Singida BS yatinga makundi Shirikisho, ikiandika rekodi mpya

KLABU ya Singida Black Stars imetinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kuifunga Flambeau du Centre ya Burundi mabao 3-1, katika mechi ya mkondo wa pili iliyopigwa leo Jumamosi Oktoba 25, 2025 kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salam.

Flambeau ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia David Irishura dakika ya 26, huku Singida Black Stars ikijibu mapigo na kusawazisha

dakika ya 55 kupitia mshambuliaji nyota wa kikosi hicho raia wa DR Congo, Malanga Horso Mwaku.

Wakati timu hizo zikishambuliana kwa zamu kila moja ikisaka bao la pili, Flambeau ilijikuta ikicheza pungufu baada ya nahodha wa kikosi hicho, Amissi Asmani kuunawa mpira eneo la hatari na kusababisha penalti iliyopigwa na Clatous Chama na kuzama wavuni dakika ya 67.

Baada ya Flambeau kuwa pungufu ya mchezaji mmoja, Singida Black Stars iliendelea kulisakama lango la wapinzani wao na dakika ya 75, ilipata bao la tatu kupitia kwa Idriss Diomande na kuifanya kufuzu kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya pambano la kwanza kutoka sare ya bao 1-1.

Singida ilianza hatua ya kwanza ya michuano hii kwa kuitoa Rayon Sports kutoka Rwanda kwa jumla ya mabao 3-1, huku kwa upande wa Flambeau iliyoaga rasmi katika Kombe la Shirikisho Afrika ikiitoa Al Akhdar ya Libya kwa jumla ya mabao 4-3.

Kufuzu kwa Singida Black Stars katika hatua ya makundi, inaifanya timu hiyo kuandika rekodi mpya na kuwa ya pili msimu huu katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa Tanzania, baada ya Azam FC kuiondosha KMKM ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 9-0.

Mbali na Singida Black Stars na Azam FC zilizofuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, timu nyingine ya Tanzania iliyofuzu makundi ni Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya leo jioni kuiondosha Silver Strikers ya Malawi kwa jumla ya mabao 2-1.