SAN FRANCISCO, MAREKANI : TIMU za Golden State Warriors na Denver Nuggets zilianza msimu huu zikiwa na lengo moja tu kurejea kwenye fainali za NBA na kuzuia utawala wa Oklahoma City Thunder katika ukanda wa Magharibi.
Wababe hao ambao walitwaa ubingwa wa NBA (Warriors 2022 na Nuggets 2023), walichuana majuzi katika mchezo wa kusisimua kiasi cha kuhitaji muda wa nyongeza, lakini mwisho wa siku hakukuwa na mshangao kuhusu nani aliyetofautisha matokeo Stephen Curry akiibuka shujaa akiipatia Warriors ushindi wa pointi 137-131, licha ya Aaron Gordon kuifungia Nuggets alama 50.
Kwa sasa, Golden State inaonekana kuanza msimu kwa kujiamini dhidi ya mmoja wa wapinzani wakubwa ukanda wa Magharibi. Huu ni mwanzo tu wa safari ndefu ya miezi saba ambayo huenda ikawa ya kufurahisha kwa mashabiki wa NBA. Haya hapa mambo manne muhimu ambayo yalishuhudiwa katika mchezo huo:
Kipindi cha mwisho cha robo ya nne na muda wa nyongeza kilikuwa cha maajabu ya Curry pekee alifunga pointi 16 mfululizo kwa Warriors, akiwazidi Nuggets wote kwa wakati huo. Ilikuwa ni taswira ya Curry wa zamani, yule ambaye alitisha kila alipokuwa na mpira mkononi.
Msimu uliopita hakuwaka sana kama ilivyokuwa kawaida yake. Kuna mechi alikuwa akifanya vizuri na nyingine akicheza chini ya kiwango, asilimia zake za mitupio zikiwa chini ya asilimia 40kutoka nje ya mstari wa “pointi tatu”, huku wastani wake wa kufunga pointi ukiwa 24.5 ni mdogo zaidi tangu 2015. Lakini mashabiki waliomuona aking’ara kwenye michezo ya Olimpiki ya Paris 2024, hasa fainali, wanajua wazi kuna bado anaweza kufanya kitu.
Dhidi ya Nuggets, Curry alifunga jumla ya pointi 42.
Aaron Gordon aliweka rekodi mpya binafsi kwa kufunga pointi 50 kwenye mchezo wa ufunguzi wa msimu wa Nuggets na kuwa mchezaji wa sita tu katika historia ya NBA kufanya hivyo.
Kabla ya kujiunga na Denver, Gordon alijulikana zaidi kwa staili yake ya kuruka (slam dunk contest) kuliko uwezo wa kufunga pointi. Lakini usiku wa Alhamisi, alishtua wengi kwa kufunga 10 kati ya mitupio 11 ya “3-point”, akionyesha mabadiliko makubwa katika uchezaji wake.
Hii kilikuwa kiwango bora zaidi katika maisha yake (nje ya dunk contest), na Warriors walishindwa kumdhibiti. Kwa kumbukumbu, Gordon alianza kuvaa jezi namba 50 baada ya kuhisi alinyimwa ushindi wa dunk contest, akimaanisha “nafikia kiwango cha juu (50)”. Usiku huo alithibitisha maana ya namba hiyo.
Curry alimpongeza: “Lolote alilofanya wakati wa kiangazi, limefanikiwa.”
WARRIORS WAPATA JIBU KWA JOKIC
Nikola Jokic amekuwa mchezaji bora zaidi wa miaka mitano iliyopita akiwa na mataji matatu ya MVP, lakini usiku huo hakuwa na madhara mwishoni mwa mchezo.
Alimaliza na alama mbili mbili katika takwimu tatu (pointi 21, rebounds 13, asisti 10), lakini alikosa mfululizo nafasi muhimu kiwemo mtupio wa ushindi mwisho wa robo ya nne na mingine minne kati ya mitano katika muda wa nyongeza.
Sifa zilienda kwa Draymond Green na Al Horford waliomkaba kwa nidhamu. Green alimzuia kwenye nafasi ya ushindi na Horford akamdhibiti vizuri katika dakika za nyongeza.
Jokic mwenyewe aliwahi kusema kuwa Green ndiye mchezaji anayemcheza kwa ufanisi zaidi. Sasa Warriors wana wachezaji wawili wenye uzoefu wa kumkaba Horford na Jimmy Butler III jambo linaloweza kuwa silaha muhimu ikiwa timu hizi zitaonana tena katika hatua za mtoano.
Msimu huu kulikuwa na matumaini makubwa Denver baada ya kufanya mabadiliko makubwa, ikiwemo kumpa David Adelman nafasi ya kocha mkuu wa kudumu na kuongeza wachezaji wapya kama Cam Johnson, Tim Hardaway Jr. na Bruce Brown.
Hata hivyo, mchezo wao wa kwanza haukuwa wa kuridhisha. Jokic bado alibeba jukumu kubwa, huku Gordon na Jamal Murray wakishika nafasi ya pili kati ya wachezaji ambao walionyesha kiwango kizuri.
Johnson alionekana mlegevu, akipiga mitupio minane tu na kufunga pointi tano katika dakika 32. Hardaway na Brown walitoka benchi na kuchangia pointi 14 pekee kwa pamoja.
