Unayopaswa kufahamu kuhusu asili ya makalio makubwa

Dar es Salaam. Kwa baadhi ya wanawake, urembo ni pamoja na kuwa na makalio makubwa, hali ambayo imekuwa kama kipimo kipya cha mvuto wa mwili.

Wapo wanaoamini kuwa umbo hilo linavutia zaidi na kuongeza kujiamini, hasa katika zama hizi ambazo mitandao ya kijamii imetawala taswira ya urembo.

Ni kutokana na hilo, wapo waliofikia hatua ya kufanya upasuaji wa urembo kuongeza makalio, huku wengine wakivaa ‘tight’ maalumu kuonyesha umbo kubwa kuliko lilivyo asili.

Hata hivyo, ukweli ni kuwa wenye maumbile hayo kwa asili hutokana na mkusanyiko mkubwa wa mafuta sehemu ya makalio na mapaja kwa juu, hivyo kuonekana zimejazia au zimechomoza zaidi nyuma, hali inayojulikana steatopygia.

Historia inaeleza hali hii ya kimaumbile kwa asili ipo kwa jamii za Kiafrika, hususani miongoni mwa watu wa Khoisan (San na Khoikhoi) wa Afrika Kusini na Namibia. Pia kwa baadhi ya wanawake wa Kibantu kutoka Kusini mwa Afrika na Mashariki na kwa kiasi kidogo kwa watu wa visiwa vya Pasifiki.

Kwa mujibu wa wataalamu, kibiolojia mafuta hayo hukusanyika chini ya ngozi na ni sehemu ya namna mwili unavyohifadhi nishati.

Steatopygia inaelezwa si ugonjwa, bali ni sifa ya kimaumbile kama ilivyo urefu, rangi ya ngozi au umbo la mwili.

Daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha maumbile kutoka Hospitali ya Aga Khan, Alex Njau, anasema steatopygia ni kuongezeka kwa mafuta katika makalio nje ya utaratibu kamili unaofaa.

“Huonekana zaidi katika familia au makundi fulani ya watu, hapa Afrika ni kama hapo Central Africa, maana yake ni kwamba huwa na mkondo wa vinasaba au jeni,” amesema na kuongeza:

“Japo mazingira pia huchangia kama baadhi ya vyakula na dawa ambazo huleta myumbo wa homoni, lakini zaidi kwa wanawake, japo na wanaume hupata, lakini hili halina utafiti uliokamalika.”

Hata hivyo, anasema hakuna utafiti wa kina kwenye hilo akieleza: “Halichukuliwi kama ugonjwa na halihatarishi maisha, zaidi tu labda maumivu ya mgongo kadri umri unavyoenda, kushindwa kutembea kwa haraka na kunyanyapaliwa kama upo nje ya jumuia isiyotambua umbile hilo.”

Amesema wanawake wenye maumbo kama hayo huweza kuzaa kawaida na maisha yanaendelea kwani si ugonjwa.

Dk Njau amerejea habari ya Sarah Baartman ya Europe (Ulaya) mwaka 1800, akisema ni mfano halisi wa hali kama hiyo.

Sarah Baartman (huitwa pia Sara Baartman au Saartjie Baartman) alikuwa mwanamke wa asili ya Khoikhoi kutoka Afrika Kusini, ambaye maisha yake yaligeuka kuwa ishara ya ubaguzi wa rangi, unyanyasaji wa kijinsia na unyonyaji wa kibinadamu katika historia ya ukoloni wa Ulaya.

Alitumika kama kivutio cha maonyesho kutokana na umbo la mwili, hususan makalio makubwa – steatopygia, hali ambayo ni ya kawaida miongoni mwa baadhi ya wanawake wa jamii za Khoisan.

Mwaka 1810 akiwa mdogo Sarah Baartman alipelekwa Uingereza na mfanyakazi Mholanzi aliyemuahidi utajiri na kazi ya kuonyeshwa kama kivutio cha asili, badala yake alitumiwa vibaya na kuonyeshwa kwenye maonyesho ya wanyama ya London na baadaye Paris, ambako watu walimlipa kuona mwili wake akiwa takribani mtupu.

Dk Njau anasema tiba kwa wenye maumbile hayo kwa sasa inawezekana kwa wale wasioyapenda.

“Kwa namna sayansi ya matibabu inavyobadilika, baadhi ya wanawake na wanaume hufanyiwa upasuaji kuondoa mafuta haya na kuurekebisha mgongo,” amesema.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema makalio yanapokuwa makubwa hugeuka mzigo na kuwanyima raha wahusika, kuwasababishia maradhi ya ngozi na kuwa kwenye hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza.

“Mkusanyiko mkubwa wa mafuta kwenye makalio na mapaja kwa juu husababisha sehemu hizo kuwa pana, zenye umbo la duara au lililochomoza sana. Hali hii si ugonjwa, bali ni sifa ya kiasili ya mwili inayohusiana na urithi (genetics)” amesema.

Dk Nkoronko amesema wengi wenye maumbo hayo hupatikana zaidi miongoni mwa makabila ya Afrika Kusini, kama vile Khoisan (Bushmen) na Hottentot, pia baadhi ya wanawake kutoka Afrika ya Kati na Mashariki.

“Kwa watu hawa, steatopygia inachukuliwa kama alama ya uzuri au uzazi, kihistoria ikihusishwa na umbo la kike linalovutia. Watafiti wa Ulaya waliitambua kwa mara ya kwanza katika karne ya 19, hasa walipokutana na wanawake wa kabila la Khoisan,” amesema.

“Wataalamu wengine wanaamini ni njia ya mwili kuhifadhi nishati au kulinda viungo vya uzazi kwa wanawake wanaoishi katika mazingira magumu kama jangwani. Si tatizo la kiafya, bali ni sifa ya kimaumbile inayotofautisha baadhi ya makabila na watu kwa asili yao ya kijenetiki,” amesema.