Raha, karaha wenza kupishana sana umri

Mwanza. Simulizi ya Neema Daudi, mwanamke wa miaka 20 aliyeolewa na mzee wa miaka 50, imekuwa gumzo linalozua maswali mengi kuhusu uhalali, uhalisia na uhalali wa ndoa kati ya watu wanaopishana sana umri. 

Ingawa ndoa ni muungano wa ridhaa, kuna nyakati ambapo ridhaa hiyo huzaa mateso makubwa kwa mmoja wa wenza, hasa pale tofauti ya umri inapozidi kuwa mwanya badala ya daraja la kuelewana.

Neema aliolewa akiwa na miaka 19, muda mfupi baada ya kumaliza kidato cha nne. Alivutwa na ahadi za maisha mazuri, gari la kifahari, na nyumba yenye dari ya kisasa. 

Mumewe, Bwana Saulo, mwenye miaka 50 wakati huo, alikuwa mfanyabiashara mashuhuri wa mbao na vifaa vya ujenzi.

“Mwanzo nilidhani ni bahati, niliona wenzangu wakiishi maisha ya tabu na vijana wa umri wao, nikaona bora niwe na mtu mzima mwenye mali,” anasema Neema huku machozi yakimtoka.

Lakini baada ya mwaka mmoja wa ndoa, Neema alianza kuhisi pengo kubwa. Mumewe alikuwa mtu wa mila, mwenye misimamo mikali.

 Alitaka Neema aishi kama wake wa kale asivae suruali, asitumie simu saa nyingi, na zaidi ya yote, amwite “baba”.

“Huwa najisikia vibaya kila ninapomwita baba. Mwili wake, maneno yake, tabia yake vyote vinanikumbusha baba yangu mzazi,” anasema Neema kwa sauti ya huzuni.

Kwa Neema, raha iligeuka karaha. Maongezi kati yao yakawa kama hotuba darasani; kila alichosema Neema kilionekana kinyume na mila za Saulo. Alipompendekezea waende likizo  kama wanandoa wengine, Saulo alijibu kwa dhihaka: “Huko kuna vijana wanaovaa vibaya, unataka tukutane nao ili uanze tabia za kisasa?”

Kilichomuumiza zaidi Neema ni upweke wa kihisia. Saulo hakuelewa lugha ya mapenzi ya kizazi kipya. Hakujali ujumbe mfupi wa kimahaba, hakutaka picha za pamoja, wala kushiriki kucheza naye. Kwa maneno rahisi, Neema alihisi kama anaishi na mzazi, si mwenza.

Mkazi wa Butimba jijini Mwanza, Ayoub Swed anasema: “Mara nyingi wanaume tunaoa mwanamke tunayemzidi umri sana. Hii ni kwa sababu tunaamini mwanaume ni kichwa cha familia, huwezi kuoa mwanamke aliyekuzidi itakuwa shida japo vijana wa sikuhizi wanaoa wanawake wakubwa wamewazidi umri hata miaka 10.’’

Anaongeza: ‘’Kuwa na mwenza unayemzidi umri kuna faida, kwanza anakusikikiliza, anafanya unachotaka lakini kikubwa anakuwa mfariji wako, yaani anakuliwaza.

Hata hivyo, anasema kuna hasara yake kwani mtu mzima akioa binti mdogo lazima wasumbuane.

‘’.Unajua ukioa binti wa miaka 25 halafu wewe ukawa na miaka 50 lazima tu usumbuliwe na wivu. Utambana bana mtoto wa watu ooh huyo ni nani oh ulikuwa wapi mwishowe migogoro ya ndoa au kupata presha kwa hofu ya kuibiwa,’’ anaeleza.

Si kila ndoa yenye tofauti kubwa ya umri huishia kwa maumivu. Kuna ndoa nyingi ambazo zinafanikiwa licha ya pengo la miaka. Zifuatazo ni baadhi ya faida zinazoweza kupatikana:

Mosi, ukomavu wa kiakili: Mtu mzima anaweza kuwa na uwezo mzuri wa kuhimili migogoro, kufanya uamuzi wa busara, na kuelekeza mwenza wake katika maisha.

Pili, usalama wa kifedha: Mara nyingi watu wakubwa tayari wamejijengea maisha, hivyo mwenza mdogo hujikuta akifurahia utulivu wa kiuchumi.

Tatu, uaminifu na malengo ya maisha: Mtu mzima huweza kuwa tayari kuishi maisha ya utulivu na familia, tofauti na vijana ambao bado wanajaribu kuelewa dunia.

Hata hivyo, changamoto ni nyingi na zenye uzito. Mfano pengo la kizazi huleta tofauti kubwa za fikra, mitazamo na mtindo wa maisha. Kinachovutia kijana wa leo huenda ni kero kwa mtu wa miaka 50.

Mwenza mwenye umri  mdogo bado anajifunza kuhusu mapenzi na maisha, ilhali mwenza mkubwa tayari anaamini anajua kila kitu,  hali inayoweza kuzima mawasiliano na mapenzi.

Wakati mwingine, ndoa hizi huishia kwa huzuni pale mmoja anapofariki mapema, au kuzeeka kabla ya mwingine kuwa tayari kwa mabadiliko hayo ya kimwili na kiafya.

Aidha, kuna wakati mapenzi hukosa mizizi na mwenza mmoja kuwa tegemezi wa kifedha, hali ambayo huibua migogoro.

Kwa Veronica Jacob anasema changamoto ya kuolewa na mtu aliyekuzidi sana umri, ni kwamba  mwanaume atataka umchukulie kama mzazi wake.

‘’…wanataka uwatendee kama baba, mume na mkubwa wako. Kuna baadhi ya makosa mtu unaweza kufanya kwa bahati mbaya lakini utasikia anasema ebu niheshimu kama mtu niliyekuzidi umri, kama mkubwa wako na kama mume wako. Maneno hayo yanapunguza mapenzi kwa sababu inafikia wakati unajuta kuolewa na mtu aliyekuzidi umri mkubwa,’’ anaeleza.

Wataalamu wa saikolojia na uhusiano wanashauri kwamba tofauti ya miaka mitano hadi 10 inaweza kuvumilika kirahisi katika ndoa, kwa kuwa wenza bado wanaweza kuwa na mitazamo inayoelewana. 

Hata hivyo, kila uhusiano ni wa kipekee, na jambo la msingi ni mawasiliano, heshima, na malengo yanayofanana.

Tofauti ikizidi miaka 20 au zaidi, kama ilivyo kwa Neema na Saulo, mara nyingi huwa na changamoto nyingi hasa pale mwanandoa mmoja akiwa bado kijana anayetaka kushirikiana mambo ya kisasa, na mwingine akiwa tayari kuishi maisha ya utulivu, pengine hata ya uzee.

Mtaalamu wa saikolojia, Jesusa Malewo, anasema: ‘’Mtu anahitaji kumzidi mwenza wake umri angalau miaka mitatu hadi mitano inategemea japo hatuna umri mahususi. Ila angalau mpishane miaka mitano kwa sababu ya namna ya kuangalia mambo. Kwa mfano mimi nina miaka 30 nikamchukua mtu mwenye 20 nitakuwa mbali sana..yaani mimi ninavyovifikiria ni vikubwa kuliko anavyovifikiria yeye na unyanyasaji ndipo unaanza hapo kwa sababu mimi nina uelewa, nina uzoefu..unaweza kukuta yeye yupo nje ya vitu ambavyo ninavyo. Kwahiyo inakuwa shida angalau tunasema mitano kwa sababu tunakuwa tunakaribiana.’’

Ni kweli kwamba penzi halichagui, lakini umri una nafasi kubwa katika kuathiri ufanisi wa mahusiano. 

Kisa cha Neema ni funzo kwa jamii, wazazi, na vijana wanaotamani maisha ya haraka bila kufikiria athari za muda mrefu.

Leo hii Neema anatamani angechukua muda kujitambua, kujifunza maisha, na kuoa au kuolewa na mtu mwenye ndoto sawa, lugha ya mapenzi inayofanana, na msisimko wa kijana anayeishi wakati wake.

Kwa wale wanaowaza kuingia kwenye ndoa zenye tofauti kubwa ya umri, ni vyema kujiuliza: Je, tunaishi kizazi kimoja, au mimi na mwenza wangu ni mgeni wa mwingine?

Ndoa ya Emmanuel Macron na Brigitte Macron

Ndoa hii ni mfano wa wenza maarufu duniani waliooana wakipishana kwa umri mrefu. Tofauti yao ni miaka 24.  MacronambayeniRaiswaUfaransa alizaliwa mwaka 1977, huku mkewe BrigitteMacron akizaliwa mwaka 1953.

Uhusiano wa Macron na Brigitte ni mojawapo ya uhusiano maarufu zaidi duniani wenye tofauti kubwa ya umri na pia ni wa kipekee kwa jinsi ulivyoanza.

Brigitte alikuwa mwalimu wa Macron katika shule ya sekondari wakati Macron akiwa na umri wa miaka 15. Walianza kuwasiliana kwa karibu zaidi wakati huo, jambo lililozua maswali mengi kutoka kwa jamii na familia zao.

Wawili hao walifunga ndoa mwaka 2007, baada ya kuwa pamoja kwa muda mrefu licha ya vizingiti vya kijamii. Wakati huo, Brigitte tayari alikuwa na watoto watatu kutoka ndoa ya awali.

Licha ya tofauti ya umri, uhusiano wao umesimama imara na Brigitte amekuwa mshirika muhimu katika safari ya kisiasa ya Macron.

Alipokuwa rais wa Ufaransa mwaka 2017 (akiwa na miaka 39), Brigitte alikuwa na miaka 64 jambo lililozua mijadala mikubwa kimataifa kuhusu uhusiano wenye tofauti kubwa ya umri, lakini pia kuwafanya kuwa mfano wa kuvunja vikwazo vya kijamii na mitazamo ya kimapokeo kuhusu ndoa.

Leo hii, Brigitte anaheshimika kama “First Lady” wa Ufaransa mwenye ushawishi mkubwa, huku akiendelea kuonekana bega kwa bega na Macron katika shughuli za kitaifa na kimataifa.

Mfano mwingine ni wa RupertMurdoch, mfanyabiashara tajiri na mwenye ushawishi mkubwa nchini Marekani hasa katika sekta ya vyombo vya habari. Ameoa mara kadhaa, na ndoa zake nyingi zimekuwa gumzo la kimataifa, hasa kwa sababu ya tofauti kubwa za umri kati yake na wake zake, pamoja na umaarufu wake.

Kwa mfano aliwahi kumuoa mwanamitindo, Jerry Hall waliotofautiana kwa miaka 26. Walioana mwaka 2016 na kuachana 2022.