Wasimamizi wa uchaguzi watakiwa kutenda haki

Simiyu. Wasimamizi wa uchaguzi wametakiwa kuhakikisha wanasimamia uchaguzi mkuu kwa uwazi, haki na kushirikisha vyama vyote vya siasa vilivyoko kwenye mchakato huo ili kujenga imani kwa wananchi.

Wito huo umetolewa  leo Jumapili Oktoba 25, 2025 na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Maswa Mashariki na Jimbo la Maswa Magharibi, Julius Ikongora wakati akifungua mafunzo ya wasimamizi wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura.

Ikongora amesema jukumu kubwa la wasimamizi wa vituo ni kuhakikisha kila hatua ya uchaguzi inafanyika kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Maswa Mashariki na Jimbo la Maswa Magharibi,Julius Ikongora akifungua mafunzo kwa wasimamizi wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura wilaya ya Maswa.Picha na Samwel Mwanga

“Nasisitiza suala la kutenda haki, kutoshabikia upande wowote na kuhakikisha vyama vyote vya siasa vinashirikishwa katika kila hatua ya mchakato wa uchaguzi. Uadilifu wenu ndio utakaosaidia kuimarisha amani na uaminifu wa matokeo,” amesema.

Ikongora amesema wasimamizi wanapaswa kuwa mfano wa nidhamu na weledi katika vituo vyao, kwa kuwa, wao ndio taswira ya tume katika macho ya wananchi.

“Kosa dogo la msimamizi linaweza kuibua taharuki, hivyo kila mmoja ahakikishe anafuata maelekezo, taratibu na kutoa huduma kwa wapiga kura wote kwa usawa,” amesema.

 Ikongora amewataka wasimamizi hao kusoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuizingatia kila wanapotekeleza majukumu yao ili kuhakikisha wanaheshimu misingi ya demokrasia na utawala wa sheria.

“Wasimamizi wa uchaguzi wasome Katiba, wazingatie taratibu na washirikishe vyama vyote kwa uwazi na haki. Hayo ndiyo yataifanya kazi yetu iheshimiwe na matokeo yakubalike na wote,” amesema.

Wasimamizi wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura wilaya ya Maswa wakiwa kwenye mafunzo.Picha na Samwel Mwanga

Mwajabu Rashid, msimamizi msaidizi kutoka Kata ya Buchambi amesema mafunzo hayo yamekuwa msaada mkubwa kwao kuelewa taratibu za kupokea na kuhesabu kura.

“Tulikuwa hatujui baadhi ya hatua muhimu, kama jinsi ya kushughulikia malalamiko ya mawakala, lakini sasa tumepewa mwongozo wa wazi kabisa,” amesema.

Bugumba Juma, msimamizi wa kituo kutoka Kata ya Senani amesema mafunzo hayo yamewajengea uelewa kuhusu umuhimu wa kuepuka upendeleo na kuhakikisha vyama vyote vinapata haki sawa.

“Tumejifunza kuwa ushirikiano na mawakala ni muhimu sana. Haki na uwazi ni silaha pekee ya kudumisha amani katika uchaguzi,” amesema.

John Kubebeka, mmoja wa wasimamizi wa vituo kutoka Kata ya Zanzui amehimiza INEC iendelee kuwa karibu nao ili kuongeza uelewa na kuondoa makosa ya kiufundi siku ya kupiga kura.

“Tunajisikia kuaminiwa na tume, na tutaenda kufanya kazi kwa weledi na uadilifu mkubwa,” amesema.