MABAO mawili ya kipindi cha kwanza kutoka kwa nahodha msaidizi, Dickson Job na Pacome Zouzoua, yameifanya Yanga kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiiondosha Silver Strikers ya Malawi.
Yanga imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa leo Oktoba 25, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Matokeo hayo yamefanya kuwa Yanga 2-1 Silver Strikers kutokana na mechi ya ugenini wenyeji kushinda 1-0.
Yanga imekuwa timu ya pili kutoka Tanzania kutinga hatua ya makundi michuano ya CAF msimu huu baada ya jana Azam FC kufanya hivyo ikiifunga KMKM mabao 7-0 na kuifanya ifuzu kwa jumla ya mabao 9-0 upande wa Kombe la Shirikisho Afrika.
DUBE MAMBO MAGUMU
Licha ya Yanga kuibuka na ushindi huo, lakini haikuwa siku nzuri kwa mshambuliaji Prince Dube ambaye ndani ya dakika 80 alizocheza kabla ya kufanyiwa mabadiliko na nafasi yake kuchukuliwa na Andy Boyeli, amekosa nafasi za wazi zaidi ya nne.
Dube ambaye alianzishwa kwenye mechi hiyo ya uamuzi kwa Yanga kutinga hatua ya makundi, hakuwa na maajabu, ndipo Kocha Patrick Mabedi akamfanyia mabadiliko.
MOTO WA YANGA
Dakika 15 za kwanza, zilikuwa na moto upande wa Yanga iliyoingia na kasi ikisaka bao la mapema hali iliyofanya wapinzani wakose muda mwingi wa kujipanga. Dakika ya tano, Yanga ikapata kona ya kwanza.
Mpira wa kona uliochongwa na Mohamed Doumbia, ukaunganishwa na Job na kutikisa nyavu hali iliyoibua shangwe kutoka kwa nyomi la mashabiki waliojitokeza uwanjani baada ya mechi hiyo kutokuwa na kiingilio.
Licha ya kupata bao la kuongoza dakika ya sita, Yanga iliendeleza kasi ikisaka bao lingine kwa kucheza mpira wa kuonana, wachezaji wakipasiana pasi safi zilizokuwa zinaibua shangwe majukwaani.
Dakika ya kumi, Pacome Zouzoua nusura aiandikie Yanga bao la pili, lakini shuti lake kali alilopiga nje ya 18 liligonga mwamba wa pembeni na kurudi ndani.
Wapinzani ni kama walipotezwa na kasi ya Yanga kwani kila wakigusa mpira walikuwa wanakosa mwanya wa kupenya na kujikuta wanapoteza mipira na kuendelea kuwapa wenyeji wa mchezo kuutawala. Dakika ya 18 walipata kona nyingine haikuzaa matunda kutokana na umakini wa walinzi wao.
Yanga iliendelea kucheza mpira mzuri tofauti na mechi za nyuma chini ya Roman Folz, dakika ya 23 Mudathir Yahya aliomba kufanyiwa mabadiliko na kusababisha kikao cha muda kati ya nahodha na baadhi ya wachezaji akiwemo Djigui Diarra ambaye aliitwa kutoa mawazo juu ya nani achukue nafasi yake.
Baada ya kikao cha muda, Job alienda kuzungumza na kocha, kabla hajarudi uwanjani aliitwa nahodha wa kikosi hicho, Bakari Mwamnyeto ambaye alikuwa benchi, akatoa maelekezo kidogo, ndipo uamuzi wa mabadiliko ulipofanyika.
Kocha alimuingiza Edmund John kuchukua nafasi ya Mudathir, huku Maxi Nzengeli akatoka pembeni na kurudi kati kupishana na kiungo huyo mshambuliaji aliyeenda pembeni.
Dakika ya 33 baada ya pasi nyingi kuelelea lango la wapinzani, Maxi Nzengeli alimtengenezea nafasi Pacome Zouzoua ambaye alikwamisha mpira nyavuni na ubao kusoma Yanga 2-0 Silver Strikers.
Bao lililopachikwa nyavuni na Pacome lilimkosha shabiki ambaye alivamia uwanja na kutolewa na walinzi waliojazwa Uwanja wa Mkapa kwa ajili ya ulinzi.
Kipindi cha pili timu zote ziliingia kwa kuheshimiana na kushambuliana kwa zamu, Yanga licha ya kufunga mabao mawili, ilionyesha kuendelea kuhitaji kutafuta bao lingine huku wapinzani wakizidiwa mbinu kila walipopata mipira ilipotea.
Mwanzoni mwa kipindi cha pili katika dakika 15 za kwanza, hazikuwa na mwenyewe, timu zote zilionekana kuzurula uwanjani bila mipango, dakika ya 54, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wa Yanga alionyeshwa kadi ya njano ikiwa ni ya kwanza katika mechi hiyo.
Kwa kiasi fulani, Yanga ilionekana kuridhika na mabao hayo, hali iliyofanya Silver Strikers kuamka na kushambulia, lakini haikubadilisha ubao wa matokeo. Hata hivyo, Yanga imeonekana kutokuwa vizuri kiuchezaji kipindi hicho na kuwapa mwanya wapinzani wao kutawala.
Kiwango cha Yanga kipindi cha pili, kimezua gumzo na kuonekana kuna haja ya wachezaji kuongezewa utimamu wa kupambana dakika tisini bila kuchoka.
Pia Yanga ilifanya mabadiliko mengine kwa kumtoa Doumbia, nafasi yake ikachukuliwa na Offen Chikola.
Kwa ushindi huo, Yanga imefuzu hatua ya makundi michuano ya CAF kwa msimu wa nne mfululizo baada ya 2022-2023 (Kombe la Shirikisho Afrika) ambapo timu ilifika hadi fainali. Kisha 2023-2024 katika Ligi ya Mabingwa Afrika, timu ilikwenda hadi robo fainali na 2024-2025, ikaishia makundi.
YANGA: Djigui Diarra, Israel Mwenda, Mohamed Hussein, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Prince Dube, Mohamed Doumbia na Pacome Zouzoua.
SILVER STRIKERS: George Chikooka, McDonald Lameck, Maxwell Paipi, Nickson Mwase, Dan Sandukila, Chikondi Kamanga, Levison Maganizo, Uchizi Vunga, Stanie Davie, Andrew Joseph, Zebron Kalima.
