Dar es Salaam. Benki ya Absa Tanzania kwa kushirikiana na ASA Microfinance, imeadhimisha miaka minne ya mafanikio tangu kuanzishwa kwa ushirikiano wao mwaka 2022.
Ushirikiao huo umewezesha wanawake wajasiriamali 50,000 nchini kupata mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh40 bilioni.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumapili Oktoba 26, 2025 wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Obedi Laiser amesema benki yao inaona uwezeshaji wa wanawake kama dhamira ya kudumu, si mradi wa muda. “Kwa kuwawezesha wanawake kupata mitaji na kukuza biashara zao, tumeona mabadiliko makubwa yanayogusa familia, ajira, elimu na ustawi wa jamii,” amesema Laiser.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa ASA Microfinance Tanzania, Muhammad Shah Newaj amesema ushirikiano huo umeleta mageuzi katika maisha ya wanawake waliokuwa nje ya mfumo rasmi wa kifedha.
“Kupitia msaada wa Absa, tumeweza kupanua huduma zetu na kufikia maelfu ya wanawake wajasiriamali nchini. Hatufadhili biashara pekee, bali tunafadhili matumaini na fursa zinazoinua vizazi,” amesema.
Katika kipindi cha miaka minne, ushirikiano huo umehusisha utoaji wa mikopo sambamba na mafunzo ya elimu ya kifedha.
Hivi karibuni, wanawake 50 kutoka Dar es Salaam walishiriki mafunzo maalumu kuhusu upangaji bajeti, akiba, uwekezaji na utunzaji wa kumbukumbu, hatua inayolenga kuhakikisha mikopo inachochea ustawi wa kudumu.
Mpango huo ni sehemu ya mkakati wa uwajibikaji wa kijamii wa Absa, unaolenga kujenga ujumuishaji wa kifedha na kuunga mkono ajenda ya kitaifa ya kuwawezesha Watanzania wote hasa wanawake, kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi.
