TARURA Mkuranga Yaendelea na Ujenzi wa Barabara ya Vikindu–Sengetini Kuunganisha Pwani na Dar es Salaam

Na Miraji Msala, Mkuranga – Pwani

Mhandisi Aidan Maliva kutoka Kampuni ya Ubaruku Construction Co. Ltd, alisema kazi hiyo inaendelea vizuri kwa kasi na kwa viwango vya juu, huku timu yake ikifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati uliopangwa.

Mradi huu unatekelezwa kwa ubora wa hali ya juu. Tulianza kazi tarehe 20 Agosti 2025 na tunatarajia kukamilisha tarehe 20 Februari 2026. Hadi sasa tumeifikia asilimia 60 ya utekelezaji,” alisema Mhandisi Maliva.

Amefafanua kuwa mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.351, na unahusisha ujenzi wa barabara na madaraja yanayounganisha kati Vikindu–Sengetini na barabara yenye urefu wa kilomita 18.66, inayounganisha Wilaya ya Mkuranga na Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuamini na kutupatia miradi hii muhimu ya maendeleo. Tunaahidi kuitekeleza kwa ubora wa juu na ndani ya muda uliopangwa,” alisema Maliva.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha usafiri wa wananchi kutoka Mkuranga kuelekea Kigamboni na Dar es Salaam, kupunguza gharama za usafiri, na kuongeza mzunguko wa biashara kati ya mkoa wa Pwani na jiji la Dar es Salaam.