Serikali yagawa hati 580 za kimila kwa wananchi wa Sikonge

Tabora. Serikali imetoa jumla ya hati 580 za hakimiliki za kimila kwa wananchi wa Kijiji cha Makibo, Kata ya Nyahua, Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, kupitia Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo (DSL-IP), unaoratibiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama wa milki za ardhi, kupunguza migogoro kati ya jamii na mamlaka za uhifadhi, pamoja na kuchochea maendeleo endelevu katika maeneo ya vijijini.

Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Thomas Myinga akizungumza na wananchi  wa Kijiji cha Makibo, Kata ya Nyahua, Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora katika hafla ya kukabidhi hati za hakimiliki za kimila.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa hati hizo leo Jumapili, Oktoba 26, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Thomas Myinga amesema hati hizo zitawawezesha wananchi kuwekeza katika shughuli endelevu kama kilimo, ufugaji na biashara za mazao ya misitu, hatua itakayosaidia kukuza uchumi wa kaya na kulinda mazingira.

“Mipango hii na hati hizi ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kupunguza upotevu wa bioanuwai na kuzuia uharibifu wa ardhi. Tunataka kuona jamii zikiwekeza katika matumizi bora ya ardhi na uhifadhi wa misitu ya miombo,” amesema Myinga.

Kwa upande wake, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Dk Zainab Bungwa amesema mradi huo wenye thamani ya Dola 6.8 milioni za Marekani (Sh16.8 bilioni) unatekelezwa kwa miaka mitano kuanzia 2023 hadi 2027 katika wilaya za Kaliua, Urambo na Sikonge (Tabora)naMlele (Katavi).

Amebainisha kuwa lengo kuu la mradi ni kurejesha uoto wa asili, kupunguza uharibifu wa ardhi na kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi karibu na misitu ya miombo.

Dk Bungwa ameongeza kuwa mradi huo unahusisha nchi 11, ikiwemo Tanzania, Kenya, Malawi, Zimbabwe na Angola, na tayari umeanza kutambua vikundi vya wazalishaji wa mazao ya misitu na mashamba (FFPOs) ili kushiriki kikamilifu katika uhifadhi na biashara endelevu.

Aidha, amesema TFS inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali inayolenga kuimarisha uhifadhi, ikiwemo ujenzi wa vituo vya ulinzi wa misitu (Ranger Posts), matumizi ya ndege zisizo na rubani (drones) kwa doria, pamoja na ujenzi wa nyumba za nyuki, maghala ya mbegu na miundombinu ya maji kwa jamii zinazoshiriki katika uhifadhi.

Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Thomas Myinga akikabidhi hati ya hakimiliki ya kimila kwa Mwananchi  wa Kijiji cha Makibo, Kata ya Nyahua, Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.Picha na Hawa Kimwaga

Naye Obed Katonge kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) amesema tume itaendelea kushirikiana na mamlaka za upangaji kuhakikisha ardhi inapangwa, inapimwa na kumilikishwa kwa wananchi ipasavyo.

Amesisitiza wananchi kulinda hati zao na kuepuka kuziuza au kuazimishana kiholela, akisema kufanya hivyo ni kuvunja sheria na kunaweza kuhatarisha usalama wa milki zao.