Dar es Salaam. Mashahidi 17 na vielelezo 24 vinatarajiwa kutolewa Mahakamani katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini na Methamphetamine zenye jumla ya uzito wa kilo 447, inayowakabili raia wanane wa Pakistan.
Washtakiwa hao ni Mohamed Hanif (50), Mashaal Yusuph (46), Imtiaz Ahmed (45), Tayab Pehilwam (50) maarufu kama Tayeb, Immambakshi Kudhabakishi (55).
Wengine ni Chandi Mashaal (29), Akram Hassan (39) na Shehzad Hussein (45), wote wakiwa raia wa Pakistan.
Washtakiwa hao wanakabiliwa kesi ya uhujumu uchumi namba 395 ya mwaka 2025, yenye mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini na Methamphetamine katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mashahidi hao wanatarajia kutoa ushahidi wao, Mahakama Kuu, pindi kesi hiyo ya kusafirisha dawa za kulevya itakapopangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa, baada ya washtakiwa hao kusomewa maelezo ya Mashahidi na vielelezo (Commital Proceedings) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washtakiwa hao wamesomewa maelezo ya mashahidi na vielekezo (Commital Proceedings) leo, Jumatatu Oktoba 27, 2025, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya upelelezi wa shauri hilo kukamilika.
Kabla ya usomwaji wa maelezo hayo, Mahakama ilitafuta mkalimani anayetafsiri lugha ya Kiingereza, Kiswahili kwenda lugha ya Urdu ambayo inatumika nchini Pakistan. Kutokana na washtakiwa hao kutojua lugha ya Kiingereza na Kiswahili.
Mkalimani huyo Salma Mohameda raia wa Pakistan alitafsiri maelezo ya mashahidi na vielelezo kutoka lugha ya Kiswahili kwenda lugha ya Urdu na wakati mwingine kutoka lugha ya Kiingereza kwenye lugha ya Urdu.
Wakili wa Serikali, Titus Aron ameieleza mahakama hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, wakati akiwasomea washtakiwa maelezo ya mashahidi na vielelezo.
Wakili Aron alidai vielelezo 13 ni vya maandishi na vielelezo 11 ni nyaraka halisi ikiwemo hati ya ukamataji mali, ripoti kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, kiasi cha dawa kilichokamatwa kwa washtakiwa hao, maelezo ya onyo ya washtakiwa wote na fomu ya uwasilishaji wa sampuli kwenda kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
Aron baada ya kueleza hayo aliwasomea upya mashtaka yao na kisha maelezo ya mashahidi na vielelezo.
Raia nane wa Pakistani wakiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo. Hata hivyo kesi hiyo kwa sasa imehamishwa Mahakama Kuu kwa ajili usikilizwaji. Picha na Hadija Jumanne.
Na baada ya hapo aliwasomea idadi ya mashahidi na miongoni mwa mashahidi hao ni Seleman Mbwambo, ambaye ni Ofisa kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya nchini (DCEA), ambaye ndiye aliyewakamata washtakiwa hao kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama wakati wakiwa doria katika bahari ya Hindi.
Ofisa huyo aliwakamata washtakiwa hao wakiwa na jahazi lenye shehena ya dawa hizo, wakati akiwa katika doria bahari ya Hindi, wakiwa njiani kuelekea Mafia.
Inadaiwa kuwa wakiwa umbali wa maili 50 kutoka bandari ya Dar es Salaam, waliona chombo kikielea baharini na baada ya kukipima kwa kutumia rada walibaini ni jahazi na kuanza kulifuatilia.
Mbwambo akiwa na maofisa wenzake sita wakiwa katika boti maalum walifuatilia jahazi hilo na wakati wakikaribia eneo hilo walibaini jahazi hilo lilikuwa limezima taa na ndani yake kulikuwa na watu.
“Hata hivyo nahodha wa boti hiyo alimuonyeshea ishara nahodha wa jahazi ili asimame lakini ilishindika na ndipo mmoja wa askari waliokuwa doria kufyatua risasi hewani kwa lengo ya kumtaka nahodha wa jahazi hilo asimame lakini alikaidi,” alidai wakili Aron wakati akisoma maelezo ya shahidi huyo.
Kutokana na kukaidi kwa amri hiyo, boti hiyo ilianza kulifukuza jahazi na kufanikiwa kulikamata ambapo walikuta raia nane wa Pakistan wakiwa ndani ya jahazi hilo.
Raia hao walikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi na ndani ya jahazi hilo la mbao kulikuwa na mifuko mingi ya salfeti, hivyo Mbwambo alijadiliana na maofisa wenzake kuwapeleka watu hao eneo la wazi kwa ajili ya kufanya upekuzi.
“Niliwasiliana na mkuu wangu wa kazi na kumpatia taarifa na kuomba nitafutiwe mkalimani kwa sababu raia hao nane wa Pakistan hawajui Kiingereza, isipokuwa nahodha wa jahazi hilo ndio anajua kidogo lugha ya Kiingereza,” alidai Aron wakati akisoma ushahidi wa Seleman.
“Nahodha wa chombo chetu aliongoza jahazi hilo hadi sehemu ya nchi kavu, huku watu hao wakiendelea kuwa chini ya ulinzi,” alidai Wakili Aron.
Alidai kuwa maofisa hao wa DCEA walitoka eneo hilo walikokamata washtakiwa hao kwenda Dar es Salaam saa 5 usiku na alimuomba mkuu wake wa kazi amuongezee maofisa wengine na pia aliomba kutafutiwa mkalimani ili watakapofika Dar es salaam wawepo na pia aliomba atafutiwe shahidi huru atakayeshuhudia upekuzi.
Alidai kuwa walitembea usiku kucha majini kutokana na bahari kuchafuka na jahazi hilo kunesanesa na kuhatarisha usalama wa maofisa hao.
Hata hivyo, Novemba 25, 2024 walifika Dar es Salaam saa mbili asubuhi na upekuzi ndani ya jahazi hilo lililokuwa na bendera rangi ya kijani na nyeusi, ulianza saa 5 asubuhi na kukamilika saa 11 jioni.
Katika upekuzi huo, walikuta kontena ndogo za plastiki 409 zikiwa zimefungwa kwa nailoni na ndani yake kukiwa na chengachenga zinazo dhaniwa kuwa ni dawa za kulevya.
Kontena hizo zilikuwa na rangi ya kijani, nyeupe, nyeusi, rangi ya chungwa, njano pamoja na pakiti 33 zenye picha ya korosho kwa juu ambazo ndani yake zilikuwa na chengachenga za unga unaodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya.
Waomba kubadilishiwa gereza
Wakati huohuo, washtakiwa hao wameomba kubadilishiwa gereza kwa madai walipokuwa awali, gereza la mahabusu Keko walikuwa wanapata maji ya kutosha na hivyo kuwafanya waweze kufanya ibada (kuswali) bila kikwazo.
Washtakiwa hao wamedai kuwa baada ya kuhamishiwa gereza la mahabusu Segerea wamekuwa hawafanyi ibada kikamilifu kutokana na changamoto ya maji.
Vilevile, Mohamed Hanif (50) alidai anaumwa miguu na mgongo na kwamba anaomba kuonana na daktari ili aweze kupatiwa matibabu.
Washtakiwa baada ya kueleza hayo, hakimu Nyaki aliwaeleza kuwa hivi karibuni walivyoenda kufanya ukaguzi gereza la mahabusu Keko lilikuwa limejaa na ndio sababu ya wao huhamishiwa Segerea na hapo Segerea kuna maji ya kutosha.
Kuhusu suala la ugonjwa, Hakimu Nyaki alimueleza mshtakiwa afuate utaratibu ili aweze kutibiwa kwa kuwa magereza ina utaratibu wa kuhudumia wagonjwa ambao ni mahabusu.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Nyaki aliwaambia washtakiwa hao kuwa kesi yao ameihamishia Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji na wakati wakisubiri kupangiwa tarehe kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi, washtakiwa hao watakuwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.
Washtakiwa wanadaiwa Novemba 25, 2024 katika eneo la Navy lililopo Kigamboni wilaya ya Kigamboni, wanadaiwa kusafirisha kilo 424.77 za dawa za kulevya aina ya Methamphetamine.
Pia siku na eneo hilo, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina heroini, zenye uzito wa kilo 22.53, kinyume cha sheria.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Januari 9, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi.
Hata hivyo, kwa muda wote huo washtakiwa hao walikuwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.
