Bwana Yesu asifiwe, ni siku nyingine ya Baraka Mungu ametupa mimi na wewe ili tuweze kumwabudu yeye.
Katika somo lilipita nilifundisha “Kwanini kizazi cha sasa kimepoteza Hofu ya Mungu”. Miongoni mwa sababu za msingi nilizofundisha zilikuwa ni Kukosekana kwa Misingi Bora ya Kiroho katika Familia zetu.Leo hii nitafundisha Namana ya Kurejeza hofu ya Mungu katika Familia. Sababu za kufundisha somo hili ni kutokana na Umuhimu wa Hofu ya Mungu kuwa chanzo cha Amani na Utulivu katika familia,Jamii na Taifa kwa ujumla. Pia ni kutafuta suluhu kwa mambo ya kuumiza mioyo tunayoyashuhudia katika familia zetu nyingi yanayo sababishwa na kupotea kwa hofu ya Mungu ndani ya familia zetu.
(……Lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana. Yoshua 24:15)
Nini maana ya hofu ya Mungu?
Katika somo lililopita nilisema kwamba hofu ya Mungu ni utambuzi kwamba Mungu yupo, ni Mtakatifu, ana nguvu, anaona, anasikia, ana haki ya kuhukumu dhambi na tutawajibika mbele yake. Kwa hiyo Mtu mwenye hofu ya Mungu anampenda Mungu na kumuheshimu. Anahofu ya kumtenda Mungu dhambi (Kuiba, kuua, kudhulumu na kufanya matendo yoyote yasiyo faa katika jamii. Biblia inasema, “…Mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, Mtu aliye mnyonge (mwenye hofu ya Mungu), mwenye Roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu. Mtu asiye na hofu ya Mungu haoni shida kuiba, kuua, kudhulumu na kufanya matendo yote yasiyo kubalika katika jamii.
Ni kundi la watu waliounganishwa kwa damu, ndoa au uhusiano wa kiroho na wanaishi pamoja na kushirikiana kwa upendo na kuwajibika. Familia ni shule ya kwanza au msingi wa maisha ambapo mtu anawweza kujifunza kupenda, kusamehe, kuheshimu watu na kumcha Mungu. Ukiono jambo lolote zuri kutoka kwa mtu, mara nyingi chanzo chake huwa ni familia aliyotokea, vilevile ukiona jambo lolote lisilo zuri huwa mara nyingi chanzo chake ni familia aliyotokea japo wakati mwingine tabia inaweza kuathiriwa na mazingira.
Namna ya kurejeza hofu ya Mungu ndani ya familia
Kumcha Bwana. Biblia inasema kumcha Bwana ni kuchukia uovu, kiburi, majivuno,njia mbovu na kinywa cha ukaidi…. (Mithali 8:13). Ili familia yoyote iwenze kuwa na hofu ya Mungu ni lazima kila mwanafamilia achukie uovu, aache kiburi, majivuno, njia mbovu na maneno ya ukaidi (kukosa utii kwa Mungu). Kwa hiyo ni muhimu viongozi wa familia kufundisha na kusisitiza wanafamilia juu ya kumcha Mungu ili kurejeza hofu ndani ya familia.
Kuheshimiana na Kujaliana. (…. Msitende Neno lolote kwa kushindana,wala kwa majivuno, bali kwa unyenyekevu, kila mtu amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake…..Wafilipi 2:3). Miongoni mwa vitu vinavyoweza kusababisha familia kupoteza hofu ya Mungu ni pamoja na kudharauliana kwa hiyo ni muhimu kuwaheshimu wanafamilia wenzetu. Mfano baba amheshimu mama na wote anaowalea na mama amheshimu baba na wote anaowalea. Kwa kufanya hivyo hofu ya Mungu itajengeka ndani ya familia.
Kuwajibika (…Lakini mtu yeyote asiyewatunza walio wake, yaani wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana imani tena ni mbaya kuliko mtu asiye amini….1Timotheo 5:8). Si watu wengi tunatambua kuwa kutokuwajibika kutunza familia ni dhambi. Katika kizazi cha sasa si ajabu kuona kiongozi wa familia ametelekeza familia yake au kutokutunza familia yake. Ni wajibu wa kila mwanafamilia kuwajibika kuihudumia familia kulingana na nafasi aliyo nayo ndani ya familia. Kwa kufanya hivyo ni rahisi Mungu kupata nafasi ndani ya familia hiyo
Kusameheana. (…Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe atawasamehe nini, Bali msipo wasamehe yao, Wala baba yenu hatawasamehe ninyi makossa yenu….Mathayo 6:14-15). Msamaha ni mlango mkubwa wa kumruhusu Mungu kurejea ndani ya familia iliyokuwa imetengana au kuwa na mafarakano. Katika kizazi cha sasa watu wengi tumekuwa tukibeba uchungu kwa muda mrefu bila kusamehe kiasi cha kusababisha kuongezeka kwa migogoro na mafarakano ndani ya familia. Endapo tutaruhusu mioyo yetu kusamehe tutafungua mlango kwa Mungu kuwapamoja nasi.
Kufanya ibada pamoja/maombi na Neno la Mungu(…Wala tusiache kukusanyika pamoja kama ilivyo desturi ya wengine,bali tuonyane, na kuzidikufanya hivyokwa kadri mwonavyo sikunile kuwa inakaribia…Waebrania 10:25).
Hofu ya Mungu inaambukizwa hivyo kadiri wanafamilia wanazidi kufanya ibada pamoja kila mmoja anapata nafasi ya kusikia kile Neno la Mungu linasema. Kazi ya ibada ya pamoja ni kuonyana, kufundishana na kutiana moyo.
Faida ya kurejeza hofu ya Mungu ndani ya familia
Miongoni mwa faida za kuwa na hofu ya Mungu ndani ya familia ni pamoja na kuwa na familia yenye upendo na amani, malezi bora kwa watoto, kupata baraka na ulinzi wa mungu,kuheshimiana, kuwa chachu ya hofu ya Mungu kwa jamii na vizazi vijavyo.
Madhara ya familia kukosa hofu ya Mungu
Familia inapokosa hofu ya Mungu husababisha kuvunjika kwa mahusiano ndani ya familia, kuporomoka kwa maadili katika familia, jamii na Taifa kwa ujumla, kukosa baraka za Mungu na Ulinzi wa Mungu, pia huwa ni msingi mbovu kwa vizazi vijavyo.
Ubora wa jamii na Taifa hutengenezwa na familia zenye hofu ya Mungu, hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kuwajibika kutengeneza familia iliyo na hofu ya Mungu.
