Mwalimu atua kwa Mpina, apokea malalamiko bei ya mazao

Meatu. Mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, ametua katika Jimbo la Kisesa, Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu, jimbo lililowahi kuongozwa na Luhanga Mpina.

Akiwa katika mkutano wake, wananchi wamemwomba kwamba iwapo atachaguliwa kuwa Rais, achukue hatua za haraka kushughulikia kuporomoka kwa bei ya mazao ya choroko, mbaazi na pamba, hali ambayo imekuwa ikiwakandamiza wakulima tangu mwaka 2020.

Ombi hilo limetolewa na mgombea ubunge wa Chaumma, Jimbo la Kisesa, Francis Kishabya, alipokuwa akielezea kero kubwa zinazowakabili wananchi wa Kisesa kwa mgombea urais huyo.

Kishabya amesema kuwa mwaka 2020, wananchi walipewa ahadi kwamba bei za mazao hayo zingepanda, lakini hadi leo zimeendelea kushuka bila ya hatua zozote za dhahiri kuchukuliwa.

“Pamba mwaka  2020 ilikuwa Sh2,000 lakini imeendelea kushuka hadi sasa imefika Sh1,100 wakati zao la mbaazi na choroko tulikuwa tukiuza kilo Sh3,000 lakini  sasa inauzwa Sh800.

“Bei hizi za mazao zimekuwa zikituumiza na kutukatisha tamaa wakulima, kwani tunatumia nguvu nyingi kulima halafu inapokuja kwenye kuuza  unajuta kwa nini ulilima na tukiuliza tunambiwa wanaopanga bei ni wengine,” amesema mgombea ubunge huyo.

Kutokana na changamoto hiyo, amemuomba Mwalimu siku zake 100 za kwanza akiwa madarakani kuhakikisha anaondoa changamoto hiyo ili wakulima waweze kuondoka katika kilimo cha umasikini.

Kwa upande wake, Mwalimu akijibu kero hizo, amesema kuwa hapa nchini kuna mazao yanayojulikana kama ya “kimkakati.”

Ameongeza kuwa mazao huuzwa nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na choroko na mbaazi, ambazo zina mahitaji makubwa katika nchi za India na China.

“Niwaulize mmewahi kusikia zao la mahindi au maharage ni zao la kimkakati na pia mjiulize zao linalohitajika duniani, unaambiwa bei ni ndogo wakati huo huo  mahindi na maharage bei ni ndogo.

“Sasa niwaibie siri wanunuzi wa pamba, mbaazi na choroko ni vigogo na wanaweka bei ndogo ili waje wanunue halafu wao wakauze bei kubwa huko nje, hamuamki, hamuoni hili wana Kisesa,” amehoji Mwalimu.

Kuhusu pamba, mgombea urais huyo amesema kuwa hakuna siku kanga inayotengenezwa kwa pamba iliyopungua bei; badala yake, bei ya pamba huongezeka kila mwaka. Vilevile, bei za mashati, suruali, pamoja na sare za shule za watoto pia huendelea kupanda.

“Kanga inatengenezwa na nini, yaani kanga bei kubwa lakini pamba bei ndogo, wee umeona wapi, walikuja hapa wakawaahidi kupandisha bei je wamepandisha.

“Chaumma tunaahidi tunakwenda kupandisha bei ya pamba kufika Sh5,000 kwa kilo na kuwafanya wasukuma kuwa matajiri kwani hili halihitaji mjadala kwa kuwa dunia haijawahi kusitisha kuzalisha nguo, kwa nini pamba isipande bei,” amesema Mwalimu anayejiita rais wa wasela.

Kuhusu mazao, mgombea urais huyo amesema kwa kuwa si muumini wa udalali wa mazao, katika Serikali yake ataondoa mfumo wa kuuza mazao kwa stakabali ghalani, na badala yake ataacha soko liwe huru.

Pia, kuhusu zao la pamba, amesema atahakikisha wakulima wanauza mara mbili: awamu ya kwanza kwa nyuzi na awamu ya pili kwa mbegu.

Amesema hali hii huko nyuma iliwafanya wakulima kuwa matajiri, lakini kwa sasa vyote vinauzwa pamoja na kupewa bei moja, jambo ambalo sio sahihi na linapunguza faida ya wakulima.

Kuiunganisha Meatu, mikoa mingine

Katika hatua nyingine, Mwalimu ameahidi kuwa ana mpango wa kuhakikisha Wilaya ya Meatu inaunganishwa vyema na wilaya zingine.

“Hivyo mkiniamini nawahakikishieni nitajenga barabara ya lami kutoka Mwandoya mpaka Bariadi, kutoka Mwandoya mpaka Mwanuzi, Thibit na kuendelea Singida na hivyo kuifungulia fursa za kiuchumi Meatu,” amesema Mwalimu.