HISIA zikawazidi kuwapanda, wawili hao walikuwa kama vile wako katika dunia nyingine. Kila mmoja wao alikuwa na shauku na mwenzake, wakaoneshana ufundi zaidi wa kupandishana hisia zao, aliyepagawa zaidi alikuwa ni Linnie ambaye alivutiwa zaidi na joto la mwili alilokuwa nalo Muddy.
Mwili wa mwanaume huyo ulikuwa na joto kali na kumfanya Linnie kuhisi faraja kiasi cha kumkumbatia kwa nguvu zake zote mwanaume huyo na kwa muda mrefu wote wawili walikuwa katika hisia kali za mapenzi ambazo zilipaswa kutendewa haki tangu siku za mwanzo walipokutana.
Muddy naye alikuwa amepagawa na urembo wa Linnie, alivutiwa zaidi na ngozi yake laini kama ya mtoto mchanga, macho yake ya bluu kama yale ya paka yaliyokuwa makali kiasi kwamba alihisi yaliyokuwa yakiuona moyo wake. Pamoja na mwili wake kuwa na baridi lakini alikuwa akivutia na kusisimua zaidi.
Naye akazidisha utundu wa kuipitisha mikono yake katika kila idara muhimu ya mwili wa Linnie, Muddy hamu yake ilikuwa kubwa kwa kuwa ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kumkumbatia mwanamke wa aina ya Linnie, mwanamke aliyekuwa katika ndoto zake muda mrefu. Mwanamke wa Kizungu mwenye hisia kali na msisimko mkubwa kuwahi kukutana naye.
Muddy alijitahidi kwa kila njia kuhakikisha anamfanya Linnie kuvutiwa zaidi na vitendo vyake kwa ajili ya kumaliza kiu zao ambazo zilistahili kutendewa haki. Alikuwa na uhakika wa kushinda pambano lake la kwanza ughaibuni. Alikuwa akitarajia kuandika historia ambayo haijawahi kuandikwa hata na mababu zake. Wakati wote Muddy alifanikiwa kuzifanya hisia za Linnie ziwe juu kama moshi wa kifuu.
Masikini mzungu wa watu alikuwa akitoa miguno ya hisia kuonyesha kwamba alikuwa akifurahia kila kitendo kilichokuwa kikifanywa na Muddy.
“You’ll kill me… (Utaniua…)” Linnie alisema huku akivuta pumzi zake kwa ndani mara kwa mara kama mgonjwa wa mafua aliyekuwa akihitaji msaada wa kupatiwa vidonge vya piriton.
Muddy wala hakumuonea huruma, ndio kwanza aliongeza juhudi na kuendelea kumpagawisha kwa mikono yake kusafiri katika kila idara ya mwili wa mwanamke huyo wa Kizungu.
Alikuwa akijua jitihada na ufundi wake ndizo zilizokuwa mkombozi wa yeye kupata maisha bora katika jimbo hilo la Ulaya. Alitaka kutengeneza historia ya maisha yake kuanzia hapo.
Masikini, Mzungu wa watu alikuwa ameshabadilika rangi kutoka kuwa wa njano na kuwa mwekundu, damu ilikuwa imemvilia mwili mzima, kama vile alikuwa amekunywa chupa za damu za kutosha.
Muddy aliamini angeweza kumaliza mechi siku hiyo na kuondoka na pointi tatu hata kama angefunga bao moja. Alimtoa Linnie chini ya kapeti na kumpandisha juu ya kochi kubwa lililokuwa sebuleni, alikuwa akijandaa kupiga hatua nyingine kubwa kutimiza kile alichokuwa akitaka kukitimiza.
Lakini kilitokea kitendo cha ghafla ambacho hakikutarajiwa, Linnie alimsukuma Muddy kwa mikono yake kisha akatoa sauti za kusimamisha pambano.
Alikuwa akimtaka Muddy asiendelee kufanya kile alichokuwa akitaka kukifanya kwani alimuona tayari mzimu wa mababu zake ulishampanda na alikuwa amefikia hatua sasa alikuwa akitaka kutambika.
Kitendo cha kusukumwa na Linnie kilimshtua Muddy kwani wote wawili miili yao ilionekana kujawa na shauku ya kutaka kuendelea hadi mwisho.
“Stop… stop… please… (acha… acha tafadhali),” alisema Linnie kisha akainuka na kuondoka katika eneo la tukio. Moja kwa moja alishika mwelekeo wa kwenda msalani.
Muddy alibaki pale akiwa amepigwa na butwaa asijue cha kufanya, alikuwa akijiuliza kwa nini Linnie alichukua uamuzi wa kusitisha pambano lao la kwanza. Pambano ambalo lingefungua njia ya mapambano mengine.
Kwa unyonge, kama mtu aliyenyang’anywa kata ya maji ukweni kabla hajameza hata fundo la maji, Muddy alijiinua kutoka chini alipokuwa ameketi baada ya kusukumwa na Linnie na kutoka kwenye kochi, bado alikuwa na mshangao wa tukio zima lililotokea.
Baada ya muda, Linnie alirejea na kuketi pembeni yake, huku uso wake ukiwa umetawaliwa na aibu. Hakuweza kumtazama Muddy usoni moja kwa moja kama alivyokuwa amefanya awali.
“I am sorry… (samahani…)” alisema Linnie na kumfafanulia Muddy kwanini alikuwa amesitisha mchezo wao uliokuwa unaelekea kwenye hatua muhimu.
Linnie alimwambia Muddy kulikuwa na hatua walizokuwa wanapaswa kuzipitia kabla ya kufikia katika hatua ya mwisho ya mchezo ule.
“I know you don’t know me well and I don’t know you well either…(Ninajua wewe hunijui vizuri na hata mimi sikufahamu vizuri…)” alisema Linnie huku akimwangalia Muddy kwa kumuibia.
“We should examine our health first before doing anything…(Tunapaswa kuchunguza afya zetu kwanza kabla ya kufanya chochote…)” aliendelea kuzungumza Linnie kwa sauti yake iliyokuwa laini.
Muddy hakuwa na budi kukubaliana na uamuzi huo wa Linnie ingawaje ilikuwa kwa shingo upande. Alikuwa mnyonge kama mtu aliyekosa chaza ndani ya kisahani cha dhahabu.
***
Kuanzia siku hiyo mambo yalibadilika, milango ya hisia zao ikafunguliwa na kuwaacha kuwa huru. Wawili hao wakakubaliana kuingia katika uhusiano wa mapenzi, wakawa wapenzi, ingawaje bado walilinda mipaka yao kwa kila mmoja kuendelea kulala katika chumba chake hadi pale walipoenda kupima afya zao ndipo walipoanza uhusiano wao rasmi.
“You impressed me from the first day I saw you at the airport. (Ulinivutia tangu siku ya kwanza nilipokuona pale uwanja wa ndege),” alisema Linnie kumwambia Muddy.
“I don’t know why I had feelings for you and I believed you would be my savior in that saga. (Sijui kwanini nilikuwa na hisia na wewe na niliamini wewe ndiye ungekuwa mwokozi wangu katika sakata lile),” alijibu Muddy akikumbusha siku ya kwanza walipoonana.
“That day I made a plan, I told some of my colleagues to delay leaving until night (Siku ile nilipanga mpango, niliwaambia baadhi ya wenzangu wakucheleweshe kuondoka hadi usiku),” alisema Linnie na kumfanya Muddy kuendelea kumshukuru kwa wema wake.
“I’m not surprised because your eyes were speaking the language of love since you came to talk to me, every time I looked at you I saw the light of my life (Sishangai kwa sababu macho yako yalikuwa yakizungumza lugha ya upendo tangu ulipokuja kuzungumza nami, kila nilipokutazama niliuona mwanga wa maisha yangu…),” alisema Muddy.
“ I just found myself attracted to you and loving you, it was the most sudden love that ever happened to me..(Nilijikuta tu nikivutiwa na wewe na kukupenda, lilikuwa penzi la ghafla sana kuwahi kunitokea…)”
“ I believe there is something God has planned between us… because you have been like an angel sent to save me in a difficult situation.” (Naamini kuna kitu Mungu amepanga kati yetu… maana umekuwa kama malaika uliyetumwa kuja kuniokoa katika hali ngumu).
Hata hivyo, Linnie alimwambia Muddy alipata wakati mgumu baada ya kuwekewa pingamizi kutoka kwa mabosi zake baada ya kugundua nia yake ya kutaka kumbakisha Muddy Sweden.
“However, it was not an easy task to achieve my plan.” (Hata hivyo haikuwa kazi rahisi kufanikisha mpango wangu…) alisema Linnie huku akiendelea kumtazama Muddy kwa macho yaliyokuwa yamejaa upendo.
“ That’s why I will never stop thanking you for your decision, I believe you will not regret what you did to me.” (Ndio maana sitaacha kukushukuru kwa uamuzi wako, naamini hutajutia ulichokifanya juu yangu…), Muddy alikula kiapo cha uaminifu mbele ya Linnie.
Mara baada ya kukubaliana kuingia katika uhusiano, wawili hao wakwa wazi kwa kila mtu.
Wengi waliwaona Muddy na Linnie wakiwa pamoja wakitembea huku wakiwa wameshikana mikono au wakati mwingine wakiwa wamekumbatiana.
Pea yao ilipendeza na kuzua gumzo katika Kitongoji cha Sigtuna. Wapenzi hao walikuwa wakizungumziwa takribani na kila mtu kiasi cha kuwafanya kupata umaarufu mkubwa katika mji huo mdogo.
Kila mtu aliwafahamu na kupendezwa na uhusiano wao.
Hata hivyo, kama ilivyokua desturi walikuwepo watu waliowapenda na wengine waliwaonea wivu na hivyo kusababaisha kuwachukia kutokana na sababu zao binafsi.
Baadhi ya wanawake waliitamani nafasi ya Linnie kwa sababu tu alikuwa na mwanaume wa tofauti. Baadhi ya wanaume nao walimchukia Muddy kutokana na rangi yake na kuweza kummiliki msichana mrembo kama Linnie. Hawa walikuwa ni wale waliojawa na hisia za ubaguzi.
Mbali na katika Kitongoji cha Sigtuna pia, wapenzi hao walijulikana katika kumbi, hoteli na sehemu mbalimbali za starehe zilizokuwa zikipatikana katika Jiji la Stockholm.
Mara nyingine wakati wa siku za mwishoni mwa wiki, wawili hao walionekana katika eneo lenye mandhari nzuri la Mosebacke Terrace wakicheza muziki uliokuwa ukipigwa na bendi hususan kipindi cha kiangazi.
Pia, walikuwa wakipendelea kwenda katika Klabu ya Debaser Strand wakifurahia matamasha na mazingira ya kisasa na kufurahia muziki wa aina ya Rock.
Wakati mwingine pia walipokuwa Stockholm walipendelea sana kula chakula cha jioni katika Mgahawa wa Himlen sehemu inayowavutia wapenzi wengi kutokana na madhari yake ya kuvutia.
Siku moja moja Linnie alimpeleka mpenzi wake katika Kitongoji cha Vasastan kula vyakula vya Kiskandinavia katika Mgahawa wa Tranan.
Kipindi cha likizo, Linnie alimpeleka Muddy katika nchi za zinazopakana na Sweden kwa upande wa Kaskazini na Magharibi, yaani Norway na Finland kwa upande wa Kaskazini Mashariki ambako walikuwa wakila bata la kutosha na kufanya shopingi za nguvu.
Katika mitoko yote waliyokuwa wakifanya, kuna kitu kilimshangaza sana Linnie, pamoja na starehe zote lakini Muddy hakuwa mnywaji wa pombe.
Hata pale mwanamke huyo alipojaribu kumshawishi alikutana na kipingamizi, Muddy hakuwa akinywa na mara zote alikuwa akitumia vinywaji laini visivyokuwa na kilevi cha aina yoyote.
Uhusiano wao ulizidi kuimarika na watu wengi walizidi kuwaonea wivu. Tangu Muddy akutane na Linnie maisha yake yalibadilika kwa kiasi kikubwa na kuwa mtu wa kutazamika mbele ya watu.
Maisha yalimkubali ngozi yake ilinawiri na kuwa na afya na mwonekano wa kupendeza sana mbele za macho ya watu.
Sio kiafya tu hata katika maisha kwa ujumla alikuwa ni tofauti na Muddy yule aliyekuwa akiishi mitaa ya Gerezani, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Wanawake wengine waliokuwa wakimuona akitoka na Linnie wakaaanza kummezea mate, waliitamani nafasi ya mwanamke mwenzao.
Wanawake hao wakaanza kumfanyia visa na kumpa ahadi za maisha mazuri zaidi ya yale aliyokuwa akipata kwa Linnie.
***
BAADA ya kesi ya Muddy kuisha na mzee Mangushi kuwa huru, ingawaje ilitumika nguvu kubwa kuweza kuimaliza kutokana na maaskari wengi kutaka kuifufua mara kwa mara na kumtishia mzee Mangushi kwa nia ya kutaka kumtoa pesa, wazazi wa Muddy wakaanza kuumizwa na kitendo cha kutokujua alipokuwa mtoto wao.
Damu nzito kuliko maji, familia ikaanza kuteseka na kutamani kujua kama Muddy alikuwa hai au alikuwa amefariki dunia.
Walijaribu kufanya uchunguzi kwa marafiki zake wa mtaani kujua kama alikuwa akiwasiliana nao lakini hawakuweza kuzipata taarifa zake.
Miezi ilendelea kukatika na hakuna aliyekuwa na taarifa za Muddy, mtu pekee aliyekuwa na taarifa hizo ambaye angeweza kuwahakikishia kwamba Muddy alikuwa hai ni Hamisi ambaye naye aliamua kulowea Nairobi.
Tangu Hamisi alipoingia katika nchi hiyo hakutaka kurudi Tanzania alikuwa ameanza maisha mapya kwa kushirikiana na Fashanu na jamaa zake.
Watu waliowafahamu Muddy na Hamisi waliamini kwamba walikuwa pamoja, lakini kilichokuwa kinawapa wasiwasi ni kwamba Hamisi alionekana siku chache baada ya Muddy kutoweka.
Akili za kuamini kwamba Muddy alikuwa ametoroka nje ya nchi ni kama ilikuwa ikiwaingia na kutoka.
Katika kutaka kujiridhisha kama Muddy bado yuko hai, familia ikawatuma ndugu zake wawili, Meja na Kizanda kwenda Kimanzichana, mkoani Pwani kwa mganga wa kienyeji mzee Matobo ambaye aliaminika kwamba alikuwa na ujuzi mkubwa wa kuweza kutambua mambo mengi.
Mara baada ya Meja na Kizanda kufika mzee Matobo aliwambia asingeweza kufanya chochote bila ya kupata nguo ya mhusika na kondoo mmoja.
Ilibidi ndugu hao warudi tena Dar es Salaam kuchukua nguo ya Muddy na pesa ya kondoo kisha kumpelekea mtaalamu huyo wa tiba asilia.
Waliporudi kwa mara ya pili, mzee Matobo aliwataka kujiandaa kwa safari ya kwenda kwenye mzimu wake. Ilikuwa ni mbali na pale walipofikia na aliwataka safari hiyo ifanyike usiku wa manane.
Iliwabidi Meja na Kizanda kukbaliana na masharti ya mganga kwa sababu walitakiwa kwenda huko wakiwa wamevaa kaniki tu huku wakiwa matumbo wazi.
Ilikuwa ni safari ya kutisha na kuogofya sana kwa kupandisha mabonde na milima hadi kufika katika mizimu ya mzee Matobo.
Mara baada ya kufika mzee Matobo kwa kusaidiana na kina Meja na Kizanda alimchinja kondooo chini ya mti mkubwa uliokuwa ukiamimika kwamba ndipo ilipokuwa mizimu yake kisha aliichukua nguo ya Muddy na kuiweka chini ya mti huo na kuanza kuzungumza na mizimu yake kwa lugha asiyoeleweka na wengi.
Kabla ya kuanza kuzungumza na mizimu yake, mzee Matobo alimwaga dawa na damu ya mbuzi chini ya mti ule huku kile kisu kilichochinjiwa kondoo kikiwa juu ya vitu hivyo, kisha kwa dakika kama kumi hivi upepo mkali ulivuma kiasi cha kuwatisha wateja wake.
Mara upepo alipotulia ndipo mzee Matobo alipoanza kuzungumza na mizimu yake katika lugha ambayo hakuna kati ya Meja na Kizanda aliyekuwa akiijua.
Kulikuwa na sauti iliokuwa ikitoka kwenye mti ule mkubwa, lakini ilikuwa kama inaunguruma hivi na kutoa mitetemo ni mzee Matobo pekee ndiye aliyekuwa akiilewa kilichokuwa kikizungumzwa na aliendelea kujibu kwa lugha hiyo isiyoeleweka.
Baada ya kumaliza kazi yake aliwaageukia wateja wake na kuwaambia kwamba ndugu yao bado alikuwa hai na alikuwa katika maisha mazuri.
“Yuko mbali sana na maisha yake ni mazuri…” alisema mzee Matobo kuwaambia Meja na Kizanda ambao nao hawakuwa na maswali zaidi kutokana na furaha ya kuamini kwamba ndugu yao alikuwa hai.
Hata waliporudi nyumbani na kutoa taarifa hiyo, waliulizwa maswali mengi ambayo hawakuwa na majibu nayo.
Baba yao mzee Manyara alikuwa mkali na kuwaambia makosa ambayo waliyafanya kwa kushindwa kumuuliza mzee Matobo maswali.
“Ilitakiwa mumuulize yuko mbali ya wapi? Tanzania hii hii au nje ya nchi…
“Pia, mlitakuwa kuuliza kama atarudi salama au ndio hatarudi tena?” mzee Manyara aliendelea kuwaambia wanawe kwamba walitakiwa kumwambia mzee Matobo amfanye Muddy arudi nyumbani.
***
USIFANYE mchezo na damu ya mswahili, baada ya miezi mitano ya kuwa na uhusiano kati yake na Muddy, Linnie alipatwa na mabadiliko makubwa ya mwili.
Hali yake ilibadilika na kuonekana kunawili na kuwa mrembo zaidi ya alivyokuwa awali.
Hatimaye akakosa kuziona ada zake za mwezi na ilikuja kubaini kwamba alikuwa ni mja mzito.
Ilikuwa furaha kwa Linnie kwa sababu ulikuwa ni uja uzito wake wa kwanza katika maisha yake. Alipokuwa na uhusiano na mwanaume wake wa kwanza wa Kizungu aliyekuwa akiishi naye awali hawakufanikiwa kufikia katika hatua hiyo.
Kutokana na hali hiyo, alizidi kumpenda Muddy kwa kuamini alikuwa mwanaume rijali na sahihi kwake, kitendo cha kupata mtoto kilikuwa katika akili yake na alikuwa akihisi kama alikuwa amechelewa kukifia.
Mbali na mapenzi Linnie aliongeza uaminifu kwa Muddy, akamfanyia kila jambo zuri alilokuwa akilitaka, ulikuwa humwambii kitu kuhusu mwanaume huyo.
Pia,kwa upande wa pili ilikuwa furaha kubwa sana kwa Muddy, kupata mtoto na mwanamke wa Kizungu kilikuwa ni kitendo cha ushujaa wa hali juu kwake.
Kitendo ambacho hakijawahi kufanywa na mtu yeyoye katika ukoo wao kwa mwanamke wa Kizungu. Mababu na mababu walikuwa wamepita hakuna kati yao aliyewahi kuchanganya rangi na mzungu.
Pia, alifurahi kwa sababu sehemu ya ndoyo yake ilikuwa inaenda kutimia, alikumbuka maneno waliyokuwa wakihadithiana katika kijiwe chao pale Gerezani na kina Ally Baga na Hamisi Sungajao kuhusu wanawake wa Kizungu.
Aidha alikumbuka ndoto yake ya kurudi Tanzania akiwa na mwanamke wa Kizungu sambamba na mtoto wao na kuwafunga midomo watu wote waliokuwa wakimbeza na kumdharau.
Hapo aliwakumbuka wanawake wote waliokuwa wamemkataa, ni wale aliokuwa akiishi nao jirani pale Kariakoo, pia akawakumbuka wanawake aliokuwa akisoma nao ambao walikuwa wakimkataa kwa kuwa hakuwa na kitu.
“Nitawafunga midomo…” aliwaza huku akijisifu kwa hatua aliyokuwa ameifikia hadi wakati huo.
Hiyo ilikuwa ni moja tu ya sehemu ya ndoto zake, bado kulikuwa na kitu kimoja tu kilichokuwa hajakikamilisha, ndoto zake. Ndoto ya kumiliki gari ya kifahari…fikra zake zilikuwa ni kumiliki gari aina ya BMW…
“Nikiwa na mke wangu na mwanangu ndani ya BMW… tunavinjari mitaa ya Kariakoo….hata wazee watanipa shikamooo…” aliwaza Muddy huku akipiga mahesabu ya kufanya kazi kwa bidii ili siku akirudi nyumbani aweze kununua nyumba maeneo ya Kariakoo au Ilala kama sio Magomeni Mapipa.
“Ndio, mtoto wa mjini hawezi kuishi mbali na maeneo hayo,” aliwaza na kuamini kama atapambana ataweza kununua gari ya ndoto zake.
Mtoto wa Mjini – 14