TPDC yatumia Sh3.4 bilioni kuboresha miradi ya kijamii Mtwara, Lindi

Dar es Salaam. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema limetumia jumla ya Sh3.4 bilioni katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa jamii zinazozunguka maeneo yenye shughuli za mafuta na gesi asilia Mtwara na Lindi.

Utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya dhamira ya shirika hilo, kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na rasilimaliza mafuta na gesi.

Kulingana na taarifa aliyoitoa Meneja Mawasiliano wa TPDC, Marie Msellemu, Oktoba 25,2025 amesema miradi hiyo imetekelezwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na 2024/25.

Meneja huyo amasema miradi hiyo imejikita katika sekta za afya, elimu, maji, usalama na miundombinu katika mikoa ya Mtwara na Lindi.

“Tunataka wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya miradi ya mafuta na gesi wawe miongoni mwa wanufaika wakuu wa shughuli hizi. Ndiyo maana TPDC imewekeza kwenye miradi inayogusa maisha yao moja kwa moja,” amesema Msellemu.

Msellemu amesema kwa Mkoa wa Mtwara, TPDC imejenga kituo cha afya Msimbati kwa Sh759.9 milioni, kituo cha polisi Msimbati kwa Sh186.2 milioni, pamoja na uwekaji wa taa za barabarani katika vijiji vya Mngoji na Msimbati kwa Sh498.21 milioni.

Aidha, amesema miradi mingine ni pamoja na mradi wa maji kijiji cha Mngoji unaoendelea kwa Sh47.7 milioni, mradi wa maji kutoka kijiji cha Mayaya hadi Mahiva unaoendelea kwa Sh38.8 milioni, na ujenzi wa kituo cha afya Mtendachi unaoendelea kwa Sh38.84 milioni.

Ameongeza kuwa, TPDC pia inatekeleza ujenzi wa kituo cha afya Nanyamba kwa Sh400 milioni.

Kwa upande wa Mkoa wa Lindi, Msellemu amesema TPDC imetekeleza miradi kadhaa ikiwemo ujenzi wa Shule ya Msingi Likongo kwa Sh1.3 bilioni, ujenzi wa madarasa matatu katika Shule za Msingi Marendego na Kilwa Masoko kwa Sh72 milioni, na ujenzi wa madarasa katika eneo la Mbwemkuru kwa Sh20 milioni.

Miradi mingine ni mradi wa maji Kilangala B wenye thamani ya Sh50 milioni umekamilika na unafanya kazi.

Msellemu ameongeza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unaonyesha dhamira ya TPDC kuimarisha mahusiano na jamii sambamba na kuchochea maendeleo endelevu, katika maeneo yanayohusiana na sekta ya mafuta na gesi nchini.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Kata ya Somanga wilayani Kilwa, Salum Kumbora amesema jamii inanufaika kutokana na miradi mbalimbali inayotekelezwa na TPDC.

Tunawapongeza TPDC kwa namna ambavyo wanaishika jamii mkono, wametujengea shule kuwasaidia wanafunzi kutokaa nje, wanafunzi na walimu sasa wanasoma na kukaa katika mazingira mazuri, pia tumepata madawati.

“Hii imetusaidia wanafunzi kupata hamasa ya kuhudhuria shule bila kukosa kutokana na mazingira kuwa mazuri,” amesema.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Marendego Shaban Nasoro amesema walikuwa na uhaba mkubwa wa madarasa na sasa kukamilika kwa ujenzi wa madarasa matatu kumeondoa adha waliyokuwa wanapata kwa wanafunzi kukaa wengi kwenye darasa moja.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji Marendego Said Yusuph amesema kimbunga Hidaya kilisababisha madarasa mengi katika kijiji hicho kuezuliwa na hivyo msaada huo umekuwa na tija kwa wakazi hao.

“Tunaahidi kutokana na mradi huu kukamilika kwa wakati na wanafunzi wetu wanasoma kwa uhakika tutatunza mradi huu uwe endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo, tutaweka mlinzi ili miradi hii isiharibiwe na watu wasiopenda maendeleo,” amesema.