Ulega Ahamasisha Wananchi Tambani Kujitokeza Kupiga Kura Oktoba 29

 

MKURANGA, Pwani – Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mkuranga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Ulega, amewataka wananchi wa Kijiji cha Tambani kujitokeza kwa wingi katika 

Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, na kuwachagua wagombea wa chama hicho kwa nafasi zote.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Kijiji cha Mkonga, Ulega alisema ushindi wa CCM utawezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya kijamii katika eneo hilo.

Ulega alieleza kuwa serikali inaendelea kuboresha huduma za afya, na akawahakikishia wananchi kuwa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Tambani utaendelezwa kwa kasi. Aidha, aliahidi kupigania kupunguzwa kwa gharama za umeme ili kuwawezesha wakazi wa eneo hilo kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa tija.

“Tukichagua wagombea wa CCM katika nafasi ya Rais, Mbunge na Diwani, tutakuwa tumeelekeza nguvu katika dira moja ya maendeleo. Tambani itasonga mbele,” alisema Ulega.

Kwa upande wake, Mgombea Udiwani wa Kata ya Tambani, Dickson Mwaijibe, aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kuhakikisha wanawachagua wagombea wa CCM, akisema chama hicho kimejipanga kusukuma maendeleo katika kata hiyo.

Uchaguzi Mkuu unatarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, nchini kote, ambapo wananchi watapiga kura kuwachagua viongozi wa ngazi za udiwani, ubunge na urais.