OMO ahitimisha kampeni Zanzibar, akifanya mikutano 75

Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo visiwani Zanzibar, Othman Masoud Othman, amehitimisha kampeni zake, akijivunia kufanya mikutano 75 tangu alipoanza.

Ameitumia hotuba yake ya kuhitimisha kampeni hizo kwa kutoa shukrani na pongezi kwa makundi mbalimbali, likiwamo Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania, kwa kuendelea kuimarisha ulinzi katika mchakato wote wa kampeni visiwani humo.

Othman amehitimisha kampeni hizo leo Jumapili, Oktoba 26, 2025, katika Uwanja wa Kibandamaiti, Unguja, mkutano uliohudhuriwa na wananchi, wafuasi, na wanachama wa chama hicho.

Amesema amefanya mikutano 75 hadi anafunga kampeni zake na kwamba bado yuko imara na sauti yake inasikika bila kukwamakwama.

Ameigawa hotuba yake ya kufunga kampeni hizo katika sehemu mbili, ya kwanza kutoa shukurani kwa waliofanikisha kufanyika kwa kampeni hizo, ikiwamo timu yake ya ushindi.

Jambo la pili, ametoa kutoa pongezi kwa makundi mbalimbali, vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama, kwa ushirikiano vilivyouonyesha kulinda mikutano yao ya kampeni.

“Tupo kwenye uchaguzi, na uchaguzi hasa wetu una mambo yake. Wapo wengine ambao wangetaka uharibike, tuwashukuru sana. Wenzetu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, sasa hivi ukipita utaona baadhi ya maeneo wanalinda; haya ni mahitaji ya wakati,” amesema.

Amesema anaamini watakwenda kushinda katika uchaguzi huo kwa kuwa wameingia ikiwa tayari walishajiandaa na wana ushindi mkononi mwao.

Ametumia jukwaa hilo kurejea sehemu ya ahadi zake alizozitoa katika mikutano yake ya kampeni, akisema anafanya hivyo kupigia msumari uelewa wa kile alichokiahidi.

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa, amewaomba wananchi na wafuasi wa chama hicho kufanya ibada ya kufunga ili kumwomba Mungu awape ushindi usio na wasiwasi.

Sababu nyingine ya kufunga, amesema ni kuwajaalia ushindi wa haki ndani ya amani na nchi ikiwa imetulia bila matatizo.

“Sisi si watu wa bonge la party ‘sherehe’, sisi ni watu wa Mungu. Sisi kila hatua ni Mwenyezi Mungu,” amesema Jussa.

Amewatoa wasiwasi wanachama na wafuasi wa chama hicho kwamba watakwenda kupiga kura, kuhesabu, kufanya majumuisho, na washindi watatangazwa kwa amani.

Amewasihi watumishi wa umma kuhakikisha wanapiga kura kwa uhuru, na asitokee atakayewatisha au kuwalazimisha kumchagua mgombea fulani kwa sababu fulani.