Dar es Salaam. Wanachama wa Rotary Club ya Mikocheni jijini Dar es Salaam, wakishirikiana na wenzao wa Rotaract, wameadhimisha Siku ya Polio Duniani 2025 kwa kufanya matembezi ya uhamasishaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Matembezi hayo yamelenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa chanjo na kuunga mkono jitihada zinazoendelea za kutokomeza ugonjwa wa polio duniani.
Shughuli hiyo ilianza kwa kikao cha pamoja cha maelewano na ushirika, kisha kufuatiwa na matembezi yaliyofanyika katika eneo la hospitali, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kuendelea na chanjo licha ya Tanzania kutokuwa na kisa cha polio tangu mwaka 2015.
Baada ya matembezi hayo, wanachama wa Rotary na Rotaract waligawa vifurushi vya mahitaji mbalimbali kwa akinamama waliolazwa wodi ya wazazi na kutoa elimu fupi kuhusu umuhimu wa chanjo za mara kwa mara kwa watoto wachanga.
Washiriki pia waliungana na wahudumu wa afya katika zoezi la utoaji chanjo ambapo watoto wachanga walipatiwa chanjo ya polio ya matone.
Shughuli hiyo ilihitimishwa kwa hafla fupi ya kutambua na kuwapongeza wajitolea na washirika walioshiriki katika kampeni ya uhamasishaji ya wiki kumi iliyoitwa “Mama, Mkinge Mtoto Wako!”, iliyowafikia akinamama 184 kwa elimu kuhusu kinga dhidi ya polio.
Rais wa Rotary Club ya Mikocheni, Nasibu Mahinya amesema klabu hiyo itaendelea kuunga mkono miradi ya afya ya jamii inayolenga kudumisha hali ya kutokuwa na polio nchini.
“Mapambano dhidi ya polio bado yanaendelea, na huu ni wakati wa kuongeza kasi katika kuhakikisha tunatokomeza kabisa ugonjwa huu,” amesema Mahinya.
Ameongeza kuwa ni muhimu kupambana na upotoshaji unaohusiana na chanjo.
“Tunataka akinamama waelewe kuwa chanjo ya polio ni salama, ni bure, na ni muhimu kwa ajili ya kulinda vizazi vijavyo,” amesisitiza Mahinya.