Dodoma. Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtumba kwa Chama cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde, ameombwa kufikisha huduma ya maji ya uhakika na kuwapatia eneo la makaburi alipofanya kampeni kwenye kata ya Mtumba.
Katika mkutano wa kampeni alioufanya leo Oktoba 26,2025 katika kata hiyo, wananchi wameeleza kero wanazopata ambazo wangetamani kiongozi ajaye awasaidie kuzitatua.
Upungufu wa maji na eneo la maziko kwa wapendwa wao vilichukua nafasi kwa kutajwa na wengi lakini wakitaka mambo hayo yawekwe kwenye utekelezaji wa muda mfupi.
Shida ya maji mbali na Mtumba lakini maeneo mengine ya Kata za jimbo hilo yamekuwa na kilio cha kukosa maji au kuwa na upungufu wa kiasi kikubwa.
Akijibu hoja hizo, amewataka wananchi kuwa wapole kwani dawa ni kujitokeza kwa wingi na kuipigia kura CCM ili waingie na deni.
“Kilio hiki nilikisikia na kujionea mwenyewe nilipofanya ziara za mtaa kwa mtaa lakini ndugu zangu msiwe na hofu wala mashaka maana changamoto zetu zimekuja kutokana na ongezeko la watu, tutamaliza yote kwa kipindi kifupi,” amesema Mavunde.
Mavunde ambaye ni Waziri wa Madini, amesema suluhisho la kudumu kwa changamoto ya maji katika Jimbo la Mtumba na hasa kwenye Kata hiyo, ni mradi wa uchimbaji visima 18 katika mtaa wa Nzuguni A.
Amesema maji yatakayotoka katika eneo hilo yameonyesha kutosheleza mahitaji ya maji katika maeneo yenye upungufu na kwamba visima vitatu hadi sasa vimeshakamilika.
Mavunde amesema ndani ya muda mfupi wananchi wa Mtumba watasahau kabisa kero ya maji, kwani serikali ya awamu ya sita ina dhamira ya kweli ya kuboresha huduma za jamii vijijini na mijini, hivyo akaomba kwenye uchaguzi wamchague Samia Suluhu Hassan yeye (Mavunde) na diwani wa CCM ili iwe rahisi kufanya mawasiliano katika mahitaji yao.
Akizungumzia ukosefu eneo la makaburi, amesema jambo hilo ni muhimu na lazima atalifanyia kazi kwa haraka kwani baadhi ya mambo hayahitaji mjadala kama hilo la makaburi.
Katika mkutano huo Mavunde ameahidi kuanzisha ujenzi wa shule ya msingi katika Mtaa wa Majengo ili kuwapunguzia wanafunzi umbali wa kutembea wanapofuata elimu.
