KUJENGA IMANI ZAIDI YA KURA: Jinsi uandishi wa habari kwa kufuata maadili unavyounda mustakabali wa Tanzania tuitakayo

Tanzania ipo katika hatua muhimu sana ya kihistoria, inayokwenda kuunda mustakabali wa Taifa letu.

Namna tunavyopitia kipindi hiki, ndivyo tutakavyojenga uimara wa msingi wa maendeleo yetu ya kitaifa katika awamu inayofuata.

Chaguzi zinaweza kutugawa, hasa tunapokuwa katika mkondo wa ukuaji unaotia matumaini. Hata hivyo, ni wajibu wa kikatiba unaofanyika kila baada ya miaka mitano na kila raia ana haki ya kuchagua viongozi watakaoliongoza Taifa letu.

Kama nguzo ya nne ya utawala, vyombo vya habari vina jukumu la kulinda misingi ya demokrasia na kukuza jamii inayofikiri kwa umakini zaidi.

Tunaweza kutimiza jukumu hili kupitia uandishi wa habari unaowawajibisha viongozi na wananchi sawasawa.

Katika maktaba na hifadhi za kumbukumbu za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), uchunguzi wa kina wa Kiswahili unaokutana na uandishi makini, zipo habari zilizobadilisha maisha ya watu na taasisi. Kampuni hii, inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen, na Mwanaspoti, imeendelea kuwa daraja muhimu la upatikanaji wa taarifa sahihi zikiwamo za afya, uchumi, siasa, elimu na michezo na popote kunapohitaji suluhisho, uandishi wa habari huanza mbele.

Tumeshuhudia nguvu hii kwa macho yetu wenyewe kupitia kalamu za waandishi hawa:

•             Herieth Makwetta, alibaini upungufu wa vifaa vya saratani, wiki iliyofuata, mashine ziliahidiwa kufikishwa kwenye maeneo husika.

•             Elias Msuya, alifichua uhaba wa maji Mbezi Msumi, visima vilichimbwa na viongozi wakachukua hatua.

•             Juma Issihaka, alichunguza usalama wa vivuko na kusababisha kusitishwa kwa safari kabla ya maafa kutokea.

•             Charles Abel, aliripoti kuhusu uharibifu wa viwanja vya michezo, hatua zilizochukuliwa mara moja kurekebisha bila malalamiko.

•             George Helahela; aligeuza mijadala ya haki za ardhi kuwa majukwaa halisi ya kisheria.

•             Alawi Masare; alichambua masuala ya masoko na michezo ya kubahatisha na kuchochea mijadala ya kitaifa iliyoifikia hadi Ikulu.

Haya si mafanikio ya bahati, ni ushahidi kuwa uandishi wa habari wa maadili unaofundisha, unaoelimisha na unaosukuma maendeleo mbele.

Kila uchaguzi tunapouripoti, wajibu wetu huzidi kuwa mkubwa. Tunakusudia kujenga, si kubomoa.

Tunataka kuhabarisha, si kupotosha. Kanuni kuu za uandishi wa habari ndizo zitakazotuongoza tena wakati Taifa linachagua mustakabali wake Oktoba 29, 2025.

MCL imeripoti habari za uchaguzi mkuu wa Tanzania mara tano tangu mwaka 2000. Kila mzunguko ulitupa changamoto chanya, si kama waandishi tu, bali kama walinzi wa demokrasia na daraja kati ya Serikali na wananchi wake. Kila uchaguzi umetutia nguvu zaidi ya kufanya kitu kikubwa zaidi kwa mustakabali wa Watanzania na Taifa kwa ujumla.

Tunadumisha usawa wa habari:

Kila taarifa ya uchaguzi itapitiwa kwa umakini kuhakikisha uwiano, mikutano ya kampeni na foleni za wapiga kura, kanuni na matumaini. Tunaripoti ukweli kama ulivyo, si kama unavyoonekana au kufikiriwa.

Uchaguzi hauishi kwenye sanduku la kura. Wajibu wetu unahusisha siku na miezi inayofuata, kuhakikisha amani inadumu na kila sauti inasikika.

Habari zilizopita zimethibitisha kuwa uandishi wa heshima, wa kina na wenye weledi unaweza kutatua migogoro badala ya kuichochea.

Tunapozungumzia kuangalia zaidi ya kura, tunamaanisha kulinda Kisiwa chetu cha Amani. Hebu uandishi wa habari uendelee kufungua milango, si majeraha. Kusiwe na kauli za kugawa. Kusiwe na vichwa vya habari vya kuchochea.

Zana za uangalizi wa pamoja

Tunatoa vidokezo vitano vya haraka vya kugundua upotoshaji wa habari:

1.            Thibitisha chanzo cha habari.

2.            Angalia tarehe ya taarifa.

3.            Tafuta mtazamo tofauti.

4.            Shiriki habari ukiweka muktadha.

5.            Fikiri kabla ya kuchukua hatua.

Waandishi wetu wameonyesha jinsi ukweli uliothibitishwa unavyookoa maisha na kuunda sera. Tumia zana hizi. Fundisha wengine. Linda ukweli kwa pamoja.

Majadiliano yanayounda Taifa

Tuwe wenyeji wa midahalo jumuishi jijini Dar es Salaam, ikijumuisha viongozi na wananchi, washindi na wapinzani, vijana na wazee. Tuendeshe warsha ambazo wanafunzi watajifunza namna ya kuchambua habari kwa uwajibikaji.

Haturuhusu sauti yoyote ibaki peke yake. Tunakaribisha ushirikiano katika vyombo vyote vya habari, vya Serikali, binafsi na hata vya dini.

Tunataka kuripoti kinachounganisha, si kinachotutenganisha.

Tujenge, tusivunje. Tuiweke Tanzania katika habari zilizo sahihi na salama.