Dar es Salaam. Tukio la mwanamke kunaswa kwenye video akimpiga mwenzake eneo la Kariakoo limeibua mjadala kuhusu mwenendo wa baadhi yao kujihusisha na matukio ya ukatili na udokozi.
Tayari Jeshi la Polisi limesema limemtambua mtuhumiwa na linaendelea na hatua za kisheria.
Katika taarifa ya Oktoba 22, 2025 ya Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, limesema baada ya video hiyo kusambaa mitandaoni, vyombo vya ulinzi na usalama vilianza ufuatiliaji wa haraka kubaini wahusika wa tukio hilo lililoonekana kuvunja sheria na haki za binadamu.
“Tangu picha mjongeo hiyo ilipoanza kusambaa, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu limefanya ufuatiliaji na aliyefanya kitendo hicho amefahamika majina yake, eneo analofanyia kazi pamoja na namba zake za simu,” alisema Misime.
Alieleza hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa kulingana na ushahidi unaoendelea kukusanywa, ikiwemo maelezo ya mashuhuda wa tukio hilo.
Polisi pia imewaomba wananchi wenye taarifa kuhusu mwanamke aliyepigwa kwenye video hiyo, kujitokeza kusaidia katika mchakato wa uchunguzi.
“Kwa anayemfahamu mwanamke huyo, amjulishe afike katika Dawati la Jinsia la Polisi Msimbazi ili hatua ziendelee kuchukuliwa dhidi ya kitendo alichofanyiwa,” alisema Misime akionya wananchi kuepuka kujichukulia sheria mikononi.
Tukio hilo ni miongoni mwa mengine ya namna hiyo yanayohusisha vitendo vya wizi na vurugu miongoni mwa wanawake katika maeneo mbalimbali, hususani Kariakoo, Sinza, Tandika na Karume jijini Dar es Salaam.
Udokozi unaovaa uso wa ujasiri
Katika kipindi cha hivi karibuni, kumekuwa na matukio ya wanawake kuhusishwa na vitendo vya wizi sokoni, madukani na hata kwenye magari ya abiria.
Ndani ya jamii iliaminika kuwa wanawake hutumika kama chambo kwenye matukuio ya uhalifu unaotekelezwa na wanaume, lakini sasa, baadhi yao wamekuwa wakijihusisha moja kwa moja katika uhalifu huo.
“Zamani tulikuwa tukiamini mama ni nguzo ya heshima nyumbani, lakini leo unasikia mama amekamatwa kwa kuiba dukani. Ni aibu kubwa kwa familia,” anasema Mzee Athumani, mkazi wa Temeke.
Mbali ya wizi katika maeneo hayo, yapo matukio ya wanawake kujihusisha na uhalifu huo yanapotokea matukio ya ghafla kama vile majanga ya moto.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alipozungumza na wananchi wa Kawe baada ya tukio la moto lililoteketeza soko la eneo hilo Septemba 15, 2025 alisema:
“Nimepenyezewa taarifa kwamba jana wakati moto unawaka, wanawake waliongoza kwa kuiba mali za waathirika, badala ya kusaidia kuokoa. Hili ni jambo la kusikitisha sana.”
Wapo walioshangazwa na kauli hiyo inayoonyesha jinsi maadili yalivyoporomoka, kwani ndani ya jamii inaaminika wanawake ni nadra kushiriki matukio ya kihalifu.
Ripoti ya takwimu ya wafungwa na mahabusu Tanzania Bara 2024 iliyotolewa Aprili, 2025 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inaonyesha wafungwa wanawake waliohukumiwa kwa wizi ni 93 watu wazima na vijana sita, huku mahabusu wakiwa 32 watu wazima na sita vijana.
Ripoti hiyo inaeleza mwaka 2023 wanawake waliofungwa kwa wizi ni 93 watu wazima na vijana wanane, huku mahabusu walikuwa 26 watu wazima na vijana wawili.
Takwimu hizi zinaweza kuonekana ndogo, lakini zinatoa ujumbe kuhusu hali ilivyo miongoni mwa wanawake ambao ni kioo katika malezi ya familia.
Akizungumza na Mwananchi, Rehema Mussa, mfanyabiashara wa viatu Kariakoo, anasema wapo baadhi ya wanawake wanaofika eneo hilo la biashara kwa ajili ya kuiba.
“Wapo wanawake wanaokuja dukani wakiwa na tabasamu, wanaomba bei ya bidhaa nyingi, kisha ghafla mmoja anaghairi kununua akisema haitaji tena. Unapojaribu kuhesabu bidhaa, unakuta viatu vimepungua. Ukimkagua, unakuta amevificha kwenye kwapa au ndani ya kanga,” anasema Rehema.
Anasema matukio ya aina hiyo kwa Kariakoo hususani kwa bidhaa zinazofichika kirahisi kama nguo na viatu ni ya kawaida.
Vilevile, anasema wapo wanaokwenda na watoto na ndugu ambao huwatumia kuficha mali zinazoibwa.
“Mara nyingi wanawake hawa huja wakiwa na watoto wachanga au mifuko mikubwa. Wanajifanya wateja wa kawaida, lakini wanapokuwa ndani ya duka wanapanga mikakati ya kuchukua bidhaa ndogo ndogo,” amesema.
Rehema anasema kutokana na hasara wanazopata, wamefikia uamuzi wa kufunga kamera za ulinzi ili kudhibiti udokozi huo.
Husna Shaka, mfanyabiashara mwingine wa viatu katika eneo hilo anasema wizi unaotokea katika biashara unawatia hasara.
Vivyo hivyo kwa Samson Njau, mfanyabiashara wa nguo Sinza, anasema baadhi ya wanawake huchukua nguo nyingi kwa ajili ya kujaribu kabla ya kununua, kisha hununua moja au kuacha wakati huo wakiwa wameficha nyingine.
“Hii imekuwa ni mazoea, wanavyoomba huwezi kujua kwa sababu anachukua nguo nyingi, akifika anavaa ndani au anakuomba ukamwangalie, huku nyuma mwenzake anachukia kilichopo bila mhudumu kujua,” anasema Njau.
Mfanyabiashara wa mitumba Tandika, Rashid Nyanda maarufu Chidtz amesema wamekuwa wakiibiwa nguo na wanawake ilhali gharama zake ni nafuu kuanzia Sh3, 000.
“Kinachotushangaza huku sokoni wanaotuibia ni warembo, wamependeza. Tunachofanya hapa tumejipanga, kama nipo muuzaji pekee, kuna watu kazi yao ni kuangalia wale wanaoficha nguo zetu na adhabu yao kubwa ni makofi na kurudisha alichochukua huku tukimzomea,” amesema.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa wafanyabiashara Taifa, Hamis Livembe amesema hajawahi kupokea taarifa ya malalamiko ya wafanyabiashara kuibiwa kwenye maduka zaidi ya kuona kwenye mitandao ya kijamii.
“Binafsi sijawahi kupata taarifa kutoka kwa viongozi wa maeneo tofauti kuhusu kuibiwa kuanzia mkoa hadi wilaya, zaidi naishia kuona kwenye mitandao kama watu wengine na wakati mwingine nafikiria kuwa ni watengeneza maudhui mitandaoni,” amesema.
Amesema kama kuna matukio ya aina hiyo ni muhimu wafanyabiashara kuwa na watu zaidi ya mmoja ili kuweka umakini na wezi.
Mwanasaikolojia, Ramadhani Massenga anasema kuongezeka kwa idadi ya matukio yanayohusisha wanawake, ni zidi ya uhalifu, inaashiria kwamba jamii imeshindwa kutekeleza majukumu yake ya msingi.
Amesema kwa muda mrefu matatizo ya kifungo na maumivu ya maisha yalihusishwa zaidi na wanaume kutokana na jukumu lao la kutafuta riziki, lakini sasa wanawake wameanza kuingia kwenye kundi hilo kwa kasi.
“Tumeanza kuona wanawake wakijihusisha na wizi, tafsiri yake ni kwamba mambo yaliyokuwa yakifanywa na wanaume pekee, sasa yameanza kufanywa na wanawake, hii ni ishara ya jamii kufeli,” amesema.
Massenga anasema tatizo hilo limetokana na mabadiliko ya kijamii ambapo wanawake wanataka kutazamwa kwa mizani sawa na wanaume, jambo linalowasukuma kujitumbukiza kwenye majukumu ya wanaume ikiwemo uhalifu.
“Thamani ya mwanaume inatazamwa kwa uwezo wake wa kutafuta, lakini si hivyo kwa mwanamke. Kwa sababu tumeweka viwango sawa, wanawake wanajikuta wakifanya mambo yasiyo ndani ya asili yao ili kuonekana wanaweza kama wanaume,” amesema.
Massenga amesema mabadiliko hayo yamechangiwa pia na wanaume wengi kushindwa kubeba majukumu yao, hali iliyowalazimu wanawake kujitwisha majukumu ya kiume.
“Wanaume wengi wameacha majukumu yao, wanawake wameyachukua, wakaingia kwenye mfumo wa kiume. Hapo ndipo tunapoanza kuona tabia ambazo zamani zilihusishwa na wanaume, sasa zikifanywa na wanawake,” amesema.
Amesema tatizo hilo linatokana pia na mabadiliko ya mienendo ya wanawake katika mahusiano, baadhi wamepoteza heshima na utii kwa wanaume, jambo linalowafanya wanaume kukataa kuwajibika.
“Mwanamume hujisikia fahari kubeba majukumu mbele ya mwanamke anayemheshimu. Lakini kama mwanamke hamtii wala hamuelewi, mwanamume hawezi kuwajibika kwake. Hapo mwanamke anabaki kujitafutia mwenyewe, hata kama ni kwa wizi,” amesema.
Amesema kitendo cha mwanamke kuiba si kosa pekee, bali ni kielelezo cha mfumo wa kijamii ulioporomoka.
“Mwanamke akifika hatua ya wizi na usokozi, maana yake kila ngazi ya msaada kama baba, kaka, mume au jamii imeshindwa. Hiyo ni ishara ya jamii kufeli,” amesema.
