Wanawake wanaogopa sana kuolewa na watoto wa mama au labda tuseme wanawake hawapendi kabisa kuwa uhusiano na watoto wa mama. Mtoto wa mama ni mwanaume ambaye yupo karibu sana na mama yake kiasi kwamba licha ya kuwa mtu wazima lakini bado anataka ule uhusiano na mama yake uwe kama ilivyokuwa miaka ya nyuma alipokuwa mdogo jambo ambalo haliwezekani.
Kabla ya kuwa watu wazima wanaume wote tulikuwa watoto, tulikuwa hatujiwezi kwa lolote, tunaishi kwenye nyumba zilizojengwa kwa nguvu za wazazi wetu, tunakula chakula kilichotafutwa kwa jasho la wazazi wetu, elimu, afya, nguo, kila kitu tulikipata kwa gharama za wazazi wetu, nishukuru kwa kukujulisha taarifa hizi muhimu ambazo ulikuwa huzifahamu.
Hata hivyo, mara nyingi katika makuzi yetu mzazi ambaye tunakuwa karibu naye kipindi chote ni mama. Mama humfanyia mtoto kila kitu cha karibu zaidi ya ilivyo kwa baba anavyomfanyia mtoto, kwa maana hiyo, moja kwa moja ukaribu wa mtoto na mama huwa mkubwa kuliko kawaida, mama anakuwa rafiki mkubwa kwa mtoto. Ikiwa kwa mtoto wa kike, mtoto na mama wanakuwa kama mtu na shosti yake, ikiwa kwa mtoto wa kiume mtoto anakuwa mtoto wa mama.
Wasichopenda wanawake kutoka kwa watoto wa mama ni kwamba mwanaume mtoto wa mama hawezi kufanya kitu chochote bila kumshirikisha mama. Mtoto wa mama anaweza akapanga na mke wake wafungue duka, wakakubaliana kila kitu, lakini kabla ya utekelezaji haujaanza mtoto wa mama akaja na mawazo tofauti, akasema tusifungue duka. Kwanini? Kwa sababu mama kasema hivi na vile.
Hatusemi usiombe ushauri kwa wazee wako lakini vitu havifanyi kazi namna hiyo, kama mama anakupa ushauri mzuri kuna ulazima gani kuufikisha kwa mkeo ukiwa na jina la mama? Unaweza kuuchukua na kuufanya wako, kama ni ushauri wa maana mwenzio atauzingatia.
Lakini wewe leo unasema ushauri huu umetoka kwa mama, kesho ushauri huu umetoka kwa mama, mwenzio anaweza kujiuliza kwahiyo mimi nafasi yangu iko wapi kama kila tunachokipanga kinapanguliwa na ushauri wa mama? Hapo unatengeneza bomu tu kati ya mama na mkeo.
Huwezikuwa unatafuta namna ya kumuingiza mama yako kwenye kila mnachokiongea. Ukipikiwa chakula kikiwa kizuri sana lazima useme kama alichokuwa anapikaga mama, kikiwa kina hitilafu useme chumvi ipo kwa mbali, sio kama alichokuwa anapikaga mama, maisha hayako hivyo.
Na ukiwa mtoto wa mama sana unaweza kuta hata mambo yanayokuhusu wewe na mkeo unashindwa kujizuia kutokuyafikisha kwa mama. Utaweza kweli kutunza siri za familia wewe.
Halafu chunguza sana, migogoro mingi ya mama mkwe na mkwewe ina sababishwa na mwanaume kuwa mtoto wa mama. Mungu atuepushe na kuwa watoto wa mama.
