Same. Wakati Jumatano Watanzania wakitarajia kufanya uchaguzi mwingine wa kihistoria kuwachagua viongozi watakaoliongoza Taifa kwa kipindi kingine cha miaka mitano, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, John Malecela, amewakumbusha kulinda na kudumisha amani.
Siku hiyo, Watanzania kutoka bara na visiwani watakuwa wakipiga kura kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar, wabunge wa Bunge la Jamhuri na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Hata hivyo, kama zilivyo chaguzi zingine zilizotangulia, joto la uchaguzi huambatana na matukio mbalimbali. Kwa mwaka 2025, kumekuwepo na taarifa za maandamano siku ya kupiga kura, huku wengine wakihamasisha wananchi kupiga kura kuchagua viongozi.
Kauli za Oktoba tunatiki, na zile za Oktoba tunatoka, zimeendelea kuchuana kwenye mitandao ya kijamii huku msisitizo wa Serikali, viongozi wa dini na makundi mbalimbali ni kudumishwa kwa amani na utulivu.
Kutokana na kauli hizo hasa kwenye mitandao ya kijamii, tayari Jeshi la Polisi limeonya kuwa, litadhibiti kila aina ya uhalifu na vitendo vya uvunjifu wa amani Jumatano, Oktoba 29 mwaka huu.
Hata hivyo, akizungumza na wazee wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, waliokwenda kumsabahi na kubadilishana naye mawazo kuelekea uchaguzi mkuu, Malecela amesema hakuna kitu cha thamani zaidi ya amani kwa Taifa lolote duniani.
Pia, amewaomba wananchi kuendelea kumwamini na kumpa dhamana mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika nyanja za kiuchumi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyoboresha huduma za kijamii nchini, chini ya uongozi wake.
Mkutano Mkuu wa CCM ulimpitisha Samia kuwania urais huku mgombea wenza wake akiwa Dk Emmanuel Nchimbi.
Uchaguzi wa mwaka 2025 unahusisha vyama18 na wagombea wa urais 17 akiwamo Samia na mgombea mwenza Dk Nchimbi (CCM), Salum Jumaa Mwalimu na Devotha Minja (Chaumma), Yustas Rwamugira na Amana Suleiman Mzee (TLP), Abdul Mluya na Sadoun Abrahman Khatib (DP), Saum Hussein Rashid na Juma Khamisi Faki (UDP).
Wengine ni Georges Busungu na Ali Makame Issa (Ada Tadea), Mwajuma Mirambo na Mashavu Alawi Haji(UMD), Twalib Kadege na Abdalla Mohamed Khamis (UPDP), Hassan Almas na Hamis Ali Hassan (NRA), Coaster Kibonde na Azza Haji Suleiman (Makini).
Pia, yumo Doyo Hassan na Chausiku Khatib Mohamed (NLD), Majalio Kyara na Satia Mussa Bebwa (Sau), Daud Mwaijojele na Masoud Ali Abdalla (CCK), Kunje Ngombare Mwiru na Chumu Abdallah Juma( AAFP), Haji Ambar Khamis na Dk Eveline Munisi (NCCR-Mageuzi), Gombo Samandito na Husna Abdallah (CUF) na Wilson Elias na Shoka Khamis Juma (ADC).
Katika mazungumzo yake na wazee mwishoni mwa wiki iliyopita, Malecela amesema uwepo wa kikundi cha watu wachache kuhamasisha wananchi wasiende kupiga kura na kupanga njama za maandamano siku ya uchaguzi, ni kinyume cha sheria na ni hujuma kwa Watanzania.
“Hakuna kitu chenye thamani kubwa duniani ama kwenye Taifa lolote kuliko amani, hii ndio inaamua mustakabali wa maendeleo ya nchi na familia zetu kwa jumla. Kumekuwepo na watu wanajaribu kutaka kutuingiza kwenye machafuko na migogoro, lakini siku zote wananchi na Serikali yao wamekuwa mstari wa mbele kuwakataa. Huu ni wakati mwingine wa kuwakataa watu wenye lengo la kutuvuruga,” amesema Malecela.
Pia, amesema kabla na baada ya Uhuru wa Tanganyika na baadaye kuzaliwa Tanzania, kipaumbele kikubwa ni amani na akaviomba vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi wote kwa jumla kuilinda Tanzania.
Kuhusu kauli za baadhi ya watu aliowaita wasio na nia njema kwa Watanzania, kujaribu kuhamasisha watu wasijitokeze kupiga kura, Mzee Malecela alisema: “Watanzania wajitokeze kwa wingi kuchagua viongozi wao. Kwanza, kwa nini usiende kupiga kura na sisi wenzako tukuonaje?
“Labda nianze na msingi wa Taifa letu, ambao ni jamii, familia ya mume, mke na watoto. Ningependa kutoa wito kwa viongozi wote wa familia kwamba siku hiyo, wakiamka, waamshe familia zao waende kupiga kura kwanza, ndipo warejee kushughulika na mambo mengine.
“Tukifanya hivyo, tutatimiza wajibu mkubwa wa kiraia ambao ni msingi wa kudumisha amani. Haki yako ni kuongozwa na Serikali uliyoipa kibali cha kukuongoza, na kibali hicho kinatolewa kwa kupiga kura. Kwa hiyo, Mtanzania yeyote asiyekwenda kupiga kura hatakuwa ameitendea haki nchi yake,” ameongeza.
Amebainisha kuwa, kila anayeitakia mema Tanzania lazima aende kupiga kura, akisema katikati ya safari watatokea watu watakaosema maneno ya kubeza, lakini wananchi wafahamu kwamba kwenye msafara wa mamba na kenge wapo.
Katika mazungumzo yake hayo na wazee wa Same, Malecela amesema kuwa Watanzania wanapaswa kuyaenzi na kulinda maendeleo makubwa ambayo kwake ameyataja kuwa ni miongoni mwa mambo yaliyomsisimua.
Ameitaja miradi ya reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) na mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) jijini Dar es Salaam.
Miradi mingine ni ujenzi wa barabara za lami zilizounganisha mikoa yote nchini, ujenzi wa vituo vya afya, shule za sekondari na mageuzi katika sekta ya kilimo, akisema Serikali inatoa pembejeo kupitia mfumo wa ruzuku, sasa mpango huo umepanuliwa na kujumuisha mbegu bora na zana za kisasa.
Mzee Malecela, mwenye umri wa miaka 91, alikuwa Waziri Mkuu chini ya Rais mstaafu, hayati Ali Hassan Mwinyi, kipindi ambacho Serikali iliratibu maoni ya wananchi na kuanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.
“Ndugu zangu wa Same, nawasihi mkipata nafasi nendeni Dar es Salaam, pandeni treni ya SGR mpaka Dodoma, kisha rudini Same kwa basi. Mtaona namna Tanzania ilivyobadilika,” amesema.
Kuhusu Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP), amesema mradi huo wa kuzalisha megawati 2,115 za umeme si wa kukagua kwa gari, kwa kuwa Mto Rufiji umebadilishwa kuwa bahari, jambo ambalo ni la kujivunia kama Taifa.
Kuhusu maendeleo ya usafiri jijini Dar es Salaam (BRT), amesema pamoja na changamoto zake, tatizo kubwa la jiji hilo limekuwa usafiri.
Hata hivyo, amesema Serikali imejitahidi kuboresha huduma hiyo kwa kuanzisha usafiri wa mabasi yaendayo haraka sehemu mbalimbali za jiji huku sehemu zingine zikiwa katika hatua tofauti za utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa miundombinu.
Amesema, licha ya hivi karibuni kutokea wahuni waliopiga mawe mabasi ya mwendokasi, tabia hiyo si ya kujenga bali kubomoa.
“Rais amejitahidi sana, mabasi yameongezwa na huduma inaendelea kutolewa kwa wananchi.
“Hata hivyo, hakuna wakati ambao Tanzania itamaliza matatizo yote. Matatizo huisha binadamu anapoingia kaburini. Mtu akiwa hai, changamoto ni sehemu ya maisha,” amesema.
Amesema Samia pia amefanya kazi kubwa kuunganisha barabara za mikoa kwa lami, na kubainisha kuwa, asubuhi wakati anaangalia runinga, aliiona ratiba ya wafanyabiashara wa visimbusi ikitangazwa kwamba wangekuwa Chunya na Mbambabay, jambo linalowezekana kutokana na barabara kuunganishwa kwa lami.
“Tanzania ni nchi kubwa. Ukichanganya Kenya, Uganda na Malawi bado Tanzania ni kubwa zaidi. Mtandao wa barabara kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, Dar es Salaam hadi Mwanza na Dar es Salaam mpaka Musoma zingeweza kumaliza matatizo ya miundombinu katika nchi ndogo kama Malawi kwa kujenga barabara zake kwa lami mijini hadi vijijini,” amesema mzee Malecela.
Amewaambia wazee waliomtembelea kuwa, maboresho katika huduma za afya yamefanywa kwa kiwango kikubwa, na kutolea mfano Jimbo la Same Mashariki, ambako mke wake anawania kuchaguliwa tena kama mbunge.
Amesema zamani kulikuwa na kituo kimoja cha afya, lakini sasa vipo zaidi ya vinne, akihoji, “hata kilimo kimeimarika; ukisimama hapo nje utaona mafanikio kwa macho. Tunapotaja mafanikio haya, hatusemi… Samia amemaliza matatizo yote. Tunachosema ni kwamba Watanzania tumshukuru na tumuenzi,” amesema.
“Tukisema tumuenzi, tuoneshe kwa vitendo. Uchaguzi unakuja. Ningependa wimbo wa Taifa letu uwe mmoja: Tarehe 29 Oktoba tunafanya nini?’ Wazee waliokusanyika nyumbani hapo wakaitikia, ‘Tunatiki.’ Huu uwe wimbo wa Watanzania mijini na vijijini,” amesema.
Amesema tatizo la ajira si la Tanzania peke yake, bali ni changamoto ya dunia nzima. “Ukienda Uingereza, Marekani au nchi nyingine, vijana hukabiliwa na changamoto hiyo, ingawa uzito wake unatofautiana. Hapa Afrika, changamoto ni ile ile, tofauti ni ukubwa wake,” amesema, akitoa wito kwa vijana kudai mambo kwa mipaka na kuthamini kilichopo.
“Tulikotoka ni mbali, tumetoka katika hali ya umaskini mkubwa. Leo, maendeleo ni dhahiri. Zamani tulikuwa na mabasi yenye vyoo? Hatukuwa nayo. Leo mabasi hayo yapo na abiria wanachagua mabasi wayapendayo. Hiyo ni hatua kubwa, Watanzania tunapaswa kujipongeza,” amesema.
Tanzania miaka mitano ijayo
Mzee Malecela amesema jukumu la kwanza la Watanzania liwe kumchagua Rais na wabunge huku akisema wakitokea CCM kwake itapendeza.
“Rais atakapokaa kwenye kiti chake, yeye ndiye atakayepanga majukumu kuanzia siku 100 za kwanza. Tayari amezunguka nchi nzima na kusikiliza matatizo ya wananchi. Hatupaswi kumwingilia au kumpa shinikizo. Ni lazima tumpe nafasi ya kusema, ‘nitafanya hiki na hiki,’ na kumruhusu atuongoze kwa dira yake,” amesema.
“Nikitazama miaka mitano ijayo, naiona Tanzania ikiwa mbali sana. Mungu ametujalia rasilimali nyingi, leo hakuna mkoa usiokuwa na machimbo ya dhahabu, hata Tanga, Pwani na maeneo mengine. Uwepo wa dhahabu unaimarisha uchumi wa Taifa. Ndani ya miaka mitano ijayo, Tanzania itapiga hatua kubwa kuliko nchi nyingi zinazotuzunguka.”
Amesema Tanzania inakwenda kuwa miongoni mwa nchi za ngazi ya juu kiuchumi na hakuna jirani atakayoweza kulingana nayo katika kasi ya maendeleo na ukuaji wa kiuchumi.
