‘Dk Manguruwe’ adai kupungua uzito kutokana na upelelezi kutokamilika

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40) maarufu kama Dk Manguruwe, anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, ameieleza Mahakama kuwa amepungua uzito wa mwili wake kutokana na upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili kutokukamilika.

Mshtakiwa huyo ametoa madai hayo leo Jumatatu, Oktoba 27 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati kesi yake ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Mkondya na mwenzake, Rweyemamu John (59), ambaye ni Mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, wanakabiliwa na mashtaka 28 yakiwemo ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha linalomkabili Mkondya peke yake.

Hata hivyo, John ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, yupo nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba dhamana Mahakama Kuu na pia hana mashtaka ya kutakatisha fedha.

“Mheshimiwa hakimu, mimi nimekuwa nusu mtu, mwanzoni nilikuwa na kilo 100 lakini sasa nimepungua uzito wa mwili wangu na kilo 50 na usheee hivi….natamani nimalizane na watu wanaonidai,” alidai Mkondya mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu, anayesikiliza shauri hilo.

“Naomba watu wanaonidai muwaonee huruma kwa kukamilisha upelelezi kwa haraka kwa sababu mimi nipo ndani na mali zangu zimekamatwa, hivyo naomba kama tunaweza tumalizane kwa sababu wananidai, hivyo mimi na wao wote tunateseka” amedai mshtakiwa Mkondya.

Kwa upande wake mshtakiwa wa John amedai kuwa kama mshtakiwa wa kwanza amekiri kosa lake kwa nini yeye bado yupo kwenye kesi hiyo.

“Mheshimiwa hakimu, kama mshtakiwa wa kwanza ameshakiri kosa lake, sasa kwa nini mimi bado nipo kwenye hii kesi? Wakati sihusiki? Amehoji mshtakiwa John.

Awali, wakili wa Serikali Winniwa Kasala alidai kuwa shauri hilo limeitwa kwa ajili ya kutajwa na wapo hatua ya mwisho kukamilisha upelelezi.

“Mheshimiwa hakimu, ndani ya wiki hii DPP atatoa kibali kwa ajili ya Mahakama hii kusikiliza kesi hii, hivyo kutokana na hali hiyo tunaomba tarehe nyingine ili kukamilisha upelelezi huu,” alidai Wakili Kasala.

Kasala baada ya kueleza hayo, hakimu Magutu alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 10, 2025.

Mkondya anaendelea kusalia rumande kutokana na mashtaka yanayomkabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa Mahakamani hapo Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 31523 ya mwaka 2024.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kati ya mashtaka hayo 28; mashtaka 19 ni ya kuendesha biashara ya upatu na mashtaka tisa ni ya kutakatisha viwanja.

Katika moja ya mashtaka hayo kuendesha biashara ya upatu, washtakiwa wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023, jijini Dar es Salaam, walitenda makosa hayo.

Inadaiwa kuwa Mkondya akiwa kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo na John akiwa Mkaguzi wake waliendesha biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu watapata pesa mara mbili hadi tatu kama faida zaidi ya waliyotoa.

Washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia kiasi cha Sh92.2milioni kutoka kwa watu 19 tofauti ambao walitoa kiasi tofauti cha fedha kwa kuwaahidi kuwa watapata faida mara mbili, hadi tatu ya fedha walizotoa.

Katika mashtaka 9 ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya pekee yake, inadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023 akiwa katika mkoa wa Dar es salaam na akiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni hiyo alijipatia jumla ya viwanja tisa vilivyopo katika kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe.

Pia, Mkondya anadaiwa kujipatia viwanja hivyo huku akijua viwanja hivyo ni mazalia ya makosa tangulizi ya kuendesha biashara ya upatu.