerejea kifungu cha 34 cha CPA kinachosema kadri iwezekanavyo, mtuhumiwa afikishwe kortini ndani ya saa 24, hata kama mtu alipewa dhamana au hajapewa na kusisitiza Polisi hawana mamlaka ya kukaa nao zaidi ya muda huo.
“Kisheria walalamikiwa hawana mamlaka ya kuwashikilia waombaji kwa muda mrefu bila kuwafikisha mahakamani. Tuna wajibu wa kuhakikisha kuwa kila mamlaka, wakiwamo wajibu maombi wanazingatia sheria katika utendaji wao,” amesema na kuongeza:
“Kinyume chake, nchi itakabiliwa na kukithiri kwa matumizi holela ya madaraka waliyokabidhiwa, hivyo kupoteza maana na mantiki ya kuwa na utawala wa sheria katika nchi yetu.”
Jaji amesema mahakama inaona kuwa wajibu maombi wanabanwa na Katiba na sheria kuhakikisha wanawapeleka watuhumiwa mahakamani ili kuacha taratibu zingine za upelelezi zikiendelea kufanywa na Jeshi la Polisi.
Kwa upande wake, Jaji Itemba amerejea ibara ya 15 ya Katiba na kifungu namba 34 cha CPA, akisema hakuna ubishi kuwa Kalumuna na wenzake wanne walikuwa wanashikiliwa na Polisi tangu walipokamatwa Oktoba 12 na 13, 2025.
“Kwa mujibu wa vitabu vya sheria, waombaji walipaswa kuachiwa kwa dhamana au kushtakiwa mbele ya mahakama ya sheria. Kutofuatwa kwa sheria hakuvumiliki na hakuna maelezo mazuri ya kuokoa hali hiyo,” amesema na kuongeza:
“Tuhuma hizi ambazo hazina ubishi ni nzito na mahakama haiwezi kuzichukulia kirahisi tu. Jeshi la Polisi ni chombo chenye jukumu la kulinda amani na utulivu na si kukamata watu ovyo kwa matakwa yao.”
Jaji amesema anaona ni vigumu kukubaliana na maelezo ya wajibu maombi kwamba, waombaji wako chini ya kizuizi cha muda mrefu kwa sababu wanasaidia uchunguzi na ikiwa wako huru, wanaweza kuingilia au kuharibu upelelezi.
Ni kutokana na uchambuzi huo, majaji wote wawili wametoa amri kuwa ama waombaji waachiwe huru kutoka kizuizini au kama itahitajika, basi wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma zao siyo zaidi ya Oktoba 24, 2025.
Polisi wakiri kuwashikilia
Siku mbili baada ya hukumu hiyo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa Kagera, Brasius Chatanda amezungumza na vyomba vya habari na kusema ni kweli wanawashikilia viongozi wanne wa chama hicho na wananchama makada wake watatu kwa tuhuma za kuhamasisha uchochezi wa kuandaa maandamano.
“Ni kweli hao viongozi tunawashikilia wakiwa na wanachama wao watatu tuhuma ni uchochezi wa kuhamasisha maandamano na ni miongoni mwa watu 17 tunaowashikilia katika kipindi hiki chote cha kampeni za uchaguzi,” amesema.
Amesema mpaka sasa hajapokea barua kutoka mahakamani kuhusu washtakiwa kufikishwa mahakamani na suala hilo si la Jeshi la Polisi, kwa sababu kazi yao ni kukamata na kufanya upelelezi kisha kuandaa jalada.
