SAA chache baada ya Rais wa Klabu ya Yanga kuthibitisha kuwa usiku huu wanatangaza kocha mkuu wa klabu hiyo, Mwanaspoti limenasa jina lake.
Yanga tayari imemalizana na makocha watatu ambao muda wowote kuanzia sasa watatambulishwa ndani ya timu hiyo ambao ni kocha mkuu, kocha msaidizi na kocha wa makipa.
Mwanaspoti limenasa majina ya makocha hao ambapo kocha mkuu anayechukua nafasi ya Romain Folz ni Pedro Soares Conçalves.
Kocha huyo atasaidiana na Filipe Pedro huku kocha wa tatu wa makipa, Fernando Perreira.
Makocha hao watatangazwa usiku huu kuendelea alipoishia Patrick Mabedi ambaye amekaimu nafasi ya kocha mkuu baada ya Folz kumalizana na Yanga kwa makubaliano ya pande mbili, Oktoba 18, 2025.
Pedro raia wa Ureno, anajiunga na Yanga akiwa na rekodi ya kuifikisha Angola hatua ya robo fainali kwenye Afcon iliyopita.
Pia aliiongoza Angoka katika michuano ya CHAN 2024 iliyofanyika mwaka 2025 nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Kuthibitisha hilo, Hersi katika mazungumzo yake baada ya leo Yanga kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuitandika Silver Strikers mabao 2-0, amesema wanashusha kocha mwenye rekodi ya kuipeleka timu hatua ya robo fainali.
“Tunatambulisha kocha mwenye ubora mkubwa, mwenye uzoefu mkubwa, kocha atakayetuvusha kwenye mashindano haya hadi hatua inayofuata,” amesema Hersi wakati akisisitiza ubora wa kocha huyo mpya ambaye atatambulishwa saa chache kuanzia sasa.