Othman afunga kampeni Pemba, aahidi kuimarisha ‘brandi ya Zanzibar’

Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman amefunga kampeni zake kwa upande wa Pemba huku akiwaahidi Wazanzibari kwenda kuimarisha ‘brandi ya Zanzibar’.

Amesema Zanzibar ina mambo yake, alama zake, heshima yake, dalili zake, watu wake na utukufu wake, silka, na utamaduni na mila, akisema masuala hayo ndio yanayoifanya wananchi wa Zanzibar wakaitwa Wazanzibari, lakini kwa miaka mitano iliyopita hali ilikwenda kinyume.

Othman amefunga kampeni hizo, leo Jumamosi Oktoba 25,2025 akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni zake katika uwanja wa Tibirinzi, wilayani Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.

Baada ya kumaliza upande wa Pemba, Othman anatarajiwa kufunga kampeni zake pia kesho Mjini Unguja katika uwanja wa Kibandamaiti.

“Ahadi yangu hili nitakwenda kulisimamia, ili tuisimamishe ‘Zanzibar brandi’, miaka mitano Zanzibar brandi imevurugwa na hatukubali kurudi tena huko. Tukirudi huko tutaimaliza Zanzibar brandi.

“Lazima tukalisimamie hili, kwa wivu mkubwa twendeni tukaijenga Zanzibar brandi, Zanzibar na alama na heshima zake,” ameeleza Othman.

Mbali na hilo, Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, amewataka Wazanzibari ujiepusha na ‘matango pori’ ya kujazwa hofu katika kipindi hiki kuhusu uchaguzi wa Oktoba 29.

“Kipindi hiki mtapewa na kuuziwa matango pori kwelikweli ya kuwajaza hofu, wasiwasi na kuwakatisha tamaa. Hiki ndicho kilichobakia, mara tutakuja…tulieni roho zenu msijali,” amesema.

Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa amesema ndani ya miaka mitano wametoa ushirikiano wa kuimarisha misingi ya maridhiano, lakini walioko madarakani wamewakwamisha.

“Tunahitaji kiongozi mpya atakayetembea katika misingi ya maridhiano, kama ilivyoasasiwa na Maalim Seif Sharif Hamad na Aman Abeid Karume. Kiongozi huyo si mwingine ni Othman Masoud ndiye atakayetufikisha huko,” amesema.

Jussa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi ya ACT-Wazalendo, amesema licha ya wananchi wa Pemba kupata changamoto mbalimbali ikiwemo kuteseka na hali ngumu ya maisha, lakini hawajarudi nyuma katika mapambano ya demokrasia.

“Ndugu zangu nawaheshimu sana, harakati za Zanzibar bila ya Pemba zingeshayumba zamani sana. Pemba ilihitimu zamani enzi za Maalim Seif, kisha zikahamia Unguja ambayo inafuata mkondo, sasa hivi ni kama vile mapacha,” amesema Jussa.

Jussa amewatoa hofu wafanyakazi wa umma wa Zanzibar, kuhusu kupiga kura, akiwataka kujitokeza kwa wingi kushiriki mchakato huo bila hofu yoyote na kumchagua kiongozi wanayemhitaji.

Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Omar Ali Shehe amesema, “zimebaki siku kadhaa kabla ya Wazanzibari hawajafanya uamuzi. Leo tupo Tibirinzi, uwanja wenye historia ya mapambano, miaka 38 Maalim Seif Sharif Hamad alitoa ahadi hadi leo tunaikumbuka.

“Tunatumaini Othman naye yeye atatoa ahadi ya matumaini, mwiba ulipoingia, ndipo utakapotokea. Tutahakikisha majimbo yote yanakwenda ACT Wazalendo,” amesema Shehe.

Katibu wa Habari, Uenezi, Mawasiliano kwa Umma wa ACT Wazalendo, Salim Biman amewashukuru viongozi wote wa matawi, majimbo, wilaya hadi mikoa wa kisiwa hicho kwa kufanikisha vyema mchakato wa kampeni za Othman.

“Pia tunashukuru kamati ya majukwaa kwa kazi nzuri, usiku na mchana mmefanya kazi hii bila ya kuchoka.Tunawashukuru Idara ya itifaki wamefanya kazi kubwa sana, wasanii pia bila kusahau,” amesema Biman.