UCHAMBUZI WA DANIEL MJEMA: Hii ndio hatari ya Polisi kutotekeleza amri ya mahakama

Oktoba 23,2025, Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Bukoba, kupitia maombi maalumu (Habeas Corpus), ilitoa amri kwa Jeshi la Polisi kuwaachia huru au kuwafikisha kortini, watuhumiwa wa uhalifu wanaowashikilia kinyume cha sheria.

Lakini badala ya kutekeleza amri hiyo ya mahakama, tumemsikia na kumuona Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Brasius Chatanda, akijitetea kuwa hawajapokea amri hiyo ya mahakama na kwamba sio kazi yao kuwafikisha kortini.

Kwa maneno yake, Kamanda huyo anasema kazi yao ni kukamata na kupeleleza kisha kuandaa jalada na kulipeleka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), ambao ndio wana wajibu wa kupima kama kuna viashiria vya jinai na kuandaa mashitaka…

Nimesikitishwa sana na msimamo huo wa Polisi kwa sababu waliwakilishwa kortini na wakili mwandamizi wa Serikali, Judith Mwakyusa akisaidiana na mawakili, Mgeni Mdee na Matilda Assey, hivyo walifahamu amri ya mahakama ilisema nini.

Katika maombi hayo mawili tofauti namba 25115 na 25281 ya 2025, wajibu maombi walikuwa ni Mkuu wa Kituo (OCS) Bukoba, Mkuu wa Upelelezi (RCO) Mkoa wa Kagera na Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) Kagera.

Lakini waleta maombi walimuunganisha Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) kama mjibu maombi wa nne na Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) kama mjibu maombi wanne, ambaye ndiye mwenye wajibu wa kuandaa hati ya mashitaka.

Msingi wa maombi hayo unatokana na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) huko Bukoba na raia wengine wawili, ambao wanashikiliwa mahabusu kwa zaidi ya siku nane nje ya saa 24 zinazotajwa na sheria.

Mahakama baada ya kupima hoja za pande mbili, ilitoa amri ama watuhumiwa hao waachiwe huru au wawafikishe mahakamani si zaidi ya Oktoba 24, 2025. Hawajawafikisha kama amri ya mahakama ilivyowataka.

Sasa badala ya kutekeleza amri hiyo ya mahakama, ndio ghafla Oktoba 25,2025 anajitokeza RPC Kagera na kutoa visingizio mbalimbali licha ya kuwa kuna utaratibu wa kupinga (challenge) amri za mahakama na naamini wajibu maombi wanaujua.

Kwanza niseme kuwa kitendo kinachofanywa na Polisi cha kutotekeleza amri ya mahakama ni kuudharau mhimili huo kama inavyofafanuliwa na kifungu cha 114A cha Kanuni ya Adhabu (Penal Code) kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.

Ukisoma kifungu cha 114A (b) kinasema mtu anatenda kosa endapo kwa makusudi ana kinga, au kwa kujua anazuia, au kwa kuingilia au kuzuia utekelezaji wa hati yoyote ya kuitwa shaurini, notisi au amri iliyotolewa na mahakama.

Endapo ataitwa kortini (show cause) ili kujieleza na akaonekana amekiuka amri hiyo ya mahakama au maelekezo yoyote basi mtu huyo atakuwa ametenda kosa na atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha muda usiozidi mwaka mmoja.

Kwa hiyo wajibu maombi wako katika hatari ya kufungwa jela kwa kukiuka amri ya mahakama, hivyo ni muhimu wakaongozwa vyema na mawakili wa Serikali wajue athari za kukiuka amri zile zilizotolewa na majaji.

Lakini ni lazima Polisi wetu wajue kuwa nchi hii inaongozwa kwa misingi ya utawala bora inayoheshimu utawala wa sheria, hivyo kiburi hiki cha Polisi wetu kujiona wako juu ya sheria kinapaswa kulaaniwa na wapenda haki duniani.

Utawala wa sheria ni nini? Kwa lugha ya kawaida kabisa, maana yake hakuna mtu aliye juu, au nje ya mamlaka ya sheria, kuanzia Rais wa nchi mpaka raia wa kawaida na kuanzia Dola ya nchi mpaka kaya iliyopo kwenye kijiji kidogo kabisa.

Kila chombo cha Dola, taasisi, kila mtu anawajibika kwa sheria wakiwamo Jeshi la Polisi ambao ndio msingi wa makala haya.

Dhana kwamba ni vema watu watawaliwe na sheria imeanza zamani za kale. Hammurabi, Mfalme wa Babylon, alitengeneza sheria na kuzipa uzito mkubwa, hii ilikuwa miaka 1760 kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo, zaidi ya miaka 3,785 iliyopita.

Aristotle, aliyekuwa mwanafalsafa wa Kigiriki aliyeishi zaidi ya miaka 2,000 iliyopita, naye alitamka maneno haya kuhusu umuhimu wa Dola kuongozwa na sheria:- “Utawala wa sheria ni bora kabisa kuliko utawala wa mtu binafsi”.

Tangazo la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948 kuhusu haki za binadamu linatahadharisha kwamba watu wanaweza kulazimika kuasi ili kupinga dhuluma, maonevu na ukandamizaji ambayo hutokea pale utawala wa sheria haupo.

Ni wazi kwamba utawala wa sheria unapotoweka, matokeo yake ni machafuko, fujo na maasi ya raia. Kwa hiyo Utawala wa sheria unapaswa kuanzia kwa watawala bila kuwepo kwa visingiziosingizo visivyo na mashiko.

Hayati Lord Denning (1899 1999) ambaye alikuwa Jaji maarufu wa Uingereza na mwanamapinduzi ya sheria ambaye alipanua mtazamo wa mahakama nyingi za Jumuia ya Madola alisema; “Once great power is granted, there is a danger of it being abused”.

Kwa Kiswahili alisema; “Pale ambapo madaraka makubwa yanatolewa (kwa vyombo vya Dola kama tunavyoona sasa kwa Jeshi la Polisi) basi ipo hatari kubwa kwamba yanaweza kutumiwa vibaya.

Kwa hiyo kuwabana wale walio madarakani ili wasitumie vibaya madaraka waliyopewa kisheria, kama ambavyo sasa tunaona kwa Polisi wetu ndio hatua ya kwanza ya kusimika utawala wa sheria katika nchi yetu.

Kwanza ya yote, sheria zinazotoa madaraka lazima zitafsiriwe na mahakama kwa ukali mkubwa dhidi ya wale walio madarakani ili wasidhulumu au kukandamiza raia. Pili, watawala wasikubaliwe kutenda chochote ambacho hakiko katika sheria.

Sasa kama sheria ya mwenendo wa makosa ya Jinai (CPA), inataka mshukiwa wa uhalifu aliye mikononi mwa Polisi afikishwe kortini ndani ya saa 24, nini kinawafanya Polisi wetu kuwa juu ya sheria hadi kudharau amri za mahakama.

Mwaka 1765 Lord Camden ambaye alikuwa Jaji Mkuu wa Uingereza alisema hivi kuhusu watawala kufuata sheria na hapa namnukuu “lf it is the law, it will be found in our books. lf it is not to be found there, it is not law.”

Yaani kwa Kiswahili anasema “lwapo ni sheria, basi tutaiona kwenye vitabu vyetu vya sheria. lwapo haipo humo, basi hiyo sio sheria”.

Ni muhimu Polisi wetu tukawauliza hicho wanachokifanya kipo kwenye sheria? Kama kipo basi itaangaliwa iwapo kweli sheria hiyo imezingatiwa ili kuondoa maumivu kwa wanyonge, tofauti na hivyo hata udhuru wa kujitetea haupo.

Watawala wasipoheshimu sheria na kuzizingatia katika kila hatua na katika kila uamuzi wanaochukua, basi kama Tangazo la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa linavyosema, fujo na maasi ya raia huwa ndio matokeo ya dhambi hii.

Kwa hiyo Polisi wetu wasilete visingizio kuwa hawajapata amri ya mahakama, wakati walikuwepo kortini kupitia mawakili wa Serikali niliowataja kwa sababu madhara ya kujifanya wako juu ya sheria ni makubwa kuliko kuziheshimu.

Leo hii nchini kwetu chuki dhidi ya askari wetu ni kubwa mno na ukitafuta kiini ni wao kukiuka sheria katika ukamataji na upelelezi na kuweka watu mahabusu siku zozote wanazotaka kinyume kabisa na sheria na Katiba ya nchi.

Tunasema hakuna mtu au taasisi ambayo iko juu ya sheria au nje ya sheria. Tunasema kila mmoja wetu anawajibika kwa sheria. Sasa iweje Polisi wetu wawe juu ya sheria? CPA iko wazi katika hatua zote za ukamataji hadi kufikishwa kortini.

Lord Templeman alipata kusema; “Parliament makes the law, the executive carry the law into effect and the judiciary enforce the law” akiwa na maana Bunge linatunga sheria, serikali inatekeleza sheria, na mahakama zinathibitisha sheria.

Vyombo vyote hivi vya Dola vinalazimika kufanya kazi yake ndani na chini ya sheria ili kulinda haki za wananchi ambao mara nyingi huitwa “wanyonge” na havipaswi kufanya kazi kwa masilahi ya kisiasa ya kundi fulani, bali kwa mujibu wa sheria.

Polisi wetu wajue, siku zote kunapofuka moshi chini huwa kuna moto. Turudi kwenye msitari wala hatujachelewa.