Wananchi watakiwa kulinda amani kuelekea uchaguzi mkuu

Dar es Salaam. Wito wa kulinda amani kama nguzo ya maendeleo ya uchumi, ustawi wa familia, na mustakabali wa Taifa umetolewa kwa Watanzania huku viongozi kutoka taasisi za dini, Serikali na sekta binafsi wakisisitiza kuwa bila amani, hakuna shughuli yoyote ya kijamii au kiuchumi inayoweza kusonga mbele.

Msisitizo wa amani umetolewa katika kongamano la wanawake ulioandaliwa na Umoja wa Wanawake Mkoa wa Dar es Salaam, kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Akizungumza leo Oktoba 26, 2025 katika kongamano hilo, Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, David Misime amewatoa hofu wananchi kuwa hali ya usalama nchini ni shwari, huku akiwataka Watanzania kuendelea na shughuli zao za kila siku bila wasiwasi.

“Tunafanya biashara ndogondogo kukaanga maandazi, kuuza vitumbua, kufungua genge kwa sababu tuna amani. Ndege uliyenaye mkononi ni bora kuliko tisa walioko juu ya mti. Shikilia amani hiyo inayokuwezesha kufanya kazi zako kwa utulivu,” amesema Misime.

Amesema Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kulinda wananchi, mali zao na kuhakikisha kila mmoja anashiriki uchaguzi katika mazingira salama.

“Hakuna tishio lolote la usalama nchi iko salama kabisa,  Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan, tayari amesema hakuna tishio, na sisi vyombo vyake tumeweka mikakati yote kuhakikisha wananchi wanalindwa,” amesema Misime.

Amewataka wananchi hasa kina mama kutokuwa na wasiwasi na taarifa za uongo zinazozunguka mitandaoni, badala yake wazingatie taarifa rasmi kutoka kwa Serikali na Jeshi la Polisi.

“Yale yanayozunguka mitandaoni yasiyokuwa na ukweli, yafuteni kabisa. Yanaweza kutuchonganisha, kutugombanisha na kuharibu amani tuliyonayo sikilizeni kauli za Amiri Jeshi Mkuu na Jeshi la Polisi pekee,” amesisitiza.

Misime amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la kupiga kura, akibainisha kuwa askari watakuwa mitaani kulinda usalama wa wapiga kura na mali zao.

“Jitokezeni kwa wingi mkapige kura, halafu mrudi nyumbani kwa amani. Polisi tutakuwa mitaani, tukiwa na magari yetu, kuhakikisha kila mmoja wenu yuko salama, mkituona, jua tunakulinda wewe, mume wako na watoto wako,” amesema.

Amewaomba wanawake kuendelea kuwa walinzi wa amani ndani ya familia zao kwa kutoa elimu na kuhimiza maadili mema kwa watoto na waume zao.

Misime amesema shughuli nyingi za kiuchumi kama biashara za Kariakoo, bodaboda, na machinga zinawezekana kwa sababu ya utulivu uliopo, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha hali hiyo inaendelea.

Kwa upande wake, Khadija Mjata ambaye ni mtaalamu wa masuala ya fedha na benki, amesema maendeleo ya kiuchumi hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa amani.

“Bila amani, uchumi wetu hauwezi kufika popote. Hata mimi nafanya kazi katika benki ya kimataifa inayomilikiwa na wawekezaji kutoka nje. Wanakuja kuwekeza Tanzania kwa sababu wanaamini ipo salama,” amesema Khadija.

Amesema ustawi wa Taifa si jukumu la Serikali pekee, bali ni wajibu wa kila raia kulinda utulivu unaowezesha biashara na ajira kuendelea.

“Mama ntilie, mfanyabiashara wa nguo, au mtu yeyote anayejitafutia kipato wote wanahitaji amani ili wafanye kazi zao. Tukipoteza amani, hakuna biashara, hakuna ajira, hakuna maendeleo,” amesema.

Mwenyekiti wa Wanawake wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani na Makamu Mwenyekiti wa Wanawake Jimbo la Kati, Neema Massawe, amesisitiza kuwa wanawake wana nafasi kubwa katika kulinda amani kupitia familia na jamii.

“Wanawake tunaaminika, watoto wetu wanatusikiliza, waume zetu wanatusikiliza, jamii inatusikiliza, tukiongea kuhusu amani, watu watasikia. Hivyo tusichoke kuhubiri amani majumbani na makanisani,” amesema.

Massawe amesema amani ndiyo inayoleta furaha, maelewano ya kidini, na ushirikiano wa kijamii. Leo wanakula  pamoja Wakristo na Waislamu wanacheka, kwenda kanisani na msikitini, watoto wao wanaenda shule bila wasiwasi wakipoteza amani, wamekwisha.