Same. Askofu wa Jimbo Katoliki Same, Rogatius Kimaryo amewaongoza waumini wa kanisa hilo katika ibada maalumu kuombea barabara kuu ya Dar es Salaam–Same–Mwanga–Arusha, kutokana na uwepo wa ajali zinazogharimu maisha ya watu.
Mbali ya ibada hiyo, kanisa limeweka wakfu eneo maalumu katika Kata ya Njoro, kutakakojengwa Groto ya Bikira Maria kwa ajili ya sala na tafakari kwa wasafiri wanaopita kwenye barabara hiyo.
Kwa mujibu wa kanisa, eneo hilo litakuwa mahali ambako kila msafiri ataweza kufika kusali kabla ya kuendelea na safari, kama njia ya kuomba ulinzi na baraka za Mungu barabarani.
Akihubiri katika ibada ya kuweka wakfu eneo hilo, Askofu Kimaryo amesema barabara ya Same imekuwa na ajali nyingi zisizoisha, ambazo zimesababisha watu wengi kupoteza maisha na uharibifu wa mali.
Baadhi ya waumini wakiwa katika ibada maalum ya kuombea kukoma kwa matukio ya ajali Wilaya ya Same.
“Barabara hii kuu ya Dar es Salaam -Same-Arusha tumeshuhudia katika historia ikisababisha ajali nyingi na watu kupoteza maisha na mali, wapo viongozi wa dini na siasa ambao wamepoteza maisha katika barabara hii,” amesema na kuongeza:
“Wapo viongozi wetu watano, wakiwamo mapadri, watawa wetu walifia katika barabara hii, lakini hata Askofu wa Dayosisi ya Mwanga, Askofu Sendoro Nate alikufanya kwa ajali mwaka jana katika barabara hii.”
Askofu Kimaryo amesema katika barabara hiyo Juni 28, 2025 eneo la Sabasaba, Same mjini kulitokea ajali iliyosababisha vifo vya watu 42 baada ya magari mawili ya abiria kugongana na kuwaka moto.
“Ajali hizi zinasababisha maumivu makali kwa ndugu, jamaa na marafiki, hivyo sisi tumeona ni vyema tukamkabidhi Bikira Maria barabara hii kwa kujenga Groto ya Bikira Maria awaombee wasafiri wote,” amesema.
Akizungumzia historia ya barabara hiyo, Paroko wa Parokia ya Vudee Juu, Padri Valentine Luvara, amesema kutokana na ajali nyingi kutokea katika barabara hiyo, walifanya utafiti na kubaini wazee wa wilaya hiyo walikuwa wakifanya matambiko katika barabara hiyo, hali ambayo imekuwa ikichochoa matukio ya ajali.
“Baada ya kuzunguka na kutafuta historia ya ajali hizi tumefahamu mambo ya historia, tumefahamu mambo ya ajabu sana ambayo yamesimikwa katika barabara kuu ya Same -Dar-Arusha,” amesema.
“Enzi hizo barabara hii ya tambarare kuanzia Biko hadi Kifaru eneo hili lilikuwa la wafugaji zaidi, walijitahidi kutunza kundi lao na walilisimika katika nguvu za giza katika eneo hili ambalo barabara kuu imepitia ambayo ilikuwa ni njia ya kupitisha wanyama,” amesema.
Padre Luvara ameeleza: “Wafugaji hawa wa enzi hizo waligundua mifugo yao haiwezi kuwa salama isipokuwa na ulinzi madhubuti, kwa namna hiyo walisimika mizimu ambayo waliweka kama mlinzi anayelinda barabara hii ya kupitisha wanyama wao.”
“Na kwa sababu hiyo, huyu mlinzi alikuwa na mamlaka ya kulinda mifugo iwe salama na kila anayepitisha mifugo yake alipaswa kutoa zawadi au kafara kwa mzimu ambaye anatunza njia, kila ambaye mifugo yake ilirudi salama alileta kondoo, mbuzi na mzimu ndiye aliyekuwa akipokea hizo kafara,” amesema.
Amesema mzimu huyo alipewa mamlaka ya kuokota katika mifugo yao na kwamba, walikuwa hawamuamini Mungu katika kipindi hicho.
“Katika kipindi ambacho barabara hii ya Same inachimbwa kutoka Dar es Salaam-Arusha wakaona kwa urahisi zaidi ipite barabara ambayo wanyama walikuwa wakipita ambayo sasa hivi imekuwa ni chinja chinja kweli na watu wamekufa sana,” amesema na kuongeza:
“Hivyo, hapa tutamsimika mama Bikira Maria kama msimamizi wa wanasafiri katika barabara hii ili mama Bikira Maria awe kiongozi wa wasafiri wote katika barabara hii.”
Mdau wa maendeleo katika kanisa hilo, Humphrey Lyimo, amesema wataendelea kushirikiana na kanisa kuhakikisha ajali wilayani Same zinapungua na kuchangia fedha kwa ajili ya kuanzisha eneo maalumu la sala.
Lyimo ametoa Sh3.5 milioni kwa kushirikiana na marafiki zake ili kuhakikisha malengo ya kanisa hilo yanafanikiwa.
Juni 28, mwaka huu katika eneo la Sabasaba, Same mjini kulitokea ajali iliyosababisha vifo vya watu 42 baada ya magari mawili ya abiria kugongana na kuwaka moto.
Ajali nyingine ni ya Machi 30, 2025 iliyoua wanakwaya sita wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mmeni Chome, Dayosisi ya Pare, wilayani Same na kusababisha majeruhi 23.
Novemba 28, 2023 katika barabara hiyo, watu watatu wa familia moja walifariki dunia wilayani Mwanga, akiwamo bibi harusi mtarajiwa na mama yake mzazi, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana na lori katika eneo Mwanga.
