KIKWETE AHITIMISHA KAMPENI ZA CCM MAJIMBO MATANO YA UNGUJA, ASEMA CCM NI CHAMA CHA KUTENDA NA SIO CHA MANENO MANENO

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amesema CCM si chama cha maneno maneno bali ni chama cha vitendo, akisisitiza kuwa chama hicho kitaendelea kutekeleza ahadi zake kwa wananchi kwa vitendo.

Dkt. Kikwete alitoa kauli hiyo jana jioni katika Uwanja wa Jambiani, Mkoa wa Kusini Unguja, alipohitimisha rasmi kampeni za CCM katika majimbo matano ya mkoa huo ya Tunguu, Chwaka, Uzini, Paje na Makunduchi kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Akihutubia mamia ya wananchi waliofurika uwanjani hapo, Dkt. Kikwete alisema CCM imeendelea kuwa chama cha kuaminika kwa Watanzania kutokana na utekelezaji wa Ilani yake kwa vitendo na kwa ufanisi mkubwa. 

Alisema kuwa Ilani ya CCM imefikiwa kwa zaidi ya asilimia 85 na miradi iliyosalia inaendelea kutekelezwa kwa kasi. “CCM si chama cha maneno, ni chama cha kutenda. Tumetekeleza Ilani yetu kwa zaidi ya asilimia 85, na miradi inayobaki inaendelea. Huu ndio uthibitisho kwamba ahadi za CCM ni deni, na tunalilipa kwa vitendo,” alisema Kikwete huku akishangiliwa na wananchi.

Aidha, Dkt. Kikwete aliwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa uongozi wao bora na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo katika pande zote za Muungano. 

Alisema viongozi hao wameonyesha uongozi wa wazi, wa kisasa na wenye matokeo chanya kwa wananchi. “Wananchi wanampenda kiongozi anayesema ukweli na anayetekeleza. Dkt. Samia na Dkt. Mwinyi wameonyesha uongozi wa vitendo,” alisema.

Dkt. Kikwete aliongeza kuwa chini ya uongozi wa viongozi hao, huduma za jamii zimeimarika kwa kasi kubwa, zikiwemo afya, elimu, maji na barabara. Alisema Zanzibar ya sasa imepiga hatua kubwa kimaendeleo ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita, huku akitaja mafanikio kama kuongezeka kwa upatikanaji wa maji safi kutoka shehia 54 hadi 62, na ongezeko la uzalishaji wa samaki kutoka tani 5,606 hadi tani 12,155.

Pia alitaja mafanikio katika elimu ambapo kiwango cha ufaulu wa kidato cha nne kimepanda hadi asilimia 98.5, huku shule, maabara na hospitali mpya zikijengwa maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba. “Hospitali za Kitogani, Mwera Pongwe na Makunduchi ni ushahidi wa kazi nzuri ya serikali ya CCM,” alisema Kikwete.

Akiwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, Dkt. Kikwete alisema ni muhimu kila Mtanzania kutumia haki yake ya kikatiba kwa amani na utulivu. “Usikubali mtu akuambie usipige kura, hiyo ni haki yako ya kikatiba. Ukiikosa, utamwachia asiye na nia njema ashinde,” alisisitiza.

Kikwete alisema serikali ya CCM itaendelea kuimarisha uchumi, kuongeza ajira zaidi ya 350,000, kukuza sekta ya utalii na kuanzisha hifadhi ya mafuta Zanzibar kupitia Ilani ya 2025–2030 yenye kaulimbiu ‘Kazi na Utu, Tunasonga Mbele’.

Aliwataka wananchi wa Zanzibar na Tanzania Bara kulinda amani na umoja uliopo, akisema CCM itaendelea kuendeleza misingi ya ASP na TANU ya usawa, umoja na maendeleo kwa wote. 

“Wachochezi walijaribu huko nyuma hawakufaulu, na hawatafaulu kamwe. CCM imesimama kwa misingi ya Mapinduzi ya 1964 na itaendelea kulinda umoja wa Wazanzibari na Watanzania,” alisema.

Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Kikwete aliwataka wananchi wote kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kuhakikisha ushindi wa CCM unapatikana kwa kishindo. 

“Tarehe 29 Oktoba tujitengeze historia. Tuchague Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuwa Rais wa Zanzibar na wagombea wote wa CCM,” alisema huku akishangiliwa.

Katika mkutano huo wa kufunga kampeni, Dkt. Kikwete aliwanadi kwa nguvu wagombea wote wa chama hicho ikiwa ni pamoja na Bi. Wanu Hafidh Ameir, mgombea ubunge wa Jimbo la Makunduchi, pamoja na wagombea wa uwakilishi wakiwemo Issa Haji Ussi (Gavu) wa Jimbo la Chwaka, Simai Mohamed Said Mpakabasi wa Jimbo la Tunguu, na Saidi Azani Hassani (Msingiri) wa Jimbo la Uzini.

Kutoka Wilaya ya Kusini walihusishwa pia Dkt. Mwalimu Haroun Ali Suleiman (Makunduchi) na Jaku Hashim Ayoub (Paje), ambao wote walipata fursa ya kusalimiana na wananchi na kutoa salamu za kuhitimisha kampeni kwa matumaini makubwa ya ushindi.