Dar es Salaam. Ubalozi wa Norway nchini Tanzania na taasisi ya kuendeleza kilimo ya Private Agricultural Sector Support (PASS) Trust wamesaini makubaliano ya kutekeleza mradi wa kuongeza mnyororo wa thamani katika soya ili kuimarisha sekta ya kilimo kupitia ubunifu, fedha jumuishi na teknolojia rafiki kwa mazingira.
Makubaliano hayo yaliyofikiwa mwishoni mwa wiki iliyopira ni uthibitisho wa dhamira ya Norway kusaidia maendeleo endelevu na usalama wa chakula nchini.
Kupitia makubaliano hayo, Norway imetoa ruzuku ya Dola 2.4 milioni za Marekani (Sh6 bilioni), huku PASS Trust ikichangia kiasi sawa kupitia dhamana zake za mikopo, hatua inayowakilisha uwekezaji wa kimkakati katika mustakabali wa kilimo nchini.
Kupitia mradi huo, wakulima 12,500 asilimia 40 wakiwa wanawake na vijana, watanufaika kwa kupata mbegu bora, zana za kisasa, masoko ya uhakika na huduma za kifedha.
Ifikapo mwaka 2028, mradi huo unatarajiwa kuongeza mara tatu uzalishaji wa soya, kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno na kupanua uwezo wa usindikaji wa ndani, hivyo kuleta manufaa halisi ya kiuchumi na kijamii kwa jamii za vijijini.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Kjetil Schie, Mkuu wa Ushirikiano Ubalozi wa Norway, amesisitiza umuhimu wa makubaliano hayo.
“Ushirikiano huu kati ya Norway na PASS Trust unaakisi azma yetu ya pamoja ya kufanya kilimo kuwa injini ya ukuaji jumuishi na endelevu. Kwa kuimarisha uzalishaji wa soya na kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani, tunachangia kujenga jamii imara na zenye ustahimilivu.”
Amesema mradi huo unaendana na vipaumbele vya Norway katika kusaidia kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, ujumuishaji wa kidijitali na usawa wa kijinsia.
Mkurugenzi Mkuu wa PASS Trust, Yohane Kaduma, amesema, “makubaliano haya yanawakilisha zaidi ya ufadhili wa kifedha, ni ishara ya maono ya pamoja ya kukuza kilimo jumuishi, kinachozingatia masoko na mabadiliko ya tabianchi. Kupitia ushirikiano huu, tunalenga kubadilisha sekta ya soya kuwa injini ya usalama wa chakula, ajira, na maendeleo endelevu ya vijijini.”
