Wakuu wa vyombo vya habari watoa tamko kulinda amani, Manyerere alikosoa

Dar es Salaam. Wakuu wa vyombo vya habari na wahariri waandamizi nchini wamepitisha azimio la amani wakisisitiza kulinda amani, maadili ya kitaaluma na mshikamano wa kitaifa kuelekea uchaguzi mkuu.

Azimio hilo lililotiwa saini na viongozi wa vyombo vya habari leo Jumamosi Oktoba 25, 2025, limeainisha mambo 12 ya msingi katika kuhakikisha Taifa linaendelea kudumisha amani na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi nas baadaye.

Akisoma azimio hilo, Mkurugenzi wa vituo vya habari vya ITV na Radio One, Joyce Mhavile ametaja mambo hayo 12 akianza kwa kukumbusha historia ya taifa kuwa lilipata uhuru wake kwa mazungumzo hivyo bila kugombana.

“Tanzania ilipata uhuru wake mwaka 1961 kupitia jitihada za majadiliano, mazungumzo na hoja za wanasiasa, wapigania uhuru bila kugombana. Watanzania tuna wajibu wa kuendeleza kujenga demokrasia yetu kwa majadiliano na hoja, tukipingana bila kupigana,” amesema.

Katika azimio la pili, wahariri wameridhia kwa pamoja kuwa demokrasia ni mchakato unaokua hatua kwa hatua, wakisisitiza kuwa haichipui na kukua kwa haraka hivyo jitihada endelevu zinahitajika kufikia viwango vinavyostahili.

“Demokrasia yetu bado ni changa, siyo kama mtoto wa nyumbu anayezaliwa sasa na hapo hapo akaanza kukimbia. Tunahitaji kuihudumia na kuilinda kwa hekima,” amesema Joyce.

Aidha, wahariri hao wamesisitiza juu ya wajibu wa vyombo vya habari katika kujenga demokrasia, wakikiri kuwa vyombo vya habari vinao wajibu mkubwa katika kujenga demokrasia ya vyama vingi nchini.

Katika azimio la nne, wakuu hao wa vyombo vya habari wamekumbusha umuhimu wa kujifunza kutokana na historia ya migogoro ya kisiasa nchini, hasa Zanzibar mwaka 2001, wakihimiza mafunzo yanayotokana na matukio hayo kuliepusha Taifa.

Kupitia azimio la tano, wahariri wametahadharisha juu ya athari za ubinafsi wa kisiasa na propaganda, wakitolea mifano ya mataifa yaliyowapa nafasi wanasiasa wenye sifa hizo kuhatarisha amani na mshikamano wa mataifa yao.

“Tumeshuhudia machafuko, mateso na mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia katika nchi nyingine, yalisababishwa na ubinafsi wa wanasiasa waliotumia propaganda kugawa watu bila kujali maslahi mapana ya mataifa yao,” amesema Joyce.

Akisoma azimio la sita, Joyce amekemea kwa nguvu zote kauli za uchochezi na lugha za chuki, zikiwemo zinazohamasisha wananchi kufanya vurugu, kuchoma vituo vya mafuta au mali nyingine, akisema siyo tu kosa kisheria bali ni kinyume na utu wa Mtanzania.

Katika azimio la saba, wahariri hao wameonya kuwa migogoro mingi ya Afrika ilianzia na kauli ndogo za chuki zilizopuuzwa na kuyatumbukiza mataifa yao katika machafuko ya kisiasa, vita vya wenyewe kwa wenyewe na mauaji ya kimbari.

Wameyataja mataifa jirani kama Rwanda, Kongo, Sierra Leone na Somalia ambayo yamekuwa katika histoiria ya migogoro na uvunjifu wa amnani kutokana na kile walichokiita uendawazimu wa kihalaiki, wakitoa wito wa kuepuka  tabia hizo.

“Tanzania imekuwa kisiwa cha amani kwa sababu ya misingi ya mazungumzo na maridhiano iliyoasisiwa na waaasisi wa Taifa letu, walioweka misingi ya kukaa mezani kumaliza tofauti zetu, na kuifanya nchi yetu kuwa tumaini la wakimbizi,” amesema Joyce.

Awali, akizungumza katika mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk Ayoub Rioba, amesema kikao hicho kimekuja kutokana na maombi ya wakuu hao wa vyombo  wakitaka kujadili na kuja na mkakati wa pamoja katika kulinda amani ya Taifa.

“Tumekutana hapa kufuatia maombi na maoni ya wakuu mbalimbali wa vyombo vya habari ambao wamekuwa wakisema ipo haja ya kukutana na kuweka mkakati wa pamoja juu ya kutunza amani na kweli tukakutana na kulikuwa na kukubaliana kwa hali ya juu,” amesema.

Kwa upande wake, mhariri na mwanahabari mkongwe nchini, Manyerere Jackton ametoa maoni kuhusu azimio hilo, akisema lilipaswa kwenda mbali kwamba haki ikitendeka, amani hujijenga yenyewe.

Manyerere amesema ingependeza iwapo ndani ya tamko hilo kungewekwa maneno ya aina hii: “Tunazihimiza taasisi zote zinazohusika na usimamizi wa uchaguzi, hususan Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), vyama vya siasa, na vyombo vya ulinzi na usalama, kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unazingatia misingi ya haki, uwazi na usawa kwa pande zote.

“Isivyo bahati, sisi wahariri, kama makundi mengine, tumeingizwa kwenye darasa la kuaminishwa kwamba wenye wajibu wa kulinda amani na utulivu wa taifa ni wanaotawaliwa tu,  wapigakura.”

Kwa mujibu wa Manyerere matamko ya wanasiasa, viongozi wa dini, wagombea, wapambe wa vyama, polisi na viongozi wa vyombo vya utoaji haki mara nyingi huonyesha kana kwamba jukumu la kulinda amani ni la wananchi pekee.

Hata hivyo, Manyerere kwenye maoni yake amesema azimio la wakuu wa vyombo vya habari lingewahimiza watawala na wasimamizi wa vyombo vya utoaji haki kutenda haki kwa wapigakura na wagombea wote, ili kuondoa malalamiko yanayosababisha uvunjifu wa amani.

“Tunakosea mno kuamini kuwa kulinda amani maana yake ni wananchi kukaa kimya hata wanapoona wanadhulumiwa; au haki zao za kuchagua na kuchaguliwa zikivunjwa.

Amesema azimio lingetenda haki kwa pande zote kuwaasa wananchi walinde amani, lakini pia kuzikumbusha mamlaka za nchi kutenda haki ili kuondoa maung’uniko ya dhuluma ambayo mwisho wake yanaweza kuwa chanzo cha machafuko.

“Sisi wahariri ni mhimili wa nne usio rasmi wa dola. Tunapaswa kuwa kilainishi au mafuta ya kupunguza msuguano katika mifumo ya kijamii na kisiasa.

“Tutakuwa tunafanya kosa kubwa tukidhani wajibu wa wananchi ni kukubali lolote linalotolewa kwao, ikiwamo wizi wa kura au ghiliba huku vyombo vya usimamizi wa uchaguzi vikiendelea kuhubiri amani bila haki,” amesema.