Mwanza. Wasimamizi na wasaidizi 2,870 katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza wameanza mafunzo ya siku tatu ya usimamizi wa uchaguzi mkuu, huku wakikumbushwa jukumu walilokabidhiwa ni la kikatiba linalohitaji uelewa wa sheria, weledi na utendaji haki.
Akifungua mafunzo hayo leo Jumapili Oktoba 26, 2025 Msimamizi wa uchaguzi Ilemela, Herbert Bilia amesema yanahusisha wasimamizi watakaosimamia vituo 944 katika kata 19.
Amesema washiriki hao ndio watakaoongoza shughuli ya kupiga kura, kuhesabu kura na kuwasilisha matokeo ya awali ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.
“Kuanzia siku ya uteuzi wenu mnakua watumishi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC). Hivyo mnatakiwa kutekeleza majukumu yenu kwa kuzingatia katiba, sheria ya uchaguzi na kanuni zote bila kupendelea upande wowote,” amesema.
Amesema mafunzo hayo si ya kawaida bali ni sehemu ya maandalizi ya kulinda amani na demokrasia nchini, kwa sababu hatua zote za uchaguzi zinaanzia katika kituo cha kupigia kura ambacho wasimamizi ndio walezi wake.
“Kabla ya siku ya uchaguzi mnatakiwa kusoma na kuelewa nyaraka zote mlizopewa, ikiwemo Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Sheria ya Uchaguzi namba moja ya 2024, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi namba mbili ya 2024 pamoja na kanuni na miongozo ya uchaguzi. Mnapaswa kutekeleza kila hatua kwa rejea sahihi ili kuzuia migogoro na malalamiko,” amesema.
Mkufunzi wa mafunzo, Isaya Hosea akizungumza na washiriki wa uchaguzi wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wasimamizi wa vituo na wasimamizi wasaidizi.
Ameongeza kuwa wajibu wa msimamizi wa kituo si tu kuwepo kituoni siku ya uchaguzi, bali kuhakikisha maandalizi yote yanafanyika kwa usahihi ikiwemo kuhakiki vifaa, kupanga mazingira ya kituo, na kuhakikisha wapiga kura wanapewa huduma bila ubaguzi.
Bilia amesema wasimamizi hao wanapaswa kujiepusha na vitendo vya upendeleo, vitisho au lugha za kukera, na badala yake walinde haki ya msingi ya kila mpiga kura.
“Mnapaswa kufika mapema kabla ya saa 1:00 asubuhi, kupanga meza, kukagua sanduku la kura na kuhakikisha mazingira yako tayari. Vilevile, mnapaswa kuhifadhi na kurejesha vifaa vyote vya uchaguzi baada ya zoezi kukamilika.”
“Natarajia mtafanya kazi kwa uadilifu, mkisimamia amani na kura za wananchi kwa uaminifu. Uchaguzi huu ni wa Watanzania wote, hivyo ninyi ndio nguzo ya kuhakikisha haki inatendeka kuanzia kituoni.”
Mkufunzi wa mafunzo hayo, Isaya Hosea amesema mafunzo hayo yanatarajiwa kujenga uwezo wa washiriki kumudu changamoto na kuongoza vituo kwa weledi.
Mmoja wa washiriki, Leonard Mwita amesema baada ya mafunzo hayo ataweza kusimamia vituo kwa uadilifu na kuhakikisha hakuna uvunjifu wa sheria.
Naye Zainabu Shija amesema dhamira yake ni kuhakikisha kila mpiga kura atakayefika kituoni anapata haki bila usumbufu, huku Fatuma Kilimali akisema mafunzo hayo yamemwandaa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki na uwazi kama ilivyo dhamira ya tume.
