Dar es Salaam. Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limeendelea kutengeneza faida na kukua huku uelewa na mwamko wa watu kuwekeza ukitajwa kuwa sababu ya kuimarika kwa utendaji huo.
Haya yanasemwa wakati ambao DSE imerekodi ongezeko la mapato kwa asilimia 54 katika robo mwaka iliyoishia Septemba 30, 2025, faida baada ya kodi ikipanda kwa asilimia 74 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
Faida kabla ya kodi mwaka ulioishia Septemba 30, 2025 ilikuwa Sh1.698 bilioni ikiwa ni ongezeko kutoka Sh1.195 bilioni za mwaka uliotangulia huku faida baada ya kodi ikiwa ni Sh1.609 bilioni kutoka Sh1.191 mtawaliwa.
Hili linashuhudiwa wakati ambao idadi ya wawekezaji imekua hadi kufikia 705,156 katika mwaka ulioishia Septemba mwaka huu kutoka 605,828 waliokuwapo kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.
Ripoti ya robo ya tatu katika mwaka ulioishia Septemba mwaka huu, inatolewa wakati ambao elimu ya uwekezaji katika hisa imezidi kupamba moto mitandaoni huku watu wengi wakijitokeza kuwaelekeza wananchi namna gani wanayoweza kupata fedha bila kuwa na wasiwasi kwa kuwekeza katika hisa.
Walimu hao wa fedha wamekuwa wakiwaonesha wananchi ni maeneo gani salama ya kuwekeza, hisa za kampuni gani zina faida huku wakiwapa mbinu zinazoweza kuwasaidia kukuza mitaji yao bila kuwa na mawazo.
Ripoti hii ya DSE mbali na kuonesha ukuaji wa faida na mapato, pia inataja ukuaji wa mali kwa asilimia 17 hali inayochochewa na ukuaji endelevu wa soko na kuongezeka kwa imani ya wawekezaji.
Pia, mapato kwa wanahisa yameboreshwa, faida kwa mtaji (Return on Equity) imefikia asilimia 14 huku mapato kwa kila hisa yakiongezeka kwa Sh46 hadi Sh205.37 bilioni kutoka Sh140.96 bilioni.
Matokeo hayo yanaonesha utendaji thabiti wa DSE unaoendeshwa na kuongezeka kwa shughuli za soko, uorodheshaji mpya na juhudi endelevu za kidijitali na za uhamasishaji.
Akizungumzia suala hilo leo Jumatatu Oktoba 27, 2025, Mchambuzi wa Uchumi na Biashara, Profesa Abel Kinyondo amesema ukuaji huu ni ishara kuwa elimu ya uwekezaji katika hisa imewafikia watu kikamilifu huku imani yao katika soko ikiongezeka.
Hiyo pia ni ishara ya soko kutengamaa kwa kuwa, limekuwapo miaka mingi na kumekuwa na baadhi ya maeneo ambayo watu waliwekeza na kupata hasara hali iliyowafanya kukimbia soko.
“Ukiona watu wanarudi maana yake imani ya wawekezaji inaanza kukua. Wanarudi sasa sokoni kwa sababu wana uhakika. Wawekezaji wetu ambao wanakwenda kuchukua mitaji kwenye soko wanaanza kuwa serious kwa kuiweka katika maeneo yanayoweza kurudisha maana yake, aliyewekeza katika soko la mitaji atapata chochote na atatiwa moyo wa kuweza zaidi,” amesema.
Amesema utendaji katika soko la hisa ni wa kutegemeana mtu aweke hela mwingine achukue mtaji kwenda kuzalisha ili apate faida itakayokuja kutolewa kama gawio kwa wawekezaji ambalo litawafanya waweze kupata fedha za kununua hisa zaidi hali itakayofanya soko kutanuka.
“Soko hili ni muhimu sana, hasa likikua kwani kuna maeneo ambayo uchumi unaendeshwa na soko la hisa, kuna nchi soko la hisa ndiyo uchumi, likishuka na uchumi unaporomoka, likistawi uchumi unastawi na kila biashara kubwa inaorodheshwa katika soko,” amesema Profesa Kinyondo.
Kwa kawaida ukaji wa soko la hisa unatakiwa kuendana na uchumi lakini kwa sababu la Tanzania bado ni changa kuna vitu vingi kwenye uchumi ambavyo bado havijaporodheshwa huku akitolea mfano wa baadhi ya kampuni zilizolazimishwa kujisajili katika soko la hisa lakini hadi leo hazikuwahi kutoa gawio.
“Njia kuu za uzalishaji zikiorodheshwa unakuwa na njia pana ya kuuona uchumi wako. Natamani hilo lifikiwe lakini si kwa kulazimishana. Shida inayokuja ukilazimisha watu wakajitoa kununua hisa na wasipate chochote unawakatisha tamaa wawekezaji na kuona kuwa ni uongo,” amesema.
Mtaalamu wa uchumi na biashara, Oscar Mkude amesema ukuaji huo ni ishara kuwa watu wameanza kufikiria uwekezaji unaoweza kufanya kazi bila kuwa na muingiliano na taasisi za zinazosimamia biashara ambazo mara nyingi zimekuwa zikilalamikiwa kuwasumbua wafanyabiashara.
Katika uwekezaji huu wapo wanaosimama mmoja mmoja na wengine wanawekeza kupitia mifuko mbalimbali kama UTT ambayo imekuwa ikifanya kazi hiyo.
“Mtu akiwa na Sh200,000 kuwekeza ni ngumu lakini kupitia mifuko ni rahisi kwani UTT wanakwenda kufanya uwekezaji kule na wewe unakuwa unapata faida,” amesema.
Amesema japokuwa biashara za kawaida zinaweza kutoa faida kubwa lakini zina uwezekano wa kupata hasara tofauti na kwenye hatifungani, kuna utulivu wa soko unaovutia watu.
“Inawapa watu urahisi wa kuingia na kutoka, zote hizi zimefanya watu walione soko la hisa kuwa ni kitu kizuri. Kuna wengine wanapata faida kubwa katika uwekezaji ambao wamefanya na hii inaonesha kuwa kumekuwa na uimara kwa masoko yanayowekeza katika soko la hisa,” amesema.
Mtoa elimu ya kifedha aliyethibitishwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Charles Ligonja amesema mwamko wa watu kuwekeza katika hisa umezidi kuongezeka hasa baada ya watoa huduma walioidhinishwa kuanza kutumia mitandao ya kijamii kutoa elimu jambo linaloweka urahisi wa watu kuchukua uamuzi ya kuwekeza.
“Changamoto ni watu waliwahi kupata hasara miaka ya nyuma, kuna watu hawana imani kuwa kwenye hisa wanaweza kuweka fedha na kutengeneza faida huku wakiendelea na kazi zao. Wengine wanataka wawekeze leo, wavune kesho watu wanakosa uvumilivu na wanatamani hela waliyonayo iwasaidie kufanya kazi nyingine,” amesema.
Amesema anaamini si kila mtu anaweza kufanya biashara, lakini katika uwekezaji wa hisa mtu huweza kuweka malengo yake na kuvuna fedha katika siku za mbeleni akiwa na malengo.
