Canada. Katika lugha ya Kiingereza, kuna msemo maarufu: “Mr. Right” au “Miss Right”, ukimaanisha mwenza anayefaa kuoa au kuolewa naye.
Sisi, kama wanandoa, tumepitia hatua ya kumtafuta mchumba. Kwa neema ya Mungu, hatukupita tu, bali tulifanikiwa na sasa tunaweza kushiriki uzoefu huu kwa nia ya kusaidia wengine.
Kama kichwa cha makala kinavyoashiria, bila kujali dini, kabila, au tofauti nyingine zozote, kama unatafuta kuoa au kuolewa na “malaika” , tafadhali usipoteze muda wako.
Malaika hakuwepo, hayupo sasa, wala hatakuwepo duniani. Kila mtu ni binadamu mwenye ubora na upungufu wake. Hivyo, epuka kutafuta mkamilifu asiye na dosari. Huyo hayupo.
Vivyo hivyo, kama hakuna malaika, basi pia hakuna shetani. Hakuna aliyekamilika kwa uovu. Kila mmoja ana sifa nzuri na upungufu.
Siri ni kujifunza kuishi kwa furaha na binadamu huyo halisi, si katika ndoto ya mkamilifu au mkosaji wa kudumu. Makala haya inajadili misingi ya kibinadamu ya kumtafuta mwenza anayefaa kwa mizani ya uhalisia.
Kabla hujaanza kumtafuta mchumba, ni muhimu kwanza ujitafakari na kujielewa. Jua wewe ni nani, unathamini nini, na unahitaji mwenza wa aina gani. Ikiwa una tabia fulani nzuri au mbaya, fahamu kuwa huenda ukavutia mtu mwenye tabia zinazofanana.
Ingawa wakati mwingine watu tofauti huvutiana, tofauti hizo zinaweza kuleta changamoto kubwa wanapoishi pamoja, hasa kama hawapo tayari kuelewana au kubadilika.
Kumtafuta mchumba si jambo la kubahatisha. Ni mchakato unaohitaji umakini, bidii na ubunifu. Mchunguze unayempenda; msikilize, mwelewe, muulize maswali ya msingi, na hata mfuatilie kwa makini pasipo kumdhalilisha.
Ni muhimu kufanya uamuzi sahihi kabla ya kuingia kwenye uhusiano wa kudumu. Ukishaingia, ni vigumu kutoka bila madhara. Washirikishe wazazi na watu wazima wenye busara katika safari hii.
Wakati mwingine utakutana na mtu ambaye si kamili kwa vigezo vyako. Hii si shida kama kuna nia ya kujirekebisha. Kuna tofauti zinazorekebishika kama vile tabia, mitazamo au uelewa.
Lakini kuna sifa kama kutokuwa mwaminifu au kutokuwa na upendo wa kweli, hizi ni ngumu kubadilika. Jiulize, je, uko tayari kuvumilia au bora uachane naye kabla ya kuvunjika moyo baadaye?
Ni muhimu kuhakikisha kuwa nyote wawili mnaelewa vizuri mnachokitamani. Wapo watu hasa vijana wanaoingia katika uhusiano bila malengo, wakiwa na tamaa au dhana potofu. Hali hii huweza kuharibu maisha ya mtu.
Wapo waliowaacha wachumba wazuri na kuishia mikononi mwa watu waliowatesa na kuwaumiza.
Hili ni kosa kubwa linalofanyika na wengi. Wapo wanaoanza kuishi pamoja kabla ya ndoa kwa hiari au kwa sababu ya ujauzito na mwisho wake huwa maumivu.
Wengine hujilazimisha kuzaa ili kulazimisha ndoa, bila kufahamu kuwa hilo linaweza kuwaletea majuto makubwa. Mara nyingi, hatua hizi huondoa mvuto wa ujana na heshima ya ndoa.
Kama Waingereza wanavyosema: “You lose your spendforce” yaani unapoteza mvuto na maana ya jambo kabla halijafika wakati wake.
Usikimbilie kuingia kwenye ndoa bila kufanya ‘homework’ yako vizuri. Fanya uchunguzi, zungumza na watu wake wa karibu, jua historia yake.
Haraka haraka haina baraka. Ukishaingia kwenye ndoa, kutoka ni vigumu na mara nyingi kuna maumivu.
Binadamu ana upungufu na ubora. Kila mtu ana kasoro, lakini pia kila mtu ana nafasi ya kujifunza, kurekebisha na kukua. Huna sababu ya kutafuta malaika kwa kuwa hawapo.
Badala yake, tafuta mtu mwenye moyo wa kujifunza, anayejitambua na mwenye utayari wa kubadilika kwa ajili ya maisha yenu ya baadaye.
Upungufu kama kiwango cha elimu, kipato, au baadhi ya mazoea madogo yanaweza kubadilika. Lakini mambo kama ukosefu wa maadili, ubinafsi au kutokuwa muwazi ni viashiria vya matatizo makubwa ya baadaye.
Katika kutafuta mchumba, epuka kuangalia ndoto zisizo halisi. Hakuna malaika wala shetani. Kuna binadamu kama wewe aliye na mazuri na mabaya. Ukimtafuta kwa uhalisia, kwa hekima na subira, unaweza kupata mwenza wa kukusaidia kujenga maisha yenye furaha. Usitafute mkamilifu, bali tafuta mtu wa kweli.
