Bariadi. Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, amewataka wananchi wa Bariadi kumchagua ili aweze kurejesha heshima ya zao la pamba na sekta ya mifugo, ambazo ziliwahi kuifanya wilaya hiyo kuwa kinara wa uchumi katika eneo hilo.
Mwalimu ameyasema hayo leo, Jumamosi Oktoba 24, 2025, akiwa katika siku ya pili ya kampeni zake mkoani Simiyu, ambapo leo amefanya mikutano katika Wilaya ya Bariadi Vijijini.
Katika maelezo yake, mgombea huyo amesema kuwa zao la pamba liliwahi kuleta heshima kwa wakazi wa mkoa huo, kiasi cha kuwasaidia kugharamia elimu ya watoto wao, na hata wazee waliokuwa na wake watano waliweza kuwahudumia wote pamoja na watoto wao bila matatizo.
Akizungumzia shughuli za ufugaji, mgombea huyo amesema wasukuma leo wanahangaika nchi nzima kutafuta malisho ya mifugo kwa kuwa tu eneo kubwa la ardhi limegeuzwa kuwa mapori tengefu.
Mwalimu amesema chini ya Serikali ya Chaumma hawatalikubali kwa kuwa wanataka kuwa na ng’ombe wenye afya watakaouzika kwenye masoko ya kimataifa kirahisi.
“Haiwezekani nchi hii ina ardhi kubwa na yenye malisho, lakini wafugaji wetu wanahangaika kila kona kuyasaka malisho, Chaumma tutahakikisha tunatenga ardhi ya kutosha kwa mifugo yenu,” amesema.
Pia, Mwalimu katika mikutano yake hiyo aligusia changamoto ya vijana kukamatwa kisa wamekutwa na swala na digidigi na kueleza kuwa wao wanaamini wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi wana haki ya kutumia kitoweo hicho.
“Wewe unakaa pembezoni mwa hifadhi kukutwa na swala, digidigi tatizo lipo wapi, wakati ni mboga za kawaida.
“Hawa watu wanatakiwa waachiwe wale swala na digidigi kama wale wanaoishi pembezoni mwa Ziwa Victoria ambao wanaruhusiwa kuvua samaki,” amessma.
Awali, mgombea ubunge wa Chaumma Jimbo la Bariadi Vijijini, Kwandu Seni, alisema walikuwa wakijivunia pamba, lakini leo imegeuka shubiri kwao na kutaka kumsikia Rais anawaahaidi nini katika kulishughulikia hilo.
