JKT Tanzania wamekuja kivingine msimu huu, kwani wamedhihirisha kuwa pambano la Ligi Kuu Bara dhidi yao haliishi hadi filimbi ya mwisho ya mwamuzi itakapopulizwa ndipo mpinzani anatakiwa kushangilia.
JKT Tanzania iliyomaliza nafasi ya sita msimu uliopita Ligi Kuu Bara, msimu huu imekuwa na mwendo mzuri na kabla ya jana ilikuwa nafasi ya pili ikikusanya pointi saba katika mechi tano.
Maafande hao wanaonolewa na kocha Ahmad Ally, juzi jioni kwenye Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam walichomoa bao ikitumia dakika nne za nyongeza dhidi ya Mbeya City na kutoka sare ya mabao 2-2,
ikiwa ni sare ya nne kati ya mechi tano ilizocheza ikishinda moja mbele ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union iliyowanyuka 2-1 katika pambano lililopigwa Septemba 22, 2025 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jiji Tanga.
JKT Tanzania ilianza msimu huu na staili hiyo ya kuchomoa mabao dakika za jioni dhidi ya Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mechi iloyopita Septemba 18.
Maafande hao walichomoa bao la wenyeji katika dakika ya 87 kupitia Paul Peter ambaye alirudia tena timu hiyo ilipomenyana na Azam FC na kutoka sare ya 1-1.
Mfungaji huyo aliyetua klabuni hapo msimu huu akitokea Dodoma Jiji, alifunga bao hilo dakika ya 90+3 baada ya Azam kuongoza kwa muda mrefu katika mechi hiyo iliyopigwa Oktoba Mosi, 2025 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo. Kama ulidhani JKT ilibahatisha mechi mbili, basi unakosea kwani wikiendi iliyopita kwenye uwanja huohuo timu hiyo ilirudia kitendo hicho ikiikatili Namungo.
Safari hii mfungaji alikuwa ni Saleh Karabaka aliyeitumikia Namungo msimu uliopita kwa kuchomoa bao dakika ya 90+1 baada ya wageni kutangulia kwa bao la Ally Saleh la dakika ya 53.
Ndipo juzi tena imerudia kwa Mbeya City baada ya Karabaka kufunga bao la pili dakika ya 90+4 akiiokoa JKT isipoteze mechi ya kwanza ya Ligi Kuu msimu huu. Mapema wenyeji Mbeya City inayoutumia Uwanja wa KMC kama wa nyumbani ilitangulia kwa bao la dakika 14 kupitia kwa Hamad Majimengi kabla ya Paul Peter kuchomoa dakika ya 65.
Vitalis Mayanga aliitanguliza Mbeya City kwa bao la dakika 75 na lililoonekana kama lingefanya matokeo yabaki yalivyo baada ya kuongezwa dakika nne, zilipobaki sekunde chache kabla ya mechi kumalizika, ndipo Karabaka akasawazisha.
Bao hilo la Karabaka limemfanya afikishe matatu akiongoza orodha ya wafungaji akiwa sambamba na Paul Peter pia wa JKT kabla ya mechi za jana, huku Mayanga akifikisha bao la pili.
Matokeo ya jumla kwa JKT katika Ligi Kuu kwa msimu huu, imeshinda mechi moja na kutoka sare nne ikifikisha pointi saba na mabao saba ya kufunga, ikiruhusu sita.
