Mgombea urais TLP aahidi kumaliza migogoro ya wakulima, wafugaji

Moshi. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Tanzania Labour Party (TLP), Yustas Rwamugira ameahidi kushughulikia migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa kutenga maeneo maalumu kwa kila kundi.

Mbali na mkakati huo, pia amesema ataboresha miundombinu muhimu ya kilimo na ufugaji endapo atapewa dhamana ya kuongoza nchi.

Akizungumza leo katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Makuyuni, Rwamugira amesema migogoro ya wakulima imekuwa ikijirudia kwa muda mrefu kutokana na kutotengwa kwa maeneo ya wakulima na wafugaji, jambo linalosababisha mifugo kuharibu mazao mashambani.

Rwamugira amesema Serikali yake itahakikisha maeneo ya wakulima na wafugaji yanatengwa ipasavyo ili kila kundi liweze kuendesha shughuli zake bila migongano, hatua itakayosaidia kudumisha amani na kuimarisha uzalishaji.

“Tukiwaandaa wafugaji vizuri, tukiwawekea maeneo ya  majosho, machinjio na masoko, hatutakuwa na migogoro. Kila mmoja atafanya shughuli zake kwa amani,” amesema Rwamugira.

Aidha, Rwamugira ameahidi kuboresha sekta ya kilimo kwa kuweka miundombinu ya umwagiliaji katika maeneo yenye ukame, ili wananchi waweze kulima mwaka mzima na kuongeza tija katika uzalishaji.

“Tutahakikisha maeneo yote yenye ukame yanakuwa na mabwawa na mifumo ya umwagiliaji. Lengo letu ni kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia kilimo chenye tija,” amesema.

Vilevile, ameahidi kuwa ndani ya miaka mitano ya kwanza ya uongozi wake, atafanya mabadiliko makubwa katika sekta za afya na elimu, huku akipanga kuwapatia vijana ekari 30 kila mmoja pamoja na miundombinu ya msingi ya kilimo ili waweze kujiajiri na kuchangia maendeleo ya Taifa.

“Kila kijana atapewa ekari 30 na kuwekewa miundombinu. Nataka ndani ya miaka mitano tuwe na mabadiliko makubwa nchini,” aliongeza.

Rwamugira amewaomba wananchi kumpa kura pamoja na wagombea wote wa chama hicho katika nafasi za udiwani na ubunge, ili Serikali ya TLP iweze kutekeleza mipango ya maendeleo kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Richard Lyimo, mgombea ubunge wa TLP katika jimbo la  Vunjo, ameahidi kuboresha miundombinu ya barabara, kuimarisha huduma za usafi, na kuwawezesha vijana kupata ajira kupitia utoaji wa mashine za kushona na kuchomelea pamoja na walimu wa kuwafundisha stadi za ufundi.

“Vijana hawajiingizi kwenye mambo mabaya kwa kupenda, bali kwa sababu ya ugumu wa maisha. Nikipewa nafasi ya ubunge, nitahakikisha vijana wanapata fursa za kujiajiri,” amesema Lyimo.

Lyimo ambaye ni mwenyekiti wa TLP Taifa, ameongeza kuwa baadhi ya maeneo kama Himo yamekuwa yakidorora licha ya juhudi za wananchi, hivyo akawataka wakazi wa jimbo hilo kuwapima wagombea kwa kuzingatia uwezo wao wa kuwatumikia wananchi.

Naye mgombea udiwani wa TLP kata ya Makuyuni, Devid Matowo ameahidi kuhakikisha gari la kuzolea taka linapatikana, kuboresha barabara za ndani, na kusimamia upatikanaji wa chakula shuleni kwa kushirikiana na wazazi.

“Nipeni nafasi ya udiwani nihakikishe kata yetu inarudisha hadhi ya usafi, barabara zinapitika na wanafunzi wanapata chakula cha mchana shuleni,” amesema Matowo.