Wagombea urais watakavyopishana kufunga kampeni, kupiga kura

Dar es Salaam. Pazia la kampeni za urais kwa vyama mbalimbali vya siasa linatarajiwa kufungwa katika mikoa minne tofauti, huku wagombea wa nafasi hiyo wakitarajiwa kupiga kura katika mikoa mitano.

Mikoa inayotarajiwa kushuhudiwa mikutano ya mwisho ya kufunga kampeni hizo za wagombea hao ni Mwanza, Pwani, Dar es Salaam na Iringa, kwa mujibu wa vyama 17 vilivyosimamisha wagombea wa nafasi ya urais.

Kwa mikoa ambayo wagombea wa urais kutoka vyama hivyo 17 watapigia kura siku ya uchaguzi Oktoba 29, ni Mwanza, Dar es Salaam, Tanga, Mjini Magharibi na Dodoma, kama walivyoidokeza Mwananchi.

Mkoa wa Dar es Salaam umeonekana kuwa chaguo la vyama vingi zaidi kuhitimisha kampeni zao za urais, pia ndio mkoa ambao wagombea wengi wa nafasi hiyo watapiga kura, kwa mujibu wa walivyoeleza.

Nani atafunga wapi kampeni?

Mikutano ya kampeni za kunadi sera za wagombea mbele ya wananchi itatamatishwa Oktoba 28, kutoa fursa kwa wananchi kupiga kura Oktoba 29.

Kila chama kimeweka mkakati wa eneo kitakapotamatisha safari hiyo iliyochukua takriban siku 60, sawa na miezi miwili ya kuwashawishi Watanzania.

Kwa upande wa chama tawala, CCM, kinatarajia kutamatisha kampeni zake mkoani Mwanza, eneo ambalo litatumiwa pia na chama cha ADC na Ada-Tadea.

Ukiacha vyama hivyo, chama cha TLP kimepanga kufunga pazia la kampeni zake katika Mkoa wa Pwani, kama ilivyo kwa Chama cha Wakulima (AAFP), UDP na CCK.

Vyama vya SAU, Demokrasia Makini, CUF, UMD na NRA vimepanga kufunga kampeni zake katika Jiji la Dar es Salaam.

Chama cha NLD kitafunga kampeni zake mkoani Tanga, DP mkoani Kigoma kwa mujibu wa ratiba ya INEC, huku mgombea mwenyewe akisema atafunga katika Mkoa wa Iringa.

Ukiacha vyama hivyo vilivyopanga kufunga kampeni zao siku moja kabla ya upigaji kura, Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kinatarajia kuhitimisha kampeni zake Oktoba 27,jijini Dar es Salaam.

Wapi wagombea watapigia kura?

Mgombea urais wa DP, Abdul Mluya, amesema atapiga kura Mtaa wa Mtakuja, Kata ya Vingunguti jijini Dar es Salaam, wakati Salum Mwalimu akipiga kura Jimbo la Kikwajuni, Mjini Unguja.

Kwa upande wa Swaum Rashid, anayewania urais kwa tiketi ya chama cha UDP, atapiga kura Kata ya Mzinga, Jiji la Dar es Salaam, wakati mgombea urais wa chama cha NRA, Hassan Almas, atapiga kura Chamanzi, Mbagala, Dar es Salaam.

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wakulima (AAFP), Kunje Ngombale-Mwiru, atapiga kura Ubungo, Dar es Salaam.

Naye mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha NLD, Hassan Doyo, amesema atapiga kura Kata ya Kabuku, Kijiji cha Kwedikwazu Mashariki, wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga.

Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Richard Lyimo, amesema mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Yustas Rwamugira, atapiga kura katika Kata ya Vingunguti, jijini Dar es Salaam.

Wakati Rwamugira akipiga kura mkoani Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Ada-Tadea, Juma Khatib, amesema mgombea urais wa chama hicho, Georges Bussungu, atapiga kura eneo la Ikiguru, Misungwi mkoani Mwanza.

Sambamba na hao, mgombea urais wa Chama cha Demokrasia Makini, Coaster Kibonde, ameliambia Mwananchi kuwa atapiga kura katika kituo cha Shule ya Msingi Miogoni iliyopo Sinza Vatican, wilayani Ubungo, Dar es Salaam.

Meneja kampeni wa mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Yusuph Mbungiro, amesema mgombea urais wa chama hicho, Samandito Gombo, atapiga kura eneo la Kitunda, wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Kwa upande wa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan atapiga kura Chamwino mkoani Dodoma, kwa kuwa ndilo eneo alikorekebishia taarifa zake za mpigakura Mei 17, mwaka huu.

Ilivyokuwa, wanavyosema wagombea

Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Samia ameandika rekodi ya kufanya mikutano mingi zaidi ya kampeni, ukilinganisha na wagombea wa nafasi hiyo wa vyama vingine.

Samia amefanya zaidi ya mikutano 110 ya kampeni katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, akifuatiwa na Salum Mwalimu wa Chaumma), aliyefanya mikutano chini ya 100.

Ukiacha Mwalimu, wagombea wa vyama vingine wamefanya mikutano chini ya 50 kila mmoja, huku baadhi wakitumia mbinu ya kwenda vijiweni kuomba kura badala ya kufanya mikutano ya hadhara.

Katika mikutano yake ya kampeni za urais, Samia amesisitiza umuhimu wa wananchi kumpigia kura kwa wingi ili kukiheshimisha chama hicho na Tanzania kwa ujumla wake.

Amesema wananchi wanapaswa kukichagua chama hicho kwa kuwa mgombea wake tayari ana uzoefu wa kuongoza, huku akiwapiga kijembe wapinzani wake kuwa wakipewa nafasi watatumia muda mwingi kujifunza.

Samia amesisitiza kuwa kupewa ridhaa kwa chama hicho ni msingi wa kulinda amani na kuuheshimisha utu wa Mtanzania kwa kuboresha huduma mbalimbali, zikiwemo za afya, maji na nishati.

Akizungumzia kampeni zake, mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha NRA, Almas Kisabya, amesema kampeni zake zimepata mapokezi makubwa na alieleweka kutokana na kile alichoeleza, akibainisha kuwa alizifanya kimkakati na kuanza kwa kishindo.

“Tunaamini kwa jinsi tulivyofanya kampeni, kwa tulivyozunguka nchi nzima na kampeni tulizozifanya visiwani, bara na maeneo yote, tunajivunia mambo mawili,” amesema.

Amesema mambo wanayojivunia ni kufanikiwa kutoa elimu ya kutosha kwa Watanzania kiasi cha kujua mipaka na mamlaka ya nchi yao.

Jambo lingine wanalojivunia, kwa mujibu wa mgombea huyo, ni kupata mapokezi makubwa katika mikutano yao ya kampeni, jambo linaloashiria wananchi watafanya uamuzi sahihi siku ya uchaguzi, Oktoba 29 mwaka huu.

Amesisitiza kuwa katika kuhitimisha kampeni hizo hatakuwa na kazi kubwa zaidi ya kuwakumbusha wananchi kile alichowaahidi katika siku zote alizozunguka huku na kule.

“Tumeshafanya kazi kubwa, tunajiamini, kilichobaki tunawaachia wananchi wenyewe kuamua. Kazi imebaki kwa wananchi, na kwa kuwa wametuelewa, hatuna mashaka watatupa nafasi zaidi,” amesema Almas.

Mgombea urais wa UDP, Saum Rashid ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho amesema wamejipanga kuzitumia siku za mwisho za kampeni kujihakikishia ushindi kwa maeneo yote waliyosimamisha wagombea, ikiwemo urais.

Amesema wanaamini ushindi kwa sababu wamezunguka maeneo mbalimbali kunadi sera zao, wananchi wamewaelewa, hivyo hawana mashaka na uamuzi wa Watanzania itakapofika siku ya uchaguzi.

“Tunaamini tunashinda kwa sababu tunaona mwaka huu kumekuwa na tofauti katika usimamizi wa uchaguzi wenyewe. Tumeona tuna tume huru, sheria imara, na mchakato wa upatikanaji wa wagombea umeenda vizuri.

“Kwa namna tunavyoendelea, changamoto kwa asilimia kubwa ni rasilimali fedha kwa namna wagombea walivyojipanga. Kwa hiyo, tunatarajia kwa siku zilizobaki, kwenye maeneo tuliyojipanga vizuri tutashinda,” amesema.

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia Makini, Coaster Kibonde, amesema tayari chama chake na yeye binafsi wamejipanga kuhitimisha kampeni.

Kwa kuwa anatambua kampeni za kuhitimisha zinakuwa na kishindo, ameeleza kuwa amejipanga kuhakikisha anatoa majumuisho ya yale aliyoyaahidi katika mikutano yake ya kampeni siku zilizopita.

Amesema katika mkutano huo wa kufunga kampeni, amejipanga kuhakikisha anazungumza kwa namna itakayojenga ushawishi kwa wananchi wamchague na hatimaye atangazwe kuwa mshindi.

“Kampeni za lala salama zinakuwa na kishindo, na tumekuwa tukipata mapokezi makubwa kutoka kwa wananchi, tumesikilizwa na kueleweka,” ameeleza.

Katika msisitizo wake kuhusu hilo, amesema ana uhakika wa kwenda kushinda katika uchaguzi huo kwa kuwa ana vipaumbele na ahadi zinazokubalika na wananchi.

“Mimi siku zote nimekuwa na uhakika wa kwenda kushinda. Nakwenda kushinda kwa kuwa vipaumbele na ahadi zetu zinawagusa moja kwa moja wananchi. Kupitia hizo, tunaamini kwamba wananchi wametukubali na watakwenda kutuchagua Oktoba 29,” amesema Kibonde.