Dar es Salaam. Siku tano baada ya Shirika la Amnesty International kutoa taarifa iliyozishutumu mamlaka za Tanzania kwa ukiukwaji wa haki za binadamu na ukandamizaji wa watu kuelekea uchaguzi mkuu, Serikali imejibu taarifa hiyo ikisema imesikitishwa na madai hayo yasiyo na uthibitisho.
Oktoba 20, 2025 Shirika la Amnesty ilitoa taarifa yake lilioiita “Unopposed, Unchecked, Unjust: ‘Wave of Terror’ Sweeps Tanzania Ahead of 2025 Vote” ikiipa kichwa cha habari kisemacho ‘TanzaniaMamlaka zaweka hali ya hofu na kuongeza ukandamizaji kuelekea Uchaguzi Mkuu’.
Katika taarifa hiyo Amnesty lilieleza kuwa Mamlaka za Tanzania zimeongeza ukandamizaji dhidi ya wapinzani wa kisiasa, waandishi wa habari, asasi za kiraia na watetezi wa haki za binadamu kwa mkakati mahususi wa kueneza hofu, kuzima ushiriki wa kiraia na kuimarisha utawala.
Amnesty inaeleza kuwa kabla ya kuandaa taarifa hiyo iliwahoji watu 43 wakiwemo waathirika, mashahidi, ndugu wa waathirika, wawakilishi wa kisheria na wanachama wa asasi za kiraia na pia kukusanya taarifa za mashambulizi kutoka vyombo vya habari. Kila kisa kilichorekodiwa kilithibitishwa kupitia vyanzo huru zaidi ya kimoja pale ilipowezekana.
Akiwasilisha taarifa hiyo Mkurugenzi wa Kanda wa Amnesty International kwa Afrika Mashariki na Kusini, Tigere Chagutah, alisema wapinzani wa kisiasa wamekabiliwa na mashitaka yenye ushawishi wa kisiasa na katika baadhi ya matukio haki yao ya kushiriki uchaguzi imekataliwa.
“Uchaguzi mkuu unatarajiwa kutawaliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), huku wagombea wakuu wawili wa urais kutoka upinzani wakizuiwa kushiriki. Mwezi uliopita, Luhaga Mpina aliondolewa tena kugombea, huku Tundu Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chama kikuu cha upinzani, akiwa rumande akikabiliwa na shtaka la uhaini,” amesema Chagutah.
Amnesty International linataka mamlaka kukomesha vitendo ukandamizaji wa maoni tofauti, ambayo imeongezeka tangu uchaguzi uliopita miaka mitano iliyopita. Wamezitaka mamlaka kuachilia mara moja na bila masharti wale wote waliokamatwa kwa madai ya kisiasa au kidini, wakiwemo viongozi wa upinzani kama Tundu Lissu.
Mbali na hayo Amnesty International ilibanisha kuwa kulikuwa na ukiukaji mkubwa haki za binadamu, ikiwemo kupotezwa kwa watu kwa kulazimishwa, mateso na mauaji yasiyo ya kisheria ya viongozi wa upinzani na wanaharakati.
Walieleza kuwa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kilibaini visa 83 vya watu waliopotea katika mazingira ya kutatanisha hadi kufikia Agosti 9, 2024.
Amnesty International inazitaka mamlaka kufanya uchunguzi wa haraka na makini kuhusu matukio yote ya utekaji, mauaji yasiyo ya kisheria, kupotezwa kwa watu na mashambulizi, na kuwawajibisha wahusika.
Kadhalika Amnesty lilieleza kuwa Mamlaka za Tanzania zimekuwa zikikataza, kuvuruga au kusambaratisha mikusanyiko ya amani, hasa ile inayoratibiwa na vyama vya upinzani. Viongozi wa upinzani na wanaharakati wamewekewa vikwazo vikali vya usafiri ambavyo vimezuia uwezo wao wa kufanya shughuli za kisiasa kwa kawaida.
Katika taarifa yake Amnesty lilidai kuwa Mamlaka za Tanzania hazikujibu ombi la Amnesty la kutoa maoni hata hivyo katika majibu ya Tanzania yaliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msingwa alisema kuwa Serikali haikupewa fursa na haki ya kujibu kabla ya kuchapishwa kwake.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea kwa masikitiko taarifa fupi iliyotolewa na Amnesty International yenye kichwa cha habari “Unopposed, Unchecked, Unjust: ‘Wave of Terror’ Sweeps Tanzania Ahead of 2025 Vote”, na imeonyesha wasiwasi mkubwa juu ya maudhui na mtazamo wa madai yaliyomo ndani yake.” Alieleza taarifa ya Msingwa.
Msingwa alielezea dhamira ya serikali ya thabiti ya kulinda na kuendeleza haki za binadamu kama ilivyohakikishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (kama ilivyorekebishwa) na kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa na ya kikanda ambayo Tanzania imeridhia, ikiwemo ICCPR, Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, na Mkataba Dhidi ya Mateso.
Alilaani taarifa ya Amnesty akisema mtindo wake unadhoofisha misingi ya uhalisia na kuheshimiana ambayo inapaswa kuongoza mazungumzo kuhusu haki za binadamu kimataifa akisema maelezo yaliyomo kwenye taarifa hiyo yanayoonyesha kwamba Tanzania ni nchi inayoruhusu kukamatwa kiholela, kupotezwa kwa watu kwa kulazimishwa, na kukandamiza uhuru wa raia, hayana uhusiano wowote na uhalisia wa kisheria na wa taasisi zilizopo nchini.
“Tanzania inatekeleza sera ya kutovumilia kabisa mateso au aina yoyote ya adhabu ya kikatili na isiyo ya kibinadamu. Madai ya ukiukaji wa aina hiyo huchunguzwa na mamlaka husika kama vile Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP), na Mahakama, kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Kanuni ya Adhabu, na Sheria ya Jeshi la Polisi na huduma saidizi,” alisema.
Serikali pia inasisitiza kwamba uhuru wa kujieleza, kukusanyika kwa amani na upatikanaji wa taarifa vinalindwa na Katiba, na vinasimamiwa kupitia sheria kama vile Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa, na Kanuni za Maudhui Mtandaoni. Sheria hizi zinatekelezwa kwa mujibu wa Ibara ya 19(3) ya ICCPR, ambayo inaruhusu kuwekwa kwa vizuizi vidogo vinavyohitajika kulinda usalama wa taifa, utulivu wa umma, na haki za watu wengine.
Kuhusu mchakato wa uchaguzi, Serikali imesema Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inafanya kazi kwa uhuru kama ilivyohakikishwa na Ibara ya 74 (1) ya Katiba. Tanzania inaendelea kuwezesha uangalizi wa uchaguzi na kudumisha misingi ya uwazi, kutokuwa na upendeleo, na ushiriki sawa wa kisiasa.
“Serikali ya Tanzania inasisitiza kwamba haitetei vitendo vya kupotezwa kwa watu wala mauaji yasiyo ya kisheria. Kila tukio linaloripotiwa hufanyiwa uchunguzi wa kina na kuchukuliwa hatua za kisheria. Mahakama inaendelea kuwa huru, na kila mtu ana haki ya kupata usikilizwaji wa haki kwa mujibu wa sheria za ndani na za kimataifa,”
Alisisitiza dhamira ya kwa utawala wa kidemokrasia, utawala wa sheria, na ulinzi wa haki za binadamu kabla, wakati, na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Huku akisema itaendelea kuwa wazi kwa mazungumzo na wadau wote wenye nia njema, na inahimiza taasisi zote kuwasiliana moja kwa moja na mamlaka husika kabla ya kuchapisha taarifa zinazoweza kupotosha umma.
