Mwanza. Uthubutu mdogo wa kuomba mkopo katika taasisi za kifedha, pamoja na kutokuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotolewa na Serikali, umetajwa kuwa sababu inayowafanya vijana kushindwa kuaminika kupata mikopo na mitaji ya kuanzisha biashara zao.
Kauli hiyo imetolewa jana Jumamosi, Oktoba 25, 2025 na Msajili wa Asasi na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs), Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Yusuph Omollo wakati akifunga mafunzo ya vitendo kwa vijana wajasiriamali 90 kuhusu kilimo biashara, ujuzi wa kidijitali na uwezeshaji wa ujasiriamali.
Omollo amesema vijana wengi hushindwa kusaidiwa fedha kwa ajili ya kupata mitaji ya kuanzisha biashara kwa kutoshirikisha familia, taasisi za kifedha na wadau wengine kuhusu walichonacho, matarajio yao na mahitaji yao ya msingi.
“Ujasiriamali ni uthubutu. Kama huwezi kuthubutu, basi siyo mjasiriamali. Unaweza kuthubutu kuomba fedha kwenye kampuni zinazokopesha, lakini pia Serikali inatoa mikopo mbalimbali. Nawasihi vijana kushirikisha mawazo yenu ya biashara kwa ndugu, jamaa na wazazi ili muweze kupata msaada wa kifedha na ushauri,” amesema Omollo.
Msajili wa Asasi za Kiraia na Mashirika yasiyo ya Kiserikali Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Yusuph Omollo akizungumza na vijana wajasiriamali 90 waliohitimu mafunzo ya kutambua fursa za kilimo biashara. Picha na Damian Masyenene
Amesema kutokana na kukosa uthubutu huo, mikopo mingi inayotengwa kwa ajili ya vijana huishia kurudishwa kwenye taasisi bila kufanyiwa kazi au kuombwa na walengwa.
“Inasikitisha kuona fedha za mikopo ya halmashauri kwa vijana (asilimia nne), wanawake (asilimia nne) na watu wenye ulemavu (asilimia mbili) zikibaki bila kutumika kwa sababu vijana wengi hawatimizi vigezo,” amesema.
Akizungumzia mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Agriinovate Tanzania, Omollo aliwataka washiriki kuyatumia maarifa waliyopata kwa vitendo ili kujiajiri na kuwaajiri wengine, akisisitiza umuhimu wa kuwasiliana na maofisa maendeleo ya jamii katika kata zao ili kufahamu vigezo vya kupata mikopo mbalimbali.
“Ni imani ya Serikali kwamba, mnapotoka hapa mtaenda kutumia vyema ujuzi huu, lakini pia msiwe wachoyo wa maarifa. Waelimishe vijana wenzenu ili wote mnufaike, maana ukilalia ujuzi ulionao, ni sawa na kuupoteza bure,” amesema Omollo.
Mwenyekiti wa Asasi za Kiraia Mkoa wa Mwanza, Jimmy Luhende amewataka vijana kujiamini, kuwa nadhifu na kuwa na malengo ya wazi ili waweze kuaminika na wadau watakaounga mkono mawazo yao ya kibiashara.
“Mtaji wa kwanza ni kuaminiwa. Ukipewa fedha au mkopo, hakikisha unarudisha kwa wakati. Usijioneshe kama mtu wa shaka. Mwonekano wako ni imani, na ukiwa na nidhamu katika biashara, utapata msaada zaidi,” amesema Luhende.
Ofisa Miradi wa Shirika la Vijana Tanzania (TYC), Edward Lalika amesema mradi huo wa majaribio wa mwezi mmoja umejikita katika kuwajengea uwezo vijana 90 wa Ilemela kutambua fursa za biashara, kutumia mbinu za kidijitali na kuendeleza ubunifu katika kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi.
Amesema mafunzo hayo, yanayotekelezwa kwa ushirikiano wa Agriinovate Tanzania na Unsung Heroes Foundation ya Poland, yamewapatia washiriki ujuzi wa kuongeza thamani ya mazao, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), pamoja na biashara mtandaoni.
Makamu Balozi wa Poland nchini Tanzania, Jakub Trzcinski akikabidhi vyeti vya kuhitimu mafunzo ya mwezi mmoja ya fursa za biashara kwenye kilimo na ujuzi wa tehama, kwa baadhi ya vijana kutoka wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza. Picha na Damian Masyenene
“Vijana wengi wamekuwa waoga kutokana na historia ya kukatishwa tamaa, lakini kupitia mafunzo haya wamepata ujasiri na uelewa mpya wa fursa zilizopo kwenye kilimo biashara na teknolojia ya kisasa,” amesema Lalika.
Mmoja wa washiriki, Halima Athumani mkazi wa Buswelu amesema mafunzo hayo yamempa matumaini mapya ya kujiajiri badala ya kutegemea ajira.
“Nimehitimu chuo na kupitia mafunzo haya nitaanzisha biashara yangu. Naomba vijana wenzangu tuchangamkie fursa zinazotolewa na kutumia maarifa tuliyopata,” amesema Halima.
Mjasiriamali Samweli Yohana amesema mafunzo hayo yamemsaidia kupata mbinu bora za kukuza biashara.
“Nimejifunza namna ya kukuza biashara yangu na kupata mitaji. Ushauri wangu ni kwa vijana kujiuliza na kufuatilia fursa zinapotangazwa, kwani ndizo njia za kupata ujuzi na mitaji,” amesema Yohana.
Mkurugenzi wa Unsung Heroes Foundation ya Poland, Radeck Wierzbicki amesema miaka 20 iliyopita Poland ilikuwa katika hali kama Tanzania, ikipokea misaada na elimu ya ujasiriamali, lakini sasa imepiga hatua kubwa.
“Ninaamini kupitia miradi kama hii, Tanzania nayo itapiga hatua na kuwa mfano wa kusaidia nchi nyingine baada ya miaka michache ijayo,” amesema Wierzbicki.
