Sababu Mzize kuikosa Silver Strikers, mabosi Yanga wakuna vichwa

HII inaweza kuwa taarifa mbaya kwa mashabiki wa Yanga, baada ya mshambuliaji wa kikosi hicho, Clement Mzize, kujitonesha jeraha la goti, hali iliyomfanya kuikosa mechi ya leo Oktoba 25, 2025 dhidi ya Silver Strikers.

Mzize baada ya kujitonesha jeraha lililokuwa likimsumbua awali ambalo alikuwa amepona na kuelezwa angetarajiwa kucheza leo, sasa huenda akafanyiwa upasuaji mkubwa ili kumtibu.

Mshambuliaji huyo ambaye amekuwa na kiwango bora ndani ya Yanga akiwa ameichezea kwa misimu mitatu sasa, msimu huu umeanza kwa bahati mbaya kwake kutokana na kusumbuliwa na majeraha yanayomfanya kukosa mechi kadhaa.

Taarifa kutoka kambi ya Yanga, zililiambia Mwanaspoti kuwa, Mzize amewatia hofu tena kwani jana jioni Oktoba 24, 2025 katika mazoezi ya mwisho kuelekea kuikabili Silver Strikers, alijitonesha jeraha lake la goti.

“Kuna uwezekano akafanyiwa upasuaji wa goti nje ya nchi, hivyo kumpata kwenye mechi za karibuni ni bahati sana,” kilisema chanzo.

Mechi ya mwisho Mzize kuonekana uwanjani ni ile ya Septemba 19, 2025 dhidi Wiliete ambayo Yanga ilianzia ugenini katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kushinda kwa mabao 3-0.

Baada ya hapo, Mzize alikosekana katika mechi nne za mashindano dhidi ya Pamba Jiji (Septemba 24, 2025), Wiliete (Septemba 27, 2025), Mbeya City (Septemba 30, 2025), Silver Strikers (Oktoba 18, 2025) na ya leo dhidi ya Silver Strikers.

Nyota huyo aliyeibuka kinara wa mabao ndani ya kikosi cha Yanga katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita akifunga 14, mawili nyuma ya kinara wa jumla, Jean Charles Ahoua (16), amekuwa mchezaji muhimu kikosini hapo eneo la ushambuliaji.

Bado haijaelezwa sasa Mzize atakuwa nje ya uwanja kwa muda gani baada ya jana kujitonesha.

Kikosi cha Yanga kinachoanza leo dhidi ya Silver Strikers ni Djigui Diarra, Israel Mwenda, Mohamed Hussein, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Prince Dube, Mohamed Doumbia na Pacome Zouzoua.

Waliokuwa benchi ni Aboutwalib Mshery, Bakari Mwamnyeto, Chadrack Boka, Kibwana Shomari, Aziz Andabwile, Lassine Kouma, Offen Chikola, Edmund John na Andy Boyeli.